Mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia anayechezea
Manchester United, Radamel Falcao juzi aliamua kuondoka uwanjani kwenda
kutazama mechi nyumbani baada ya kuwekwa benchi.
Nyota huyo aliye hapo kwa mkopo kutoka Monaco,
aliachwa katika kikosi cha wachezaji 18 kilichoiwakilisha United dhidi ya
Southampton na kuchapwa bao 1-0 nyumbani Old Trafford. Falcao anayelipwa Pauni
260,000 kwa wiki hakubaki uwanjani hapo na badala yake aliamua kuwasha gari
lake na kuondoka uwanjani akitokomea kusikojulikana.
Kutojumuishwa kikosini kwa Falcao kuliwashangaza wengi
baada ya Kocha wa Man United, Van Gaal kukiri kwamba mshambuliaji huyo hakuwa
majeruhi.
Badala yake Van Gaal aliwaweka katika benchi walinzi
watatu, Jonny Evans, Paddy McNair na Tyler Blackett huku katika safu ya
ushambuliaji akimuweka benchi kinda James Wilson.
Falcao, ambaye ameanza mechi saba tu za Man United
tangu alipojiunga kutoka Monaco, ameifungia Man United mabao mawili tu muhimu
katika mechi zake tano zilizopita. Hata hivyo, Kocha Van Gaal amefafanua kwa
nini alimuacha nje Falcao akidai kwamba zilikuwa sababu za kisoka zaidi na si
vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment