FOMU za mbio ndefu za
Uhuru, maarufu kama Uhuru Marathon, zinatarajiwa kuanza kutolewa kesho
Jumatano, huku Watanzania wakiombwa wachangie kwa gharama ndogo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, katika kuhakikisha kila mtu anashiriki kutakuwa na vituo 13 vitakavyofunguliwa kwa ajili ya kutoa fomu hizo, huku pia kukiwa na watu maalumu watakaozisambaza maofisini na hata majumbani.
Melleck alisema, fomu hizo zitatolewa kwa Sh 100,000 kwa wale watakaotaka
kukimbia mbio za kilomita tatu, Sh 2,000 mbio za kilomita tano, Sh 6,000 kwa
atakayeshiriki moja kati yam bio za kilomita 21 au 42.
“Hizi mbio ni muhimu zaidi kwa ajili ya Taifa letu, hivyo ni vyema kwa
Watanzania wote wakashiriki ili kuipigania amani iliyopo nchini mwetu.
“Tunataka kuungana na Rais Jakaya Kikwete katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya
kuleta umoja, amani na mshikamano ndani ya Tanzania na ndilo lengu la mbio
hizi.
“Bado tunaendelea kuwaomba wadhamini wajitokeze kuzidhamini, kwani nafasi bado
ipo wazi na watambue hata wao ni sehemu ya kupigania amani ya taifa letu,”
alisema Melleck.
Katika mbio hizo, zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia
mbio za kilomita 3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full
Marathon yenyewe kilomita 42.
Mratibu huyo anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi
wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia
zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile
viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili kushiriki, kwa
kudumisha amani na upendo.
“Pia tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia
watu wenye mahitaji mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha
maarufu zaidi duniani kushiriki,” anasema.
Mratibu huyo anafafanua kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha
wanafanya mambo makubwa zaidi na ambayo yataleta tija kwa taifa.
0 comments:
Post a Comment