Viongozi
wa vyama vinavyounda umoja huo, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, walitoa
tamko hilo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
wakielezea athari zinazoweza kutokea kutokana na Serikali ya Rais
Kikwete,kushinikiza matumizi ya BVR na kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.
Mwenyekiti
wa UKAWA, Freeman Mbowe, alisema kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya ni wazi
kwamba shinikizo la kulazimisha wananchi kuandikishwa kwa mfumo wa BVR,
linaweza kuiacha nchi kwenye machafuko.
Alisema
shinikizo hilo linatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani chama hicho,
ndicho kinanufaika na BVR; na kwamba UKAWA tayari ilishaweka msimamo wa kutoshiriki
kupiga kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.
"Ili
Rais Kikwete aiache nchi katika amani yake na kuepuka machafuko ni vyema aache
kushinikiza masuala hayo, asubiri amalize muda wake wa miaka 10 kuliko
kuendelea kushinikiza wananchi kutumia BVR huku wananchi wengine wakiwa hawana
taarifa na nini kinachoendelea kuhusiana na uandikishwaji kwa kutumia mfumo
huo," alisema Mbowe.
Alisisitiza
kwamba lazima ieleweke kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haina fedha, lakini
pia Sheria inahitaji NEC kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura angalau mara
mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu mwingine unaofuata.
"Lakini
kwa makusudi Serikali ya Rais Kikwete imevunja sheria ya kuboresha daftari
hilo," alisema na kuongeza;
"Kitendo
hiki kina malengo mabaya ya kutaka kuongeza muda wa utawala wake kwa kisingizio
kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika kwa datari hilo ambalo
halijaboreshwa," alisema Mbowe.
Naye
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema juzi uongozi wa UKAWA
ulipata taarifa kuhusiana na hali inayoendelea Makambako, mkoani Njombe ambako
uandikishaji wa majaribio unafanyika.
Alisema
katika uandikishaji huo wa majaribio mifumo ya BVR imeshindwa kufanya kazi hali
inayochangiwa kutokuwepo kwa maandalizi kwa watendaji wake.
"Kwa
mujibu wa taarifa mbalimbali kutoka kwa viongozi wetu walioko eneo la
uandikishaji wa wapigakura, mfumo huo ulifeli kabla ya kuzinduliwa rasmi juzi
na Waziri Mkuu na kupigiwa chapuo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi," alisema
Prof. Lipumba.
Alitaja
maeneo ambako mfumo huo umeonesha kufeli kuwa ni NEC kutokuwa na watumishi wa
kufanya kazi hiyo na kupuuza ushauri wa mwelekezi kutoka Marekani.
Alisema
mtaalamu huyo alishauri NEC iwe na watumishi zaidi 10,000 kwa ajili
ya kufanikisha uandikishaji huo nchi nzima,lakini haikufanyika hivyo.
Lakini
pia alisema watumishi wa NEC walioanza kufanya kazi mkoani Njombe wamepatiwa
elimu kwa muda wa siku moja tu kabla ya zoezi hilo kuanza na huku wengine
wakiwa hawajui hata kushika kamera.
Alisema
matatizo yaliyojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapigakura yanaonesha wazi
kuwa Daftari la Wapigakura halitakamilika ili litumiwe katika zoezi la kura ya
maoni.
"Ni
vyema Rais Kikwete akakubali ukweli huu. Suala la kura ya maoni liahirishwe
mpaka baada ya uchaguzi," alisema na kuongeza; " Tatizo kubwa zaidi
ni kuwa Tume kushindwa kuandikisha wapigakura wote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa
2015 kwa sababu mashine za kuandikisha wapigakura zina hitilafu."
0 comments:
Post a Comment