Mama Salma kikwete
Watanzania
wengi hawana uelewa wa tatizo la usonji (Autism) kwa
watoto hivyo basi uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii unahitajika ili
watu watambue tatizo hilo na kuweza kuwasaidia watoto hao.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma kikwete wakati akiongea na Prof. Andy
Shih ambaye ni Makamu wa Rais Mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi
ya Kimataifa ya Autism Speaks katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema jamii ikiwa
na uelewa kuhusu watoto hao kutakuwa na mabadiliko kwa wazazi na walezi hivyo
basi ni jukumu la jamii nzima kuungana na kuweza kuwasaidia watoto hao ili
waweze kupata elimu na mafunzo maalum.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alimpongeza Prof. Shih kwa kazi anayoifanya ya kuwasaidia watoto
wenye usonji Duniani na kwa kitendo chake cha kuamua kuwasaidia watoto wa
Tanzania.
Kwa upande
wake Prof. Shih alisema tatizo la usonji linatibika kama watoto watapewa
mafunzo mapema na jamii ikipata elimu na kulifahamu tatizo hilo
itaweza kuwasaidia watu wenye matatizo hayo kupata huduma.
Alisema
alitembelea shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa
huduma ya watoto wenye usonji na kujionea hali halisi na kuahidi kushirikiana
na wadau wengine ili waweze kutatua changamoto zilizopo.
Taasisi ya
WAMA kwa kushirikiana na wadau wa Afya nchini na Taasisi ya kimataifa ya Autism
Speaks yenye makao yake mjini New York Marekani watafanya kazi kwa
pamoja ili kutumia vitendea kazi na utaalam wao ambao wameukusanya kwa
miaka mingi kuwasaidia watoto wenye matatizo ya usonji nchini.
Kazi
watakazozifanya ni pamoja na kuunda timu ndogo ya wataalam wa
mitaala na mafunzo ambao watapitisha miongozo na mitaala iliyopo pamoja na ile
ya Autism Speaks na kupendekeza utaratibu wa mafunzo ya makundi mbalimbali
wakiwemo watoa huduma.
Timu hiyo
inaandaa utaratibu wa mafunzo ya wazazi, walezi na familia ya mtoto mwenye
matatizo ya usonji, kuandaa mwongozo unaokubalika wa kuwapima na kuwatambua
watoto wenye usonji, kuandaa mitaala na miongozo ya ufundishaji wa watoto wenye
usonji na kutumia jukwaa na program za kitaifa kuwalinda watoto.
Wakati wa
Mkutano wa 69 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika
mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu mjini NewYork Marekani Mama Kikwete
alikutana na Prof. Shih ambaye aliahidi kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia
watoto wenye tatizo la usonji ambao wataweza kupata elimu na huduma ya afya
kama watoto wengine.
0 comments:
Post a Comment