Image
Image

Watu 138 kijiji cha namba tisa wanahofiwa kuathirika na sumu baada ya bwawa la kuhifadhia sumu hiyo kupasuka.



WATU 138 wakazi wa Kijiji cha Namba Tisa, Kata ya Bulyanhulu, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wanahofiwa kuathirika na sumu aina ya Sayanadi (cyanide) inayotumika kusafisha dhahabu baada ya bwawa linalohifadhi sumu lililopo ndani ya Mgodi wa Bulyanhulu kupasuka na maji kutiririka katika makazi ya wananchi hao.
Bwawa hilo linadaiwa kupasuka wiki iliyopita na maji yake kutiririka hadi kijijini hapo ambapo wananchi waliyatumia kwa matumizi mbalimbali bila kujitambua.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Benson Mpesya ambaye amethibitisha hali hiyo, alisema bwawa hilo lilipasuka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na maji yake kutiririka hadi kijijini hapo.

"Mgodi huu kwa sasa unamilikiwa na Kampuni ya Acacia, wananchi waliyatumia maji hayo bila kujua kama yana sumu na watoto kuyachezea baada ya mvua kukatika.

"Kutokana na hali hiyo, uongozi wa kampuni hiyo ulikwenda kijijini hapo ambapo wananchi walilalamika baada ya kubaini maji waliyotumia yalichanganyika na sumu hivyo waliamua kuwachukua na kuwapeleka Hospitali ya Wilaya ili wachukuliwe vipimo vya afya zao," alisema.

Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Necta Foya alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema bwawa hilo ambalo linahifadhi sumu lilipasuka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na maji yake kutiririka katika kijiji hicho.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Deo Nyaga alisema wananchi hao wamefanyiwa uchunguzi wa awali juu ya usalama wa afya zao ambapo si rahisi kubaini mapema kama maji hayo.

"Baada ya watu hao kufikishwa hospitali, walidai kuwashwa mwilini, wengine kuumwa kichwa na walipofanyiwa vipimo, wengi walikutwa na malaria, minyoo, homa ya tumbo na shinikizo la damu...vipimo vingine vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali," alisema.

Mtendaji wa Kata ya Bulyanhulu, Ramadhan Madese, alisema kijiji hicho kina wakazi 3,364, zaidi ya kaya 700 ambapo maji ya bwawa hilo yalisambaa hasa katika mashamba ya mpunga na mazao mbalimbali ya wananchi ambao hadi sasa wanaishi kwa hofu kubwa wakihofia usalama wa afya zao.


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment