KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, watu wenye ulemavu wa ngozi
(Albino), wamepigana ngumi na mateke wakigombea kuingia kumwona Rais
Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi ambapo
lilianzia kwenye eneo la mapokezi Ikulu mara baada ya walemavu hao
kukaguliwa na kuwekwa kwenye chumba maalumu cha kupumzikia wageni.
Baada ya muda, ofisa wa Ikulu alifika kwenye chumba walipokuwa walemavu
hao akiwa na karatasi yenye orodha ya watu 15, ambao ndiyo waliopaswa
kumwona Rais.
Baada ya ofisa huyo kuanza kusoma majina ya wahusika, albino wote
waliokuwa kwenye chumba hicho walinyanyuka kutoka kwenye viti vyao na
kusimama karibu na mlango, ambako alikuwa amesimama.
Kila ofisa huyo alipokuwa akisoma jina, mhusika alitoka nje ya chumba hicho tayari kwa kwenda kumwona Rais.
Baada ya ofisa huyo kumaliza kusoma majina hayo, alisema: “Hawa ndio
wanaokwenda kuwawakilisha kwa sababu hamuwezi kuingia kundi lote hili.”
VURUGU
Baada ya majina hayo kutajwa, mmoja wa albino hao, Nuru Chagutu, ambaye
hakutajwa, alisema hakubalini na kitendo cha viongozi pekee kumwona Rais
ili hali wajumbe wengine ambao pia ni wahathirika wa mauaji ya albino
wakibaki getini.
Alisema pia yeye na wanaharakati wenzake wa Chama cha Tunataka Haki ya
Kuishi (THK), hawamtambui Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi
Tanzania (TAS), Ernest Kimaya, ambaye alikuwa kwenye orodha ya watu 15
waliopangwa kumwona rais.
Alihoji pia sababu za Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu
Tanzania (Shivyawata), Amon Mpanju, ambaye si mlemavu wa ngozi, kuwamo
kwenye orodha hiyo huku akiwa si mlemavu wa ngozi.
“Kama huyu mtu mweusi (Mpanju) ataingia pamoja na mwenyekiti (Kimaya) na sisi tutaingia, vinginevyo mkutano ufe,” alisema Nuru.
Baada ya maelezo hayo, watu waliokuwa wamechaguliwa nao walionekana
kutoridhishwa na kauli ya Nuru, hivyo kukaibuka kurushiana maneno kati
ya pande hizo mbili.
“Kama sisi hatuingii, chukueni simu zenu tutoke wote, hakuna kubaki mtu
ndani, wote tuondoke, mkutano umekufa,” alisikika mtu mwingine akisema.
Baada ya kurushiana maneno kuzidi, ofisa mmoja na Ikulu aliamuru
walemavu hao pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye eneo hilo
watoke nje.
Baada ya amri hiyo, watu wote walitoka nje ya chumba hicho cha mapokezi
na kuendelea kurushiana maneno wakiwa kwenye viwanja hivyo vya Ikulu.
Ofisa huyo wa Ikulu aliwafuata tena na kuwaambia: “Ninaposema mtoke nje, ninamaanisha ni nje ya geti.”
Baada ya kauli hiyo, wale waliokuwa wametajwa majina tayari kwenda
kumwona Rais, walirudi tena kwenye chumba cha mapokezi kuchukua simu zao
tayari kwa kutoka nje ya geti.
“Chukueni simu tuondoke, hakuna kubaki mtu, leo hakuna kusaini (kuchukua fedha),” alisikika mmoja wa walemavu hao akisema.
NJE YA GETI
Baada ya kutoka nje ya geti la Ikulu, waliendelea kumwandama Kimaya
kwamba hawamtambui na kuwa hata ofisi alizokuwa akizitumia kwa sasa
zimefungwa.
“Yanapotokea matukio ya mauaji tunapowaambia viongozi wetu atumwe hata
mwakilishi, wamekuwa wakikataa huku wakisema ‘kufa, kufaana’, hiyo si
sahihi, wao wananeemeka na kuota vitambi na kupewa magari, lakini sisi
tumekuwa tukiendelea kuteseka,” alisema Nuru.
Baada ya kauli hiyo, Kimaya alimpiga teke Nuru huku akimwambia; “huwezi
kutunyima haki ya kuingia kwenye kikao kumsikiliza Rais.”
Baada ya Kimaya kumpiga Nuru, walemavu wengine waliokuwa wakimpinga mwenyekiti huyo wa TAS, walianza kumshambulia kwa maneno.
“Kwanini unampiga Nuru wakati anakwambia ukweli? Kwanza muda wako
ulishakwisha. TAS hakuna viongozi na ofisi zimefungwa…hatukubali,
tunakupiga na kwenye kikao tunaingia wote?” alisikika mmoja wa walemavu
hao aliyetambulika kwa jina la Amon Anastaz.
Baada ya vurugu hizo kuendelea kwa dakika kadhaa, ofisa wa Ikulu
aliyekuwa na beji kifuani yenye jina la Andrew M.M.S, aliwataka walemavu
hao kupanda magari waliyokuja nayo na wakachaguane ili wapate
wawakilishi wanaowataka.
Walemavu hao kwa ujumla wao walitii amri hiyo na kuondoka.
POSSI AWASIKITIKIA
Dk. Abdallah Possi, mtaalamu wa sheria ambaye alikuwa miongoni mwa
walemavu wa ngozi ambao walikuwa waingie kwenye kikao hicho, alisema
kitendo kilichofanywa na wenzake hao ni cha aibu.
Alisema kitendo hicho si njia ya kupata suluhisho la matatizo yanayowakabili watu wa jamii hiyo.
“Tukio la leo ni aibu sana, jamii haiwezi kutuelewa kwa sababu
tunagombana wenyewe kwa wenyewe badala ya kukaa na kuangalia namna
ambavyo tunaweza kusaidiwa, badala yake tumeanza kutupiana maneno na
kupigana.
“Kinachotakiwa sasa ni kukaa pamoja na kuelewana kwani sisi wote ni kitu
kimoja, tunahitaji msaada wa jamii yote, tuna haki ya kuishi kwa amani
bila kubaguliwa au kuuliwa katika nchi yetu,” alisema.
Alibainisha kuwa kiini cha vurugu hizo hakijui zaidi ya kuona ngumi,
jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kuna tatizo ndani ya chama chao.
Alisema kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kuwasaidia ili kuondoa
mgogoro ndani ya chama hicho ambao unaweza kuongeza matatizo badala ya
kuyatatua.
Baada ya tukio hilo, ambalo lilidumu kwa takribani dakika 30, waliokuwa
wameteuliwa kuongea na rais, walipata fursa hiyo baada ya wale waliokuwa
wakileta vurugu kuondoka eneo hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment