Mwaka mmoja tangu kuangushwa serikali ya Victor Yanukovych nchini Ukraine, habari za uingiliaji wa Marekani katika mgogoro wa nchi hiyo kwa lengo la kuvuruga amani na uthabiti zimeanza kufichuka.
Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Nikolai Azarov amefichua kuwa, mipango na mikakati ya kuiangusha serikali ya Victor Yanukovych ilipangwa kwenye ubalozi wa Marekani mjini Kiev. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Ukraine amesema Wamarekani na waitifaki wao wa Ulaya hawakuwa wakifurahishwa na siasa za rais Yanukovych na uhusiano wake wa karibu na serikali ya Russia. Upinzani wa Yanukovych kwa takwa la Wazungu na Wamarekani la kujiunga na muungano wao wa kijeshi wa NATO ni moja kati ya sababu kuu zilizopelekea kupinduliwa kwake.
Mgogoro wa Ukraine ulianza mwezi Februari mwaka uliopita ambapo maandamano makubwa yalifanyika mjini Kiev na katika miji mingine kupinga serikali ya rais wa wakati huo, Victor Yanukovych. Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Nikolai Azarov anasema waandamanaji walijitokeza kwa wingi baada ya kupewa taarifa za uongo kuhusiana na utendaji wa Yanukovych. Kilele cha maandamano hayo kilikuwa ni kuangushwa serikali ya Victor Yanukovych na baadaye kuingia madarakani serikali ya rais wa sasa, Petro Poroshenko mwenye mielekeo ya kimagharibi.
Kuondolewa madarakani Victor Yanukovych kulikuwa mwanzo wa kuharibika kabisa hali ya mambo nchini Ukraine. Russia ilimpokea rais huyo aliyepinduliwa na kumpa hifadhi na kukitaja kitendo cha kuondolewa kwake madarakani kuwa ni mapinduzi ya Wamagharibi na wala si ya wananchi wa Ukraine. Wananchi wa Ukraine katika maeneo ya mashariki mwa nchi likiwemo eneo la Crimea hawakukubaliana na mapinduzi hayo ya mjini Kiev na kwa mantiki hiyo wakaanzisha harakati ya kujitenga ambayo baadaye ilifikia kwenye kura ya maamuzi na matokeo yake ikawa asilimia kubwa wakaamua kujitenga na Ukraine na kujiunga na Russia.
Mgogoro wa Ukraine umechochewa kwa kiasi kikubwa na Marekani ambayo kwa kiwango kikubwa imeshindwa kufikia malengo yake ambayo ni kuidhoofisha serikali ya Russia. Kwa mtazamo mpana ni kwamba mgogoro huo badala ya kutimiza malengo ya Wamagharibi wakiongozwa na Marekani, umeibuka na kuwa kaa la moto kwa nchi hizo. Mpasuko mkubwa kati ya nchi za Ulaya na Marekani umejitokeza kutokana na mgogoro huo. Kwa mfano, mjumbe wa Ufaransa katika bunge la Umoja wa Ulaya, Jean-luc mélenchon, amenukuliwa akisema kuwa, hatua ya EU ya kuiwekea Russia vikwazo vya kiuchumi ilichukuliwa kwa kukurupuka na wala si halali.
Katika kile kinachoonekana wazi kuwa ni uchochezi wa Marekani kwa mgogoro wa Ukraine, Washington imeahidi kutuma misaada ya silaha kwa serikali ya Kiev ili iweze kupambana na wapiganaji wanaotaka kujitenga katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo, nchi za Ulaya zikiwemo Ujerumani na Ufaransa zinafanya juhudi za kumaliza mgogoro ulioko kwa njia ya mazungumzo. Wiki iliyopita, viongozi wa Ufaransa na Ujerumani waliongoza juhudi za kusaka amani Ukraine na matokeo yake ikawa ni kukutana ana kwa ana Marais Petro Poroshenko wa Ukraine na Vladmir Putin wa Russia katika mji wa Minsk huko Belarus. Viongozi hao walisaini makubaliano ya usitishaji vita ingawa hadi sasa utekelezwaji wake bado unakabiliwa na changamoto chungu nzima.
Ingawa waratibu na wacochezi wa mgogoro wa Ukraine wako nje ya nchi hiyo, hapana shaka kwamba, raia wa nchi hiyo ndio wanaoteseka na kuathiriwa nao. Takwimu zinaonyesha kuwa, tangu kuanza mgogoro huo mwaka mmoja uliopita, zaidi ya watu 5000 wameuawa, maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamia ya maelfu ya wengine kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.
0 comments:
Post a Comment