Imeelezwa kwamba mtoto huyo alikuwa akilishwa chakula na watumishi wa hoteli hiyo, kabla ya kuchukuliwa na kukabidhiwa kwa watu hao wengine.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema mjini kwamba Polisi inasaka watu hao waliokabidhiwa huku mzazi (baba yake), Emmanuel Shilinde, watumishi na mmiliki wa hoteli hiyo (haikutajwa jina) wakiendelea kuhojiwa.
Mulongo alitoa taarifa hiyo wakati wa hafla ya kuapisha wakuu wa wilaya wateule watatu, Pili Bayo wa Wilaya ya Kwimba, Zainabu Telaki wa Sengerema na Mwajuma Nyiruka wa Wilaya ya Misungwi.
Pendo alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Desemba 27 mwaka jana nyumbani kwao katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza baada ya watu hao kumpora akiwa amelala na wazazi wake.
Baada ya kutoweka na polisi kutoa picha, kuwezesha atakayemwona, kutoa taarifa, pia ilitangaza kutoa dau la Sh milioni tatu kwa mtu atakayetoa taarifa, zitakazosaidia kupatikana kwa mtoto huyo.
Maisha hotelini Mkuu wa Mkoa alisema, “Baadaye Pendo alichukuliwa na kukabidhiwa kwa watu wengine, ambao walitoweka naye, kwa sasa serikali inawasaka watu hao waliokabidhiwa pale hotelini.”
Aliongeza, “Watu wote waliokuwa wanamhudumia Pendo, mzazi wake na mmiliki wa hoteli ile tunawashikilia ili watueleze alikopelekwa Pendo ingawa hatujui kama yuko hai au amekufa.”
Aliwataka wakazi wa mkoa na jiji la Mwanza, kutambua kuwa serikali inashughulikia suala la mauaji ya albino kwa umakini, ikiwa ni pamoja na kuchukua taarifa muhimu kwa idadi yao.
Alikiri, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yanasababishwa kwa sehemu kubwa na imani za kishirikina. Alisema baadhi ya waganga wa kienyeji wasiozingatia maadili ya kazi zao, wanahusishwa na mauaji hayo.
Alisisitiza, “Katika hili la mauaji ya albino, naomba niseme liko tatizo kubwa la imani za kishirikina ndani ya mkoa wetu, hivyo linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kuondokana na tatizo hili.”
Alitaka jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi, pia kwa umoja wao wajitazame kutokana na madai ya kwamba baadhi yao wamekuwa wakishiriki katika ushiriki wa mauaji hayo.
“Katika mazingira ya utekaji wa mtoto Pendo wilayani Kwimba, tumegundua kuwa mzazi wake alihusika kwa sehemu kubwa Pendo kutekwa, hivyo nichukue fursa hii kuwaomba jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wao watafakari suala hili kwa kina,” alisema.
Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Mwanza si dogo. “Liko tatizo la wazazi kuwakataa watoto wao pia,” alisema.
Alitaka wananchi kuwezesha Mahakama, kusikiliza haraka kesi zinazohusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi. Alisema kesi zinapopelekwa mahakamani zinahitaji ushahidi.
“Niwaombe wale wote watakaoshirikishwa katika hizi, wajitokeze mahakamani kutoa ushahidi.” Alisema jukumu la kupambana na mauaji ya albino ni la watu wote, jambo alilotaka kila mtu katika sehemu yake, kushiriki kikamilifu katika kupambana na mauaji hayo.
“Katika hili la mauaji ya albino, wadau wote, viongozi, wananchi na waandishi wa habari tuna kazi ya ziada ya kuhakikisha kuwa mauaji haya yanakomeshwa”, alisema.
Alishukuru viongozi wa dini wa mkoa wa Mwanza kwa kuandaa kongamano kubwa la amani, litakalofanyika Februari 28 mwaka huu katika viwanja vya Furahisha, kuzungumzia amani na viashiria vya mauaji ya albino.
Wapi wanaharakati? Aidha Mulongo alitaka wanaharakati wa haki za binadamu kujitokeza kwenye suala la mauaji ya albino. “Natoa rai kwa wanaharakati wa haki za binadamu, kama ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kudai haki mbalimbali, wajitokeze nao watusaidie katika hili la mauaji ya albino, maana sijazisikia sauti zao,” alisema.
TAS yalalamikia Mkemia Mkuu Akizungumza kwenye hafla hiyo ya kuapishwa kwa wakuu hao wa wilaya, Mwenyekiti wa Chama cha Albino Mkoa wa Mwanza (TAS) , Alfred Kapore alisema sampuli za viungo vya albino, ambazo zimekuwa zikipelekwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kubaini watu waliouawa, zimekuwa zikibadilishwa.
“Viungo vya watu wenye alibinism vinapopelekwa katika ofisi ya Mkemia wa Serikali, tumekuwa tukipata majibu yenye utata ambayo yamekuwa yakirudishwa tofauti,” alisema Kapore.
Aliongeza, “Mara utaambiwa nywele za albino zilizopelekwa zimegundulika sio nywele za mtu mwenye ulemavu wa ngozi na kwamba zilikuwa ni nywele za ‘midoli’ na mifupa tumekuwa tukielezwa sio ya watu wenye ulemavu wa ngozi ni ya kuku, mambo haya yamekuwa yanatuchanganya na kushindwa kumwamini Mkemia wa Serikali.”
Katibu wa TAS Mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju alisema Mwanza ni kati ya mikoa yenye kashfa kubwa kwa sasa, kutokana na watu wake kujihusisha na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alisema jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 15, wameuawa mkoani hapa pekee. Alitaka viongozi wa vyama na serikali, kushirikiana na wananchi kutafuta wauaji badala ya kubaki kulalamika kila wakati.
Tume ya Haki za Binadamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG), Anyony Nyanduga alisema wanao mpango wa kuandaa programu kuelimisha umma juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwa wao pia wana haki ya kuishi.
0 comments:
Post a Comment