WAZIRI wa
Ujenzi, Dk John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa Serikali ambao
wanadaiwa mikopo ya nyumba kulipa madeni yao mara moja na kuonya kwamba ikiwa
watashindwa kulipa, watanyang’anywa nyumba
hizo na watakopeshwa watu wengine.
Dk Magufuli
ameibuka na hoja hiyo mpya, zikiwa ni siku chache tangu alipopigwa ‘stop’ na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutekeleza sheria ya kuondoa msamaha wa asilimia
tano kwa mizigo inayozidi kwenye malori, hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa
baina ya Serikali na wasafirishaji wa mizigo nchini.
Akizungumza wakati
wa kuweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za watumishi wa Serikali
eneo la Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema watumishi 2500
hawajalipa mikopo ya nyumba walizonunua.
Dk Magufuli alionya
kuwa atafuatilia suala hilo na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara moja,
huku akimwomba Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kumuunga mkono kwenye
jambo hilo, ambalo ni utekelezaji wa sheria za nchi.
“Naomba ifahamike
kwamba tunapojenga nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma tunataka
kuboresha makazi yao. Pia fedha tunazokusanya zinasaidia kujenga nyumba zaidi,”
alisema Dk Magufuli. Hata hivyo alisema hadi sasa watumishi wa Serikali 4,900
ambao walikopa nyumba hizo tayari wamelipa madeni.
“Mimi nafanya kazi
kwa kufuata sheria na kila mtumishi wa Serikali anafahamu jambo hilo, hivyo
watu ambao wanajua tunawadai wakae kwa tahadhari, kwani ndani ya mwezi mmoja
kama hawatalipa tutawachukulia hatua bila kupuuzia,” alionya Magufuli.
Hii siyo mara ya
kwanza kwa Dk Magufuli kutangaza kunyang’anya nyumba hizo, kwani alifanya hivyo
mwishoni mwa Machi mwaka jana pale alipouagiza uongozi wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba hizo kulipa madeni
yao.
Dk Magufuli
aliwataka TBA kutoa ilani ya maandishi inayowataka wahusika walipe fedha hizo
ndani ya wiki moja vinginevyo wangenyang’anywa kwa maelezo kwamba
wanachelewesha malengo ya TBA kujenga nyumba zaidi.
Hata hivyo, hakuna
taarifa zozote zilizowahi kutolewa kuhusu kutekelezwa kwa amri hiyo iliyotolewa
zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Jana, Makamu wa
Rais, Dk Bilal alimuunga mkono Magufuli akisema: “Naunga mkono tamko la Waziri
wa Ujenzi kwamba ni lazima watumishi wa Serikali ambao wanakopeshwa nyumba
walipe haraka ili fedha hizo zisaidie kujenga nyumba nyingine.”
Dk Bilal alikuwa
mgeni rasmi katika shughuli ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851,
kwenye eneo la Bunju ‘B’ Kinondoni, Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA,
Elius Mwakalinga, alisema ujenzi huo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya
kwanza iligharimu Sh2 bilioni na awamu ya pili Sh1 bilioni.
“Nyumba 851 zinazojengwa
Bunju B ni sehemu ya ujenzi wa nyumba 4,400 katika Mkoa wa Dar es Salaam na
nyumba 10,000 kwa nchi nzima,” alisema Mwakalinga.
Hafla hiyo
ilisimama takriban kwa dakika 10 wakati Dk Bilal akitaka kuhutubia baada ya
jenereta kushindwa kufanya kazi, hivyo kumlazimu kurudi kuketi kwenye kiti hadi
umeme uliporejea.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Jordan Rugimbana alilazimika kwenda kufuatilia suala hilo na mafundi
waliokuwapo walifanikiwa kuunganisha mashine za kipaza sauti na umeme wa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hivyo Makamu wa Rais aliendelea kuhutubia.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment