CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa tuhuma
nzito kwa Chama cha Wananchi (CUF) na kudai ushindi wao wa majimbo katika
Visiwa vya Pemba, Zanzibar, umetokana na chama hicho kuchukua mamluki kutoka
miji ya Tanga na Mombasa nchini Kenya.
Tuhuma hizo zilitolewa juzi na Katibu wa
Idara ya Itikadi na Uenezi ya Kamati Maalumu ya CCM, Zanzibar, Waride Bakari
Jabu katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Magereza, Kata ya Tomondo,
Wilaya ya Dimani, Mkoa wa Magharibi.
Jabu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu (NEC) na Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki, alisema siri ya ushindi wa CUF
katika majimbo yote 18 wanayoyashikilia na chama hicho Visiwani Pemba
imefichuka.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu Oktoba
mwaka huu, CCM imejipanga kuidhibiti CUF ili isiweze kuchukua mamluki katika
mikoa ya Tanga na Mombasa, nchini Kenya.
Alisema Katiba Inayopendekezwa imetoa
neema kwa wanawake ambao hivi sasa watapata fursa ya kushiriki katika vyombo
vya maamuzi kama ilivyo kwa wanaume.
“Wanawake tunatakiwa tuipigie kura ya
ndiyo Katiba Inayopendekezwa ambayo imejaa mambo mengi mazuri yanayowahusu wao
ikiwemo nafasi ya 50 kwa 50," alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi
na Uenezi, Bw.Nape Nnauye, alisema CUF kimefika ukingoni, hivyo wana CCM wasiwe
na mashaka juu ya ushindi wa kishindo ambao wataupata katika Uchaguzi Mkuu ujao
upande wa Zanzibar na Bara.
“Mwisho wa CUF ni 2015 na tayari
wameanza kufungasha virago kwani CCM tutapata ushindi wa kishindo,"
alisema Bw. Nnauye.
0 comments:
Post a Comment