Ulishawahi kujiuliza maswali juu ya mtangazaji nguli wa BBC Salim kikeke,Je Unafahamu yaliyokuwa nyuma ya pazia angali ukitamani kipaji chake Soma hiki uone ilikuwaje.
Uliyafahamu haya kumhusu Salim Kikeke? Ni mtangazaji mashuhuri wa
shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Je, alifikaje? Na kabla
alitokea wapi?
Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo
Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa
kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa
labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke.
Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.Kwa karibu
mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani
Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu
kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi.
Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama
wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani kutumika kuingia kwenye
mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini. Baada ya kushauriwa na
mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es Salaam.
Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda kijiweni mitaa ya
Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake, Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni
marehemu.
Mara baada ya kuona matumaini yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo,
Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa maisha baada ya kupiga hodi katika
ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo
ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni Magic FM.
Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi huo, haikutokea kama ajali,
bali ilitokana na ushawishi aliokuwa ameupata kutoka kwa mama yake mzazi
ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Mama yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa kuingia katika
utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za redioni na
alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea duniani,
nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema
Kikeke.
Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika katika ofisi za kituo cha
kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa wanaita Magic FM, walikuwa
wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba kufanya kazi bure,
nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema Kikeke
Jambo la kujifunza hapa ni kwamba wakati mwingine katika kusaka ajira,
kubali kufanya kazi bila ya malipo, onyesha jitihada zako, huenda ikawa
ni njia nzuri ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo yale ambayo
huenda mtu amekwenda kwa ajili ya masomo kwa vitendo. Njia sahihi ya
kukaa katika ajira usiyo na ujuzi nayo
Anasema baada ya kupata uhakika wa kuendelea na kazi hiyo, Januari mwaka
1998, Kikeke aliamua kwenda kusoma kozi fupi ya Utangazaji habari
katika chuo cha uandishi wa habari cha ‘Tanzania School of Journalism
(TSJ)’.
”Pale nilisoma cheti kwa miezi mitatu na kurudi tena kazini, nikaanza
kusoma habari za kiingereza na Kiswahili wakati mwingine nilikuwa naenda
kutafuta habari,” anasema Kikeke.
“Hata hivyo mwezi mmoja baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo
nisingependa kufafanua zaidi,” anasema.
Wakati mwingine hata baya lina uzuri wake
Kikeke baada ya kufukuzwa kazi, hakuishia kulia mtaani, badala yake
alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena kwenye taasisi yenye hadhi ya
juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998.
”Kwa kipindi hicho Abdul Ngarawa alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa
idhaa ya Kiingereza, ‘English Service’, na kuandaa vipindi vya muziki
kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke
na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa muda ‘part-time.
Alianza kupangiwa vipindi vya kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya
mwaka mmoja. “Baadaye nikapewa kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa
wakati wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa
mtangazaji wa mwanzoni kabisa katika kipindi hicho,” anasema Kikeke.
Katika kipindi hicho, Radio Tanzania walianzisha kituo cha matangazo cha
FM, kiitwacho PRT kikitoa matangazo kwa lugha ya Kiingereza.
RTD na Kituo cha PRT ndizo kwa sasa zinafahamika kama TBC na TBC1. “Mimi
nikaondoka pale na kurudi tena CTN,” anasema.
Kurudi CTN
Baada ya kurudi katika kituo hicho, Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya
kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti wakati kampuni hiyo ilipouzwa
na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na DTV. Baadae alihamia ITV.
Kuingia ITV/Radio One.
Baada ya hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo
cha Radio One.
“Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Radio
One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi chochote nilichowahi
kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila nikawa na ya TV”,
anasema Kikeke.
Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya abadilishe mlango wa kutoka Redio One
na kuingia ITV. “Charles Hilary akaipeleka ile demo upande wa
televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce Mhaville,
wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,” anasema.
Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi vya taarifa za habari
kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo mambo yalibadilika kwa
muda mfupi pale ofisini.
Radio One walikuwa ni Redio washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba
wa kuchukua mtangazaji mmoja kila mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao
makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa.
Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC, ambako
anaendelea hadi leo.
Kikeke ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu. Ni baba wa mtoto mmoja
ambaye anasoma darasa la saba nchini. “Huku London ninaishi peke yangu,”
anasema.
0 comments:
Post a Comment