Image
Image

CUF:Suala la kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa ni la kisheria na sivinginevyo

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema msimamo wake ni kuendelea kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kiwe kimeingia madarakani au la.
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema suala la kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni la kisheria, kutokana na kuwemo kwenye Katiba ya Zanzibar.
Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipoulizwa na mwandishi juu ya kauli iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, juzi, ikisema hakitaunda tena Serikali ya Kitaifa baada ya kumalizika uchaguzi mkuu mwaka huu.
CCM inalalamikia kile kilichoelezwa ni kutokana na baadhi ya washiriki wake, CUF, kuvuruga utaratibu na misingi ya kuanzishwa kwa serikali hiyo. “Suala la uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa liko kwenye Katiba ya Zazibar.
Hili ni suala la kisheria na liliridhiwa na asilimia 68 ya Wazanzibari. Msimamo wa CUF ni kuwa kama itaingia madarakani, itatekeleza hilo kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Mwanasheria wa CUF, Hashimu Mziray alisema sheria inataka rais atakayechaguliwa, akishaapishwa anatakiwa kuandika barua kwenda chama kilichofuatia kwa ushindi, kipendekeze jina la Makamu wa Kwanza wa Rais, na anatakiwa kufanya hivyo ndani ya siku 14.
Alisema chama kitakachoshika nafasi ya pili, endapo kitashindwa kutoa jina au kukataa kutoa jina, sheria inamtaka aliyeshinda kuunda serikali yake. Kama chama hicho kitabadilisha uamuzi wake, rais aliyeko madarakani atatengua uteuzi wa awali na kutoa nafasi hiyo kwa chama hicho.
“Rais anayeteuliwa kabla ya kuapishwa anatakiwa kuambiwa na jaji mipaka yake ya utawala kikatiba, na suala la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa limo ndani ya Katiba ya Zanzibar ambayo Rais anatakiwa kuitetea na kuilinda, sasa kama atasema hatafanya hivyo, basi hawezi kuapishwa na uchaguzi utaitishwa upya,” alisema.
Mwanasheria huyo wa CUF alisema, “Kauli hiyo ni propaganda tu, kwani sidhani kama CCM wanaweza kuchagua rais kichaa ambaye atakataa kulinda Katiba.”
Juzi, Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu Waride alifafanua kwamba CCM ambayo ni mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inatamka bayana kwamba haipo tayari kushiriki kuunda tena serikali hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment