WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR) na kuwataka viongozi wa siasa wawahimize wanachama wao wajitokeze kwa wingi bila kujali tofauti za kiitikadi.
Ametoa wito huo leo mchana
(Jumanne, Februari
24, 2015)
wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliofika kushuhudia
uzinduzi huo uliofanyika kwenye kata ya Lumumba, Halmashauri ya Mji wa
Makambako, mkoani Njombe.
“Ninawasihi viongozi wa siasa
tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli za
kukatisha tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na lina nia
ya kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale
wasio na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo.
“Wale waliokwishafikisha
miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza
kupiga kura kama hawatajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”
aliongeza.
Akiwa uwanjani hapo,
Waziri Mkuu alishuhudia uandikishaji wa wakazi watatu wa kata hiyo ambapo zoezi
zima lilidumu kati ya dakika tatu na dakika tano. Kisha alikabidhi kadi kwa
mpigakura wa kwanza kuandikishwa ambaye alitumia dakika tatu kamili.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwamba zoezi la uandikishaji
lililoanza jana katika mji wa Makambako lilizidi matarajio ya Tume ya
kuandikisha wapigakura 1,850.
“Nimefarijika sana na
taarifa ya Mwenyekiti... Mlianza na kata tisa zenye vituo 54 na mlitarajia
kuandikisha watu 1,850 lakini badala yake mmepata watu 3,014. Hili limenipa
faraja sana. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo,” alisema.
Mapema,
akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kufanya uzinduzi huo, Jaji
Lubuva alisema ana imani wadau mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi
washiriki zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura.
Alisema uboreshaji wa
daftari hilo utafanyika kikanda na kwamba wamepanga kutumia siku saba kwa kila
kituo huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayebakizwa bila kuandikishwa
wakati ameshafika kituoni.
Aliwataka watu wanaokwenda
kujiandikisha wawe na vitambulisho vyao vya zamani vilivyotolewa na Tume ya
taifa ya Uchaguzi kwani tayari vina taarifa zao kwa hiyo vitapunguza muda wa
mtu kuandikishwa. “Kadi za Tume (NEC) au za NIDA kwa wale wachache ambao
wanazo, wakija nazo zitapunguza muda wa uandikishai sababu zina taarifa kwenye
kanzidata,” alisema
Akitoa ufafanuzi kuhusu
mfumo wa uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo
wa upigaji kura wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai bali
mfumo huo unafanya kazi kwa kutumia alama muhimu za mpigakura.
“Mfumo huu unatumia alama
zaidi kwanza ikiwa ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za
vidole na tatu ni saini ya mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama za mtu
mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu wa mikono,” alisema.
Alisema uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapigakura ni hatua ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi
kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi hilo.
Waziri Mkuu ameondoka
Makambako na anaelekea Mbeya kuanza
ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 24, 2015.
0 comments:
Post a Comment