MWANDISHI
wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye hivi karibuni alikumbwa na
madhila ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na mzazi mwenzie, ameanza kufung
uka
kidogo kidogo na kueleza kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea.
Akizungumza
kwa sauti ndogo na taratibu na gazeti hili kando ya kitanda alicholazwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanahabari huyo alieleza kushangazwa na
ujasiri na nguvu za aina yake ambazo zilimwezesha kutambaa na kujiburuza hadi
eneo la karibu ya barabara ili kuomba msaada wa kukimbizwa hospitali.
Ufoo ambaye
alionyesha dhahiri kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazozingira tukio
lake, alisema tayari alikuwa amewahakikishia polisi waliofika kumjulia hali
hospitalini hapo kwamba alikuwa akisubiri afya yake iimarike kabla hajaeleza
kwa kina kila anachokijua kuhusiana na tukio hilo.
“Alifika hapa kunijulia
hali na kuangalia maendeleo yangu afande Msangi na nikasema nitakuwa tayari
kueleza kila ninachokijua baada ya afya yangu kuimarika.
Nasikitika kuna watu
wanasema mambo wakifikia hatua ya kutaka kuonekana wananifahamu vizuri kuliko
hata ninavyojifahamu mwenyewe,” alisema akionyesha kutofurahishwa na baadhi ya
taarifa zinazoripotiwa kuhusu sakata lake.
Ufoo ambaye alifikishwa hospitalini
hapo Jumapili ya wiki iliyopita kutokana na kujeruhiwa kwa risasi na mwanaume
aliyezaa naye mtoto mmoja alisema anamshukuru sana Mungu kwa uzima alionao
sambamba na kuelezwa kupata faraja kubwa na kutiwa moyo na mwajiri wake, ndugu,
jamaa na marafiki.
Mwanahabari huyo ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa
karibu wa madaktari baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi mwilini mwake
siku chache zilizopita, amelazwa katika chumba cha peke yake ambacho ingawa
kina seti ya televisheni alisema alikuwa haruhusiwi kuiangalia kwa ushauri na
maelekezo ya madaktari.
Huku akionekana wa chini ya uangalizi mwingine wa
karibu na wa kudumu wa muuguzi ambaye muda wote wa mazungumzo haya alionekana
kuwapo katika chumba hicho, Ufoo alisema alikuwa ana mapenzi makubwa kwa mzazi
mwenzake huyo ambaye alipoteza maisha katika tukio hilo.
“Nilimpenda sana
Antheri. Alikuwa kijana mtaratibu na mpole sana. Najua kile kilichotokea ni
shetani tu na binafsi nilishasamehe alfajiri ile ile baada ya tukio lile,”
alieleza Ufoo ambaye pia alimpoteza mama yake mzazi katika mkasa huo.
TUKIO
ZIMA LILIVYOTOKEA
.
Ufoo ambaye mara kadhaa katika mazungumzo na gazeti hili
alionekana kukunja uso akiashiria kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya
bega katika mkono wake wa kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo
alipopigwa risasi ya kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti muda
mfupi baada ya Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake mzazi.
Akijaribu
kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi mwenzake huyo
alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya kazi usiku huo huo wa
tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo la Kibamba, nje kidogo ya
jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya kufika Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo
hakuzieleza, alimkariri mzazi mwenzake huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa
kujiua yeye na mtoto wao.
“Hata sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka
nyumbani Antheri alianza kwa kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na
mtoto wetu,” alisema Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea
na simulizi yake ya kusikitisha.
Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema pamoja
na kumwambia maneno hayo bado Mushi alimsisitiza kwamba waende kwa mama yake
(Ufoo) baadae warudi kumchukua mtoto wao japo Ufoo hakusema walitaka kwenda
wapi baada ya hapo.
Alisema walipofika nyumbani kwa mama yake walikwenda moja
kwa moja sebuleni na wakiwa wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na
pale ghafla Mushi akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba;
“Mama
nimeishafanya maamuzi”
Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka
maneno hayo ghafla akaingiza mkono nyuma ya suruali alikokuwa ameweka bastola
yake na kisha akaichomoa.
Katika maelezo yake Ufoo alisema baada ya kuichomoa
bastola hiyo mama yake naye alisimama na kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo
hicho kilimfanya amiminiwe risasi mfululizo.
Alisema kuona hivyo aliamua
kukimbia kuelekea jikoni ambapo Mushi alimuona na kuanza kumiminia risasi
ambayo moja ilimpata eneo la mkono wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana
titi la kulia.
Kwa mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya
kunusuru maisha yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi
nyingine kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni ambazo
zilisababisha aanguke chini
Akiendelea kusimulia, anasema ingawa alikuwa
akivuja damu nyingi, na huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema wakati akitambaa
aligeuka nyuma na akamuona Antheri akijielekeza bastola eneo la kidevu na
alipofyatua risasi alianguka chini.
“Nikiwa chini nilimuona Antheri akijipiga
risasi kidevuni na akaanguka chini, sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani
niliendelea kujiburuza ili kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo
ALIVYOJIOKOA
“Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia
kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi tumbo langu
limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba khanga ili nijifunge
kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.
Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga
na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke
mmoja.
“Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada.
Liliposimama
nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na
nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi na
kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.
“Si rahisi kuamini, yule mama
alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema
niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo.
Alisema
muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina
la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na
akakubali.
“Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia
vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.
“Wakati huo
nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa.
Nikiwa kwenye pikipiki kuna wakati
nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka katika barabara na
kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha.
Lakini nilipata ujasiri na
kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini.
Alisema anakumbuka wakati
walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya kupima uzito wa magari makubwa walikuta
barabara ikiwa imejaa magari na yeye alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita
hata nje ya barabara eneo la nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo
kijana yule alilifanya.
“Nilipofika eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza
muuguzi niliyemkuta kwamba nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba
asaidie kuokoa maisha yangu.
Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha
polisi (PF3) lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk.
Dattan ambaye tunafahamiana”
“Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na
nikamweleza yaliyonipata na mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea dripu,
na nikamsikia akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa hali niliyonayo
kama wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo zingeweza kusababisha
kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri hapo Tumbi.
Kwa mujibu wa
Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia daktari aliyekuwa akimhudumia akiomba
msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili limchukue na kumkimbiza katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili wito ambao ulijibiwa kwa maelezo kwamba lilikuwa halina
mafuta.
Majibu hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe
kuletewa gari la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na muda
mfupi baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa Muhimbili.
Alisema
wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa akipatwa na maumivu
makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa ikipanda matuta ya barabarani
na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza pumzi na kuishiwa nguvu.
0 comments:
Post a Comment