Tanzania imepitisha
Azimio linalohusu Kinga ya Jamii lenye msingi imara wa kusimamia masuala
hayo nchini na Afrika kwa ujumla ili kuwa na maendeleo halisi kwa watu wake.
Azimio hilo
limepitishwa na kusainiwa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum kwa niaba ya
Serikali jijini Arusha wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la siku tatu
kuhusu Kinga ya Jamii ambalo lilishirikisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali za
Afrika na nje ya Afrika.
Akitoa hotuba ya
kufunga kongamano hilo Waziri Saada alisema kuwa maazimio yaliyofikiwa katika
kongamano hilo yametoa mwelekeo na msingi wa kuimarisha kinga ya jamii kwa
wananchi.
“Nafurahi kusema
kongamano hili limekuwa hatua muhimu katika kutekeleza masuala ya kinga ya
jamii kwa nchi zote washiriki wa kongamano hili na Afrika kwa ujumla” alisema
Waziri Saada.
Waziri Saada alisema
kuwa maazimio yaliyofikiwa wakati wa kongamano hilo jijini Arusha yanalenga
kutumia mbinu mablimbali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuboresha huduma
za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu bora, afya, upatikanaji wa maji safi na
salama.
Kutokana na malengo
hayo, Serikali ya Tanzania iko mstari wa mbele katika kuwekeza na kusimamia
masuala ya kinga ya jamii kwa kuwa na bajeti endelevu ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wanchi wake.
Akisoma Azimio hilo
la Kinga ya Jamii, Katibu Mkuu Wazara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile alisema
kuwa historia imejirudia ambapo yapata miaka 47 (1967-2014) iliyopita Tanzania
ilipitisha Azimio la Arusha lililolenga kupambana na maadui watatu ambao ni
ujinga, maradhi na umaskini ambao Baba wa Taifa Mwl. Julius Kmbarage Nyerere
aliwaita ni maadui wa taifa.
Maazimio mengine
yaliyofikiwa katika kongamano hilo ni kupunguza umaskini na kukuza mitaji ya
rasilimali watu ambapo Tanzania Bara inalenga ifikapo mwaka 2025 iweimepunguza
tatizo la umaskini kwa watu wake wakati Tanzania na kwa upande wa Zanzibar
inalenga kufikia hatua hiyo mwaka 2020.
Maazimio mengine ni
kuwa utawala bora ambapo Tanzania imesisitiza kuendelea kuimarisha nguvu na
sauti ya wananchi katika masuala ya kidemokrasia nchini na kutoa na kusimamia
haki za watoto, wanawake na wanaume kwa kupinga ukatili wa kijinsia, ndoa za
utotoni, mimba za utotoni pamoja na uvamizi na mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi na mauaji ya wazee.
Kwa upande wake
Muwakilishi wa UNICEF nchini Dkt. Jama Gulaid akitoa neno la shukrani aliisifu
Tanzania kwa kuanza mapema kusimamia masuala ya kinga ya jamii ikiwemo mifuko
ya hifadhi ya jamii na misaada inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) kupitia mpango wake wa kunusuru kaya maskini zilizo katika mazingira
hatarishi.
Aidha, Dkt.
Gulaid aliipongeza Tanzania kwa kuwa na wimbo wa taifa unaozungumzia watu
akiwataja kuwa ni wanawake, wanaume na watoto pamoja na bara la Afrika na watu
wake licha ya kuwa na vivutio vizuri vya mlima Kilimanjaro, hifadhi ya
Serengeti na visiwa vya karafuu.
“Wimbo huu wa
Tanzania tofauti na nyimbo za nchi nyingine ambazo wao wanazungumzia askari,
watumwa, watawala wakiwemo Malkia na Wafalme”alisema Dkt. Gulaid.
Dkt. Gulaid
aliwahakikishia wajumbe wa kongamano hilo kuwa wote wapo salama na wapo kwenye
mpango wa kinga ya jamii kwa kuwa wametambuliwa na kubarikiwa na wimbo wa taifa
wa Tanzania ambapo wajumbe waliimba wimbo huo na kuhitimisha kongamano hilo.
Kongamano hilo
liliandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondo
Umaskini kwa kushirikiana na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa
konngamano hilo wanatoka katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh, Afghanistan,
Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Zimbabwe na
mwenyeji Tanzania.
0 comments:
Post a Comment