Wafanya biashara katika soko la kariakoo jijini Dar es Salaam wamegoma kufungua maduka na kufanya biashara zao kutokana na kukamatwa kwa kiongozi wao na Jeshi la Polisi,Kwa habari zaidi endelea kufuatilia taarifa zetu.
Wanunuzi
wa bidhaa mbalimbali katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam wamekutana na
adha baada ya wafanyabiashara wenye maduka sokoni hapo kufunga maduka yao kwa
madai ya kuishinikiza polisi kuwaeleza mwenyekiti wao yuko wapi baada ya
kukamatwa na polisi na baadae kuelezwa kuwa hayupo kituoni.
Katika soko la Kariakoo ambalo limezoeleka kuwa na
msongamano wa watu hali ilikuwa tofauti ambapo mitaa ilikuwa tulivu huku baadhi
ya vijana na wafanyabiashara wakiwa wamekaa kwenye makundi nje ya maduka yao
ambapo baadhi ya wanunuzi waliokutwa na Tambarare Halisi mbali na kulalamika upotevu wa nauli wameitaka
serikali kukaa pamoja na wafanyabiashara hao wakubaliane ili kuepusha migomo ya
mara kwa mara inayofanywa na wafanyabiashara hao ambayo pia inaikosesha
serikali mapato.
Kwa upande wa madereva wa magari ya mizigo ambao
wanaegesha maeneo hayo ya Kariakoo wamesema mgomo huo unawaathiri kwa kiwango
kikubwa kwani wenye magari wanahitaji hela ya siku lakini pia familia zao
zinawategemea.
Akizungumzia suala hilo katibu mkuu jumuia ya
wafanyabiashara nchini Bw Silva Kiondo amesema wao hawana mgomo isipokuwa
wamelazimika kufunga maduka yao ili wakamtafute mwenyekiti wa jumuia hiyo Bw
Minja ambaye wamedai kuwa alikamatwa na polisi na kufikishwa kituo kikuu cha
polisi lakini baadae walipokwenda kwa ajili ya kumdhamini walipewa maelezo kuwa
hayupo kapelekwa Dodoma.
Hata hivyo Tambarare Halisi ilifunga safari hadi kituo kikuu cha polisi
ili kupata ufafanuzi zaidi lakini hali iliyokuwepo kituoni hapo ilikuwa tofauti
na siku nyingine ambapo polisi walionekana kutanda eneo hilo huku wengine
wakiwa na silaha za moto na wakizuia watu kuingia katika eneo hilo na kamanda
wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova alipotafutwa kwa njia ya
simu hakujibu badala yake alituma ujumbe mfupi wa maandishi akidai kuwa yuko
Dodoma kwenye mkutano.
0 comments:
Post a Comment