MAELEZO YA SERIKALI JUU YA HOJA
MBALIMBALI ZA KAMATI YA PAC YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU SHIRIKA LA UMEME LA
ZANZIBAR (ZECO).
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba katika Mkutano wa Saba wa
Baraza la Nane la Wawakilishi, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa kuchaguliwa
na wananchi wa Jimbo la Kiwani, Mheshimiwa Hija Hassan Hija kwa kutumia haki
yake chini ya Kanuni za Baraza ya 27 (1) (m), 27 (3), 48 (1) na 49 (1) Toleo la
2011 aliwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 117 ya Kanuni za Baraza
na kulitaka Baraza liridhie kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kulichunguza
Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Mheshimiwa Spika, Vilevile
itakumbukwa kwamba Baraza lako Tukufu lilikubaliana kwamba hoja hiyo ya
Mheshimiwa Hija Hassan Hija ifanyiwe kazi kupitia Kamati ya Kudumu ya Baraza ya
Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) na
Mheshimiwa Hija mwenyewe kuingizwa katika kamati hiyo ili kusaidia katika
uchunguzi huo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi huo wa Baraza, Kamati ya PAC
ikimjumuisha Mheshimiwa Hija ilianza kufanya kazi hiyo rasmi tarehe 30 Aprili,
2012 na kuwasilisha ripoti yake Barazani katika Kikao cha Baraza kilichofanyika
Mwezi wa Machi, 2013. Baada ya kuwasilishwa, Serikali iliahidi kuifanyia kazi
ipasavyo Ripoti hiyo ya PAC na baadae kuwasilisha taarifa rasmi katika Baraza
lako hili.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea
Ripoti ya Kamati ya PAC ya Baraza lako kuhusu Shirika la Umeme la Zanzibar
(ZECO) kwa moyo mkunjufu na kuifanyia kazi kwa umakini mkubwa na uadilifu
wa hali ya juu ili kuona mapungufu yaliyoonyeshwa katika Ripoti hiyo
yanafanyiwa kazi kwa maslahi ya nchi yetu na vile vile wale walioguswa
wanafanyiwa haki na uadilifu kufuatana na matakwa ya Sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukushukuru kwa dhati wewe mwenyewe binafsi
kwa kukubali hoja ya Mheshimiwa Hija Hassan Hija kufanyiwa kazi na PAC. Aidha,
nawapongeza kwa dhati Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya PAC kwa kazi
kubwa na nzuri walioifanya katika kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme la
Zanzibar na kuwasilisha vyema kwa Baraza taarifa yao. Aidha, niwashukuru
Wajumbe wote kwa michango yao na kufikia mapendkezo yenye ufanisi. Kwa kweli
taarifa hii imetuonesha mambo mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Serikali
ili kuimarisha utendaji wa Shirika kwa maslahi ya Taifa letu. Muelekeo huu wa mashirikiano
miongoni mwa mihimili mikuu ya Serikali ndio hasa utakao tusaidia katika
kujenga mustakbali mwema wa nchi yetu na kuimarisha dhana ya utawala bora na
kupambana na vitendo vyote viovu ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Baraza lako Tukufu kwamba
Serikali tayari imeshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Baraza
la Wawakilishi na kuchukua hatua stahiki katika baadhi ya maeneo
yaliyopendekezwa na Wajumbe.
2.0 MAELEZO KUHUSU HOJA MBALIMBALI
ZILIZOTOLEWA KATIKA RIPOTI YA KAMATI YA PAC
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo ya utangulizi sasa
naomba uniruhusu kutoa ufafanuzi wa Serikali juu ya hoja mbali mbali
zilizojitokeza katika Ripoti ya Kamati ya PAC kama ifuatavyo:
Hoja Nambari 1: Wateja kupewa risiti zenye
kiwango kidogo kuliko malipo halisi waliyolipa.
Mheshimiwa Spika, katika Ripoti ya Kamati ilionyeshwa kasoro ya
baadhi ya wateja wa Shirika kupewa risiti zenye kiwango kidogo kuliko malipo
halisi waliyolipa wateja hao na hivyo Kamati kupendekeza kuwa watendaji wote
waliohusika wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya Serikali kuhusu hoja hii ni kwamba
Serikali inakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Baraza lako Tukufu na tayari
hatua imeshachukuliwa na Shirika la Umeme kwa kuliarifu Jeshi la Polisi
kuanza kuchukua hatua za kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wateja
waliolalamikia kulipa fedha nyingi lakini risiti walizopewa zimeandikiwa fedha
kidogo. Aidha, Serikali imelitaka Jeshi la Polisi liwatake wateja hao
kuwabainisha watendaji waliohusika na suala hili ili liwachunguze na iwapo
watabainika kuwa wamekiuka sheria na taratibu wachukuliwe hatua za
kisheria.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu Nam. 44 cha Sheria ya
Shirika la Umeme Nam. 3 ya mwaka 2006, Serikali imemuagiza Waziri anaehusika na
Sekta ya Nishati kuunda Kamati ya Rufaa za Wateja ili kushughulikia malalamiko
ya wateja. Napenda kuwaarifu kwamba, hatua za kuunda Kamati ya Rufaa za wateja
zinakaribia kukamilika. Mambo ya msingi yanayozingatiwa katika uundaji wa
Kamati hii ni namna itakavyotekeleza majukumu yake. Hivi sasa Shirika la Umeme
limo katika jitihada kubwa ya kushughulikia manung’uniko ya wateja na kutoa
huduma zake bila upendeleo na kuepusha kuwepo hisia za mianya ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Fundi Salum Saad Khamis,
naomba kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba mfanyakazi huyo tayari amesimamishwa
kazi ili kuruhusu hatua za uchunguzi ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Spika, Vilevile napenda kuliarifu Baraza lako
Tukufu kwamba Shirika la Umeme tayari limeshaliandikia Jeshi la Polisi
kukumbushia kuhusu kesi yenye Nambari RB1250/2012 iliyopo Kituo cha Polisi
Chake Chake na RB302/2013 ya Kituo cha Polisi Konde zinazomuhusu Ndugu
Abeid Mohammed Abeid ili Jeshi hilo liharakishe uchunguzi haraka iwezekanavyo
na upelelezi utakapokamilika na kukidhi vigezo vya kisheria hatua za kisheria
zichukue mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa huyo. Aidha, Kamishna wa Polisi
Zanzibar ametakiwa kusimamia kwa karibu ili utekelezaji wa suala hili uende
haraka.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwajulisha Waheshimiwa Wajumbe wa
Baraza lako Tukufu kwamba tayari barua za onyo zimetolewa kwa Meneja Mkuu na
Meneja wa Tawi la Pemba kwa kutokuwa makini katika kusimamia majukumu yao na
kushindwa kuwasimamia vyema watendaji walio chini yao. Barua hizo za onyo
zimetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya 2011. Na bado
Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya watendaji hao ili kuona wanatekeleza
majukumu yao kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma.
Iwapo wakibainika kwenda kinyume, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa onyo la mwisho la
maandishi kwa Ndugu Ahmed S. Yussuf kwa kitendo chake cha kujifanya wakala wa
wateja wanaotaka kuungiwa umeme wakati yeye ni mfanyakazi wa Shirika.
Aidha, Serikali haitomvumilia mtendaji yeyote wa Shirika atakaekwenda kinyume
na maadili ya kazi yaliyowekwa.
Hoja Nambari 2: Fedha za Malipo ya kuungiwa umeme
kuingizwa katika Akaunti ya Mtendaji wa Shirika, Ndugu Zakia Juma Azan.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Kamati ya PAC ilipendekeza
kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya mhusika Ndugu Zakia Juma
Azan kwa kutokuwa muadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake. Ndugu Zakia
alijihusisha na uwakala wa mteja wa kuungiwa umeme wakati huo huo akiwa ni
mfanyakazi wa Shirika la Umeme. Hatua hiyo inapelekea kuwa na mgongano wa
kimaslahi baina ya Ndugu Zakia na Shirika la Umeme. Kutokana na hali hiyo,
Serikali inakubaliana na pendekezo hilo la Kamati na tayari hatua ya kumhamisha
Ndugu Zakia kutoka Shirika la Umeme imechukuliwa. Hatua hizo za kinidhamu zimechukuliwa
kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011. Mfanyakazi
huyo amehamishwa kutoka Shirika la Umeme kwenda Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji
na Nishati na huku akiangaliwa utendaji wake.
Hoja Nambari 3 na 6: Kuwepo kwa makisio ya aina mbili kwa mteja
mmoja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inaishukuru Kamati
kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kugundua mapungufu haya ambayo yalichangia
kulikosesha Shirika la Umeme mapato kutokana na udanganyifu wa baadhi ya
watendaji wa Shirika kutoa makisio ya aina mbili kwa mteja mmoja. Serikali
imelitaka Shirika la Umeme kuwa makini katika utendaji wake na kuzingatia
sheria na taratibu za kazi na Wizara husika imetakiwa kuwa karibu zaidi
kulisimamia Shirika ili mapungufu kama haya yasitokee tena. Aidha, Shirika
limetakiwa kuanzia sasa kuwa wazi kwa kuweka bayana vigezo na viwango bila ya
kuwepo mwanya wa ubabaishaji ili kila mteja anaetaka kuunga umeme aweze kujua
gharama zake. Vile vile, Shirika limetakiwa kuwa makini katika kufanya tathmini
ya gharama za wateja wakati wa kuwaungia umeme na kutoa makisio na maelezo
sahihi ya aina na sifa za vifaa vinavyotakiwa (Specifications) kwa mteja ili
kuepuka wateja kununua vifaa visivyokuwa na viwango vinavyotakiwa au
visivyohitajika.
Hoja Nambari 4, 17 na 18: Ushiriki
wa Mohammed & Bashir kwa niaba ya Sana Express katika zoezi zima la
uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya Kamati juu ya ushiriki wa Duka
la Mohammed & Bashir ambalo halimo katika orodha ya maduka/makampuni
yaliyopewa kibali na Shirika cha kuuza na kusambaza vifaa vya umeme. Shirika
tayari limeiandikia rasmi Kampuni ya Mohammed & Bashir kusitisha mara moja
biashara ya uuzaji wa vifaa vya umeme na kwamba Shirika halitosita kuchukua
hatua za kisheria dhidi ya Kampuni yoyote itakayoendesha biashara inayohusu
masuala ya umeme bila ya kibali cha Shirika. Aidha, Serikali imeliagiza Jeshi
la Polisi na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya uchunguzi wa kina kwa
Kampuni hiyo ya Mohammed & Bashir kuhusu tuhuma za kutumia risiti za
Kampuni ya Sana na kwa kufanya hivyo kuna uwezekano wa mhusika kukwepa kulipa
kodi. Vile vile, Serikali imelitaka Shirika kuanzia sasa kuhakikisha
linajiandaa kuwa na vifaa vya kutosha vinavyokidhi mahitaji ya wateja wanaotaka
kuungiwa umeme sambamba na kuhakikisha kuwa vifaa vya umeme vinavyotoka nje ya
nchi vinakuwa na viwango bora kwa kuvifanyia ukaguzi unaostahiki kabla
havijaanza kutumika kwa kushirikiana na taasisi inayohusika na ubora wa viwango
(Zanzibar Bureau of Standards-ZBS)
Hoja Nambari 5: Namna ya
upatikanaji wa vifaa vya uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii ya vifaa vilivyotumika
kuunga umeme kwenye Hoteli ya Misali vilivyochukuliwa kutoka katika ghala la
Shirika, kumejitokeza mgongano wa maelezo yaliyotolewa. Hivyo, Serikali
imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi zaidi wa
suala hilo. Baada ya uchunguzi huo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Serikali
itachukua hatua muafaka kwa kuzingatia ushahidi utaopatikana.
Hoja nambari 7: Fundi Abeid
Mohammed Abeid si Mfanyakazi wa Shirika lakini anafanya kazi za Shirika kinyume
na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana na hoja ya Baraza lako Tukufu
kuwa fundi Abeid Mohammed Abeid si mfanyakazi wa Shirika la Umeme na kwa
kutambua hilo, Serikali imelitaka Shirika kuwa makini na watu kama hao ambao
wanafanya kazi za Shirika lakini si waajiriwa wa Shirika hilo na kupelekea
kulihujumu Shirika. Shirika tayari limeliandikia Jeshi la Polisi na
kulitaka kufanya upelelezi wa kina kwa suala hili na kwa wahusika wote na
kuchukua hatua muafaka za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kuhusika
na makosa hayo.
Hoja Nambari 8: Kukiukwa agizo la
Bodi ya Wakurugenzi kuhusu mgongano wa maslahi katika ushiriki wa Ndugu Hamidu
Saidani Ali na Ndugu Ali Abeid Haji katika ZECO na GECCO.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuwepo kwa mgongano wa maslahi
(conflict of interests) kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa ZECO pia kuwa ni
wafanyakazi wa Kampuni binafsi ya GECCO ni jambo ambalo halikubaliki hata
kidogo. Ili kuondoa mgongano wa maslahi, Serikali imechukua hatua ya
kuwahamisha wafanyakazi hao na kuwapeleka sehemu nyengine.
Hoja Nambari 9: Watu walioungiwa
umeme kinyume na utaratibu, na baadhi ya Wateja kutumia huduma hii bila ya
kusajiliwa na hivyo kutumia umeme bure. (Hawamo katika orodha ya Wateja wa
Shirika).
Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kwamba lipo tatizo la
baadhi ya watendaji wa Shirika ambao si waadilifu huwaungia umeme wateja
kinyume na utaratibu uliowekwa na Shirika kwa maslahi yao binafsi. Hivyo,
Shirika tayari limeshaliandikia Jeshi la Polisi kuanza uchunguzi wa kina kwa
wale wote waliotajwa katika Ripoti ya PAC kuwa wameungiwa umeme kinyume na
utaratibu na kuwataka watu hao kuwataja watu waliowaungia umeme huo. Baada ya
uchunguzi hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika wana makosa.
Hoja Nambari 10: Mkurugenzi Mkuu
wa ZBC aliruhusu Kampuni Binafsi ya Zanzibar Data Com kutumia umeme kutoka
katika mnara wa ZBC kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inaendelea kulifuatilia
suala hili kutokana na kukosekana kwa taarifa zitakazowezesha kutoa maelezo
sahihi.
Hoja nambari 11 na 25: Ndugu
Mohamed Hashim Ismail aliagiza kurudishwa umeme kwenye mnara wa Kampuni ya
Zanzibar Data Com. kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya PAC ilimuona aliyekuwa Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Ndugu Mohammed Hashim Ismail kuwa
ameliingiza Shirika katika hasara kwa kuagiza kurudishwa umeme katika mnara
unaotumiwa na Kampuni ya Zanzibar Data Com kinyume na utaratibu. Serikali
imefuatilia hoja hii na kuona kwamba hakuna hasara iliyopatikana kutokana na
amri ya Mwenyekiti wa Bodi, kwa sababu wakati wa kurudishwa umeme huo Shirika
liliiwekea Kampuni hiyo mita ya TUKUZA na deni lake lote la nyuma liliingizwa
katika mita hiyo. Kwa sababu hiyo Serikali imeona hakuna sababu za kumchukulia
hatua za kisheria Mwenyekiti huyo wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika
la Umeme.
Hoja Nambari 12: Bodi ya
Wakurugenzi ya ZECO ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu Mohamed Hashim Ismaili
iliichagua Kampuni ya CRJE badala ya Salcon iliyoshinda zabuni katika ujenzi wa
misingi ya majenereta 32 na baadae kuvunja mkataba na CRJE uliopelekea Shirika
kulipa fidia ya Dola za Kimarekani 20,786.00 na kulitia hasara Shirika.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Bodi ya ZECO iliichagua Kampuni
ya CRJE badala ya Kampuni ya Salcon iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa misingi ya
majenereta 32 na baadae kulazimika kuvunja mkataba na Kampuni hiyo ya CRJE.
Hata hivyo fedha zilizolipwa hazikuwa za fidia ila ni malipo ya kazi iliyowahi
kufanywa na CRJE. Aidha, Serikali baada ya kulichunguza suala hili pia
iligundua kwamba Kampuni ya MANTRAC walilipwa fedha zao za ujenzi kama
kwamba Kampuni ya CRJE haikulipwa kabisa. Hivyo, Serikali imeliagiza Shirika la
ZECO liliandikie MANTRAC kulipa fedha za CRJE.
Hoja Nambari 13: Tofauti ya malipo
kwa kazi inayofanana, au wakati mwengine kazi kubwa kuwa na malipo madogo
katika uungaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Shirika kutoza malipo tofauti kwa kazi
zinazofanana Serikali imelitaka Shirika liwe makini katika kufanya tathmini za
gharama za wateja wakati wa kuwaungia umeme. Vile vile Shirika limeagizwa
kuweka viwango vya bei vinavyoeleweka kwa ajili ya uungaji wa umeme ili kila
anaehitaji huduma aweze kujua gharama halisi.
Hoja Nambari 14: Upendeleo katika
uungwaji wa umeme ambapo baadhi ya wateja walioomba mwisho wanapewa kipao mbele
kuliko wale walioomba mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dhamira ya Shirika si kufanya kazi
kwa upendeleo, hivyo Shirika litajtahidi kuepuka manung’uniko na litoe huduma
bila ya upendeleo na liepushe hisia za kuwepo mianya ya rushwa.
Hoja Nambari 15: Malipo
yanayolipwa na baadhi ya Wateja bila ya kupewa risiti kabisa. Baadhi ya wateja
kuuziwa vifaa vya Shirika lakini hakuna risiti za mauzo hayo Mfano: Atlas
Hoteli.
Mheshimiwa Spika, Serikali imelitaka Shirika la Umeme litoe
elimu kwa wananchi kwamba kamwe wasikubali kulipa pesa mikononi kwa mtu yoyote
kwa ajili ya kupata huduma za umeme, malipo yote yalipwe katika Shirika na
walipaji wapewe risiti zinazolingana na kiasi cha fedha walizotoa. Shirika liwe
makini kuhakikisha kwamba watu wote wasiowaaminifu na wasiokuwa watendaji
hawatumii jina la Shirika kujinuafaisha binafsi. Programu ya kutoa elimu kwa
wananchi tayari imeanza na itaendelea kwa kutumia njia ya redio, televisheni na
kwa maofisa wa Shirika kutembelea maeneo mbalimbali ya wateja. Aidha, Serikali
imeona hakuna haja ya kuchukuliwa hatua yoyote kwa Hoteli ya Atlas kwa vile upo
ushahidi wa risiti wa kwamba hoteli hiyo imelipa gharama za vifaa vilivyotumika
kwa kuungiwa umeme.
Hoja Nambari 16: Kazi kubwa ya
kuunga umeme kwenye minara ya simu za mkononi kupewa Kampuni binafsi badala
Shirika kuifanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii ya kazi kubwa kupewa Kampuni
binafsi badala ya kufanywa na Shirika lenyewe, Serikali tayari imeliagiza
Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba kazi ya kuunga umeme katika maeneo yote
inafanywa na Shirika lenyewe isipokuwa pale inaposhindikana ndio Shirika
liidhinishe Kampuni binafsi kufanya kazi hizo. Aidha, Shirika lihakikishe kuwa
sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu katika kuteua Kampuni binafsi na
kwamba hakutakuwa na mgongano wa kimaslahi baina ya ZECO na Kampuni hizo,
viongozi au kwa watumishi.
Hoja Nambari 19: Shirika kuendelea
kuiruhusu GECCO kufanya Biashara ya Transforma wakati kuna agizo la Bodi ya
Wakurugenzi ya Shirika kufuta kibali cha biashara hiyo kwa Kampuni ya GECCO.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshangazwa sana na kitendo cha
ZECO kuwakataza GECCO kuuza transfoma huku Shirika hilo likiendelea kuzikubali
transfoma za GECCO zinazoletwa na wateja na pia kutoheshimu maamuzi ya Bodi
iliyolikataza Shirika hilo kupokea transfoma kutoka Kampuni ya GECCO. Kutokana
na hali hiyo, Serikali imelitaka Shirika la Umeme Zanzibar kuheshimu maamuzi ya
Bodi ya Wakurugenzi yanayotolewa kwa Shirika hilo. Serikali tayari imeshamuonya
Meneja Mkuu wa ZECO kuhusiana na suala hili na kuliagiza Shirika kuchukua hatua
za kinidhamu kwa wengine wote waliohusika na suala hili.
Hoja Nambari 20: Upotevu wa
kumbukumbu za Mteja Ras Kichanga.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kufanya
uhakiki kwa wateja wake wote wakubwa na wadogo ili kujua idadi halisi ya wateja
na kuweka kumbukumbu zao. Aidha, Serikali imeliagiza Shirika la
Umeme kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi waliohusika na kitendo
cha kuyaacha majalada ya wateja wa Shirika hilo kuroa. Pia agizo limetolewa kwa
Shirika hilo kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wote waliohusika na
upotevu wa majalada ya wateja wakubwa wa Shirika pamoja na wateja wa vituo vya
minara ya simu. Shirika tayari limeanza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya
wahusika wote kwa kuwataka kutoa maelezo kwa nini Shirika lisiwachukulie hatua
kwa makosa waliyoyafanya.
Hoja Nambari 21: Kutochukuliwa
hatua za kisheria dhidi ya Residence
Hotel ambayo ilivuta umeme kwa kutumia Kampuni ya CRJE badala ya ZECO.
Na kuiruhusu Kampuni ya GECCO kufanyakazi ya uungaji wa umeme huku
ikieleweka wazi kuwa sheria inakataza suala hilo.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu hoja hii, Serikali imebaini kuwa
kazi ya uungaji wa umeme katika Hoteli ya Residence imefanywa na ZECO na
Kampuni ya CRJE imeilipa ZECO gharama za kazi ya uungaji (labour charge).
Kampuni ya GECCO imeiuzia kampuni ya CRJE vifaa vya umeme vilivyotumika katika
kazi hiyo.
Hoja Nambari 22: Kuruhusu uungwaji
wa Umeme kwa Kendwa Beach Resort,
Docrim Hotel na The Leisure
Hotel bila ya kufuatwa taratibu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba masuala kama haya
hayajirudii, Serikali imelitaka Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba
linawahakiki wateja wote wakubwa na wadogo ili kujua idadi halisi ya wateja na
kumbukumbu zao, kazi ambayo tayari Shirika limeanza kutekeleza kwa kuandaa
mfumo wa kumbukumbu za wateja “Data
Base” ambao utakuwa unafanyiwa mapitio mara kwa mara. Aidha, Serikali
imelitaka Shirika kuhakikisha kwamba kila mteja anaetaka kuungiwa umeme anajaza
fomu ya maombi ya kuungiwa umeme na taarifa zake zinahifadhiwa vizuri ili
ziweze kupatikana wakati zitakapohitajika.
Hoja Nambari 23: Kushindwa
kuthibitisha wapi zimenunuliwa nguzo na transforma zilizotumika katika nyumba
ya kupumzikia ya Ndugu Shumbana Amani Karume. Kushindwa kuthibitisha wapi
imenunuliwa Transforma ya “The Sayyida
Hotel” na wapi yamelipwa malipo ya gharama za uungwaji wa umeme wa
Hoteli hiyo na taratibu zipi zilizotumika. Aidha, kusamehewa kodi ya VAT kwa
Hoteli hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya ukaguzi wa eneo
linalohusika na hoja hii na kubaini kwamba nguzo zilizotumika katika kupeleka
umeme huo ni ishirini (20) na Shirika la Umeme ndilo lililopeleka nguzo hizo.
Aidha, Serikali ilipeleka umeme kwa kuelewa kwamba eneo hilo ni eneo la
Uwekezaji na tayari hoteli mbili (2) zimeshajengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hoja inayoihusu “The Sayyida
Hotel”, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba hoteli hiyo ililipa kodi ya
VAT kama ilivyohitajika. Aidha, hoteli hiyo haikuunga umeme kwa kutumia transfoma
yake.
Hoja Nambari 24: Upatikanaji wa
transforma ya hoteli ya Larosa Deivent na kwa nini taratibu za kawaida
hazikufuatwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia suala hili na
kubaini kwamba transfoma iliyowekwa katika Hoteli ya Larosa Deivent imenunuliwa
na mmiliki wa hoteli hiyo kutoka kampuni ya OSAJU.
Hoja
Nambari 26: Kampuni ya Zanzibar Data
Com kwa mnara wa Mtoni inadaiwa kiasi gani? na italipa kwa utaratibu
gani na kwa muda gani?.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Zanzibar Data Com ilikuwa
inadaiwa jumla ya Dola za Kimarekani 9,600 na hadi kufikia mwezi wa Oktoba,
2013 Kampuni hiyo ilikuwa imekwishalipa Dola za Kimarekani 3,600 na kubakia
deni la Dola za Kimarekani 6,000. Shirika la Umeme limeingia makubaliano na
Kampuni ya Zanzibar Data Com ambapo utaratibu ni kufanya malipo kila mwezi
ambayo yanatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24 kuanzia mwezi
Machi, 2013.
Hoja Nambari 27: Suala la kuhamishwa “Internal Auditor”
kutoka Pemba na kwa nini kwa muda mrefu Akaunti za hesabu za Pemba
hazijafanyiwa ukaguzi wa ndani na wala wa nje?
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba
ni kweli Mchunguzi wa Hesabu wa Ndani (Internal Auditor) wa Shirika
la Umeme wa Pemba alipewa uhamisho. Hatua za kumhamisha mfanyakazi huyo
zilichukuliwa kutokana na kutowajibika kwake ipasavyo, kitendo ambacho
kilipelekea kutotoa ripoti za ukaguzi hata moja kwa kipindi chote alichokuwepo
katika nafasi hiyo. Hivi sasa Shirika tayari limeshampeleka
Mchunguzi wa Hesabu wa Ndani mwengine wa kudumu huko Pemba na pia Serikali
imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kuzifanyia ukaguzi hesabu za Shirika hilo huko Pemba.
Hoja Nambari 28: Hakuna ruhusa iliyotoka kwa Bodi ya
Wakurugenzi kuhusu ajira ya wafanyakazi 16 walioajiriwa mwaka 2008.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja ya Kamati ya PAC
na kulitaka Shirika kutofautisha baina ya kuidhinishwa kwa bajeti na
kuidhinisha kwa uajiri. Hivyo, Shirika limetenda kosa la kuajiri wafanyakazi 16
mwaka 2008 bila yakupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi, na hivyo Serikali
tayari imempa onyo Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme na kumtaka awe makini zaidi
katika utekelezaji wa majukumu yake na kufuata sheria.
Hoja Nambari 29: Kasoro
zilizotajwa kuhusu uajiri kuanzia 2008 mpaka 2012.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kasoro zote zinazohusiana na masuala ya
uajiri zilizotajwa katika hoja hii, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme
kufuata kwa ukamilifu sheria na taratibu zote za uajiri kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011, ikiwemo kuzitangaza nafasi za kazi,
kuweka vigezo sahihi, kufanya usaili na kuwepo mikataba ya ajira. Aidha,
Shirika limetakiwa kuandaa mpango wake mkuu wa mafunzo utakaotekelezwa bila ya
upendeleo.
Hoja Nambari 30: Uuzwaji wa Gari
Land Rover SLS 1023 na Toyota Pick Up SLS 1045 ambazo ziliuzwa bila ya idhini
ya Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii naomba kulieleza Baraza
lako Tukufu kwamba barua iliyotoka Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya
Maendeleo kuidhinisha kuuzwa mali za Shirika la Úmeme haikuidhinisha uuzwaji wa
gari Nam. SLS 1023 Land Rover na SLS 1045 Toyota Pick Up. Gari hizo ambazo
hazikuidhinishwa aliuziwa Ndugu Shaibu Hassan Kaduara. Hivyo, Serikali imeagiza
kufanyika uchunguzi wa kina kubaini mazingira yaliyopelekea Ndugu Kaduara
kuuziwa gari hizo. Serikali tayari imemuandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kulishughulikia suala hilo. Aidha, hatua za kinidhamu na
kisheria zitachukuliwa kwa waliohusika iwapo itabainika kuwa gari hizo ziliuzwa
bila kufuatwa utaratibu.
Hoja Nambari 31: Uuzaji wa Mali za
Shirika ambazo ziliuzwa na Uongozi wa Shirika badala ya Kitengo cha Manunuzi
kama sheria inavyoelekeza (kifungu nam. 175(3) cha Kanuni za Sheria Nam. 9 ya
mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inakubaliana na
mapendekezo ya Kamati ya PAC na hivyo imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika
hilo kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kupewa onyo wote waliohusika na kuuza
mali za Shirika bila kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.
Hoja Nambari 32: Tofauti kati ya
orodha ya vitu vilivyoidhinishwa na Bodi na vitu halisi vilivyouzwa na Shirika
katika mnada wa tarehe 18/12/2011.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida, tungetarajia kuwa kwa
vile Shirika la Umeme Tawi la Pemba liliorodhesha idadi ya vitu walivyotaka
kuviuza, Afisi Kuu ya Unguja ilipaswa kuorodhesha vifaa vyote vilivyoruhusiwa
kuuzwa na vilivyokuwa havikuruhusiwa kuuzwa na mauzo yafanywe kwa mujibu wa
ruhusa hiyo. Hivyo, kwa kuwa kuna vitu vimeuzwa bila ya kufuata utaratibu,
Serikali inaendelea kufanya uchunguzi na hatua za kinidhamu na kisheria
zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika na makosa
kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi
wa Umma na Sheria ya Manunuzi.
Hoja Nambari 33: Transforma ya KVA
1500 ambayo haimo kwenye vifaa vilivyopigwa mnada iliondolewa katika eneo
iliyokuwepo na haijulikani ilikopelekwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali imeiagiza Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kulifanyia uchunguzi ili kubaini
uhalisia wa suala hili. Hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa kwa wale
watakaobainika kuhusika na upoteaji wa transfoma hiyo.
Hoja Nambari 34: Kukodi gari kwa
mtu binafsi kwa ajili ya kazi za Shirika na kutumia pesa nyingi badala ya
kununua gari yake kama hiyo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli muda wa miezi tisa (9) ni mrefu kwa
kukodi gari ya mtu binafsi kwa kufanya kazi za Shirika. Hivi sasa Shirika
la Umeme tayari limeshapata gari zake na hivyo limeachana kabisa na utaratibu
wa kukodi gari za mizigo za watu binafsi. Aidha, Shirika limetakiwa wakati wote
kuweka mawazo ya kibiashara na kuepuka kulitia hasara Shirika.
Hoja Nambari 35: Licha ya kuwepo
na mkataba baina ya Shirika na Mtu Binafsi (Mwenye gari) kwa nini alikuwa
anatiliwa mafuta kutoka katika vituo vya mafuta vya Shirika? Fedha alizokuwa
akikatwa zilikuwa zinakwenda wapi?.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuatilia hoja hii na kuona kwamba
ni kweli baadhi ya siku gari lililokodiwa lilitiwa mafuta na Shirika baada ya
kukosekana mafuta katika vituo vya mafuta. Gharama za mafuta aliyokuwa
akitiliwa zilikuwa zinakatwa katika malipo ya mwenye gari hiyo na fedha kurudi
katika Shirika kwa faida kwa vile Shirika lilikuwa linanunua mafuta hayo kwa
bei ya jumla na kumkata mwenye gari hiyo kwa bei ya reja reja. Hivyo, hakukuwa
na upotevu wa fedha za Shirika.
Hoja Nambari 36 na 37: Majenereta
32 ya Shirika la Umeme yaliyopo Mtoni yalipatikana kwa fedha za MDRI au
Mfadhili na taratibu gani zilotumika katika kuyanunua?.
Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa ufafanuzi kwamba Majenereta
haya hayakununuliwa kwa fedha za MDRI bali yalinunuliwa kwa fedha za Wahisani
na Serikali. Aidha, ununuzi huu ulifanywa kwa mashirikiano baina ya Wahisani na
Serikali chini ya Mshauri wa Mradi wa Umeme Vijijini aliyekubalika na Wahisani
hao. Ununuzi huo ulifanyika chini ya utaratibu wa manunuzi katika hali ya
dharura ambao ulikubalika na pande zote mbili.
Hoja Nambari 38: Mpango wa Shirika
la Umeme Zanzibar wa kuyatumia majenereta 32 ya dharura kwa ufanisi na kwa
kutumia gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kutakiwa Shirika kuwa na
Mpango wa matumizi wa majenereta 32 ya dharura, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji
na Nishati tayari imeandaa mapendekezo kuhusu majenereta hayo ya dharura na
Serikali itajadili mapendekkezo hayo na itatoa maelekezo kwa Wizara husika hivi
karibuni.
3.0
MTAZAMO WA SERIKALI KUHUSU RIPOTI YA KAMATI YA PAC.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ufafanuzi juu ya hoja
mbalimbali zilizotolewa katika Ripoti ya Kamati ya PAC yapo mambo ambayo
Serikali imeona ni vyema kutoa mtazamo wake ili kuwa na uchambuzi unaostahiki
(balanced scrutiny) na kuweka mwelekeo mwema wa baadae.
Aidha, mtazamo huo wa
Serikali una nia ya kutoa ushauri juu ya masuala yaliyojitokeza
kwa Kamati wakati ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Hatua hii
itatusaidia pale itakapotokea haja ya kuwa na Kamati Maalum au Kamati Teule
inayoundwa kuchunguza jambo ili kamati hiyo iweze kufanya kazi zake kwa
uadilifu na bila ya kuonekana kuwa na upendeleo (bias).
Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri katika kazi zijazo za
Kamati ni vyema ripoti zikaonesha kwa uwazi maelezo kamili yanayotolewa na
watendaji. Aidha, Serikali inashauri kwamba Baraza liangalie Kanuni ya 120 na
kuona uwezekano wa kuifanyia marekebisho ili mjumbe anaetoa hoja asiwe mjumbe
wa Kamati itakayoundwa kuchunguza hoja hiyo.
4.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
naomba kwa mara nyingine tena kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa
jinsi unavyosimamia kazi za Baraza kwa umakini na umahiri mkubwa na kuniwezesha
kuwasilisha taarifa hii ya Serikali kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako.
Vile vile naomba nichukue fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru sana
Mheshimiwa Hija Hassan Hija, Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Kiwani kwa
ujasiri wake na uzalendo wake wa kuibua hoja ambayo kwa kweli imetuonesha
mapungufu tuliyokuwa nayo katika Shirika, mapungufu ambayo Serikali
imeweka nia ya dhati ya kupambana nayo si kwa Shirika la Umeme tu bali kwa
taasisi zote za Umma.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru na kutoa
pongezi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mheshimiwa Omar Ali Shehe na Wajumbe
wote wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa na nzuri iliyoibua mambo mengi muhimu yenye
mustakbali mwema katika kulijenga Shirika letu na kuimarisha uchumi wa Taifa
letu.
Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa
kuridhia kamati ya PAC kufanya kazi hii ambayo sote faida yake tumeiona na kwa
kufuatilia kwa utulivu na umakini mkubwa maelezo ya Serikali niliyoyatoa.
Pia nawashukuru
wale wote waliyosaidia Kamati ya PAC kufanya kazi zake kwa kuwapatia taarifa
walizozihitaji. Ni imani yangu kuwa viongozi na watendaji serikalini pamoja na
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi sote kwa pamoja tutaitumia fursa hii ya
kuibuka kwa hoja hizi kujifunza na kubadilika kwa dhati na kuachana na tabia ya
kufanyakazi kwa mazoea ili kuzidi kuijengea heshima nchi yetu, kuendelea
kujenga imani kwa wananchi wetu na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi
katika nchi yetu. Haya yote yanawezekana, sote tushirikiane na tutimize wajibu
wetu.
0 comments:
Post a Comment