WAKAZI wa Kijiji cha Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, jana
walilazimika kufukua makaburi mawili walimokuwa wamezika watoto watano
wa familia moja waliofariki dunia juzi baada ya mvua kubwa ya mawe
kunyesha kijijini hapo.
Ufukuaji wa kaburi hilo ulifanyika mchana na kuitoa miili ya watoto hao,
Luku Masemba (14), Paschal Masemba (11), Mulyante Masemba (9), Sesela
Masemba (7) na Masele Masemba (5).
Taarifa zilizopatikana zinasema kuwa kaburi hilo lilifukuliwa baada ya
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kuagiza lifukuliwe ili marehemu
hao wazikwe kila mmoja katika kaburi lake.
Kabla ya agizo hilo lililotolewa na Mpesya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Ali Rufunga, miili ya watoto watatu wote wa kike ilikuwa
imezikwa katika kaburi moja.
Wakati watoto hao wa kike walikuwa wamezikwa katika kaburi moja, maiti
mbili za watoto wa kiume zilikuwa zimezikwa katika kaburi moja.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, maiti hizo zilikuwa zimefungwa kwenye mifuko
ya sandarusi baada ya wananchi kukosa sanda kutokana na Serikali
kuchelewa kutoa utaratibu wa namna ya kuzikwa miili hiyo.
“Nimeambiwa mmewazika hawa watoto watatu kaburi moja na wengine kaburi lao moja. Hapana, hapana, huu siyo utaratibu hata kidogo.
“Nataka hawa marehemu wafukuliwe na kila mmoja azikwe kwenye kaburi lake siyo kama mlivyofanya ninyi.
“Suala la kuzikwa watu kwa pamoja labda itokee hawatambuliki na ndugu zao hawajajitokeza.
“Hawa watoto ni wa familia moja na mnawafahamu kwa majina na umri wao, iweje muwazike kaburi moja watatu na jingine wawili?
“Naagiza wafukuliwe na wazikwe upya katika mazingira ya binadamu,” alisema Mpesya.
Familia nyingine iliyopoteza watu watano kufuatia mafuriko hayo ni ya
Donald Lubunda iliyo umbali wa kilomita moja kutoka mahali ilipo familia
ya watoto hao watano.
Mahitaji ya msaada
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwakata, Shaban Jumanne, alisema zaidi ya
tani 20 zinahitajika haraka kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko
hayo na kwamba kati ya watu 42 waliofariki dunia, wengi wao ni watoto
wa kuanzia umri wa miaka 14.
“Wakazi zaidi ya 4,370 katika kaya 456 zilizoathirika na janga hili
hawana makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na kuangushwa na mvua.
“Walioathirika zaidi wanafikia watu 300 na mbuzi 86, kuku 78, ng’ombe
watano, bata zaidi ya 30 na paka zaidi ya 20 wamekufa katika maafa
haya,” alisema kiongozi huyo wa Serikali.
Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alisema yeye binafsi
ametoa msaada wa mifuko 200 ya unga yenye thamani ya Sh milioni tatu.
Alisema maafa hayo yalitanguliwa na mafuriko mengine yaliyotokea katika
Kijiji cha Segese jimboni humo na kuharibu nyumba zaidi ya 55.
Pamoja na hayo, alimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuagiza Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waende kijijini hapo kuwasaidia waathirika
hao.
PINDA AWASILI
Kutokana na tukio hilo, jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwasili
kijijini hapo na kuagiza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya
Kahama, kuhamishia shughuli zote za uratibu wa maafa katika kambi hiyo.
Aliagiza pia maofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutembelea
eneo la maafa na kufanya tathmini kwa ajili ya kuiongezea nguvu
Hospitali ya Wilaya ya Kahama inayohudumia waathirika.
“Watu 42 waliofariki dunia katika janga hili ni wengi sana, nataka
shughuli zote za uratibu wa maafa zihamishiwe hapa kwenye kambi.
“Serikali kwa upande wake, itatoa misaada yake mikubwa na hakuna
atakayekosa msaada huo maana tumejipanga vizuri,” alisema Waziri Mkuu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi,
aliiambia MTANZANIA kuwa hospitali yake ilizidiwa na wagonjwa na
kulazimika kuomba msaada kwa hospitali za jirani.
Juzi ililiripotiwa watu 42 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 91
wamejeruhiwa vibaya baada ya mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo
mkali kunyesha katika Kijiji cha Mwakata, Kata ya Isaka, Wilaya ya
Kahama, mkoani Shinyanga.
Pamoja na vifo hivyo, nyumba za makazi na majengo ya taasisi mbalimbali,
yamebomolewa na mafuriko yaliyosababishwa mawe kusambaa kijiji kizima.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, aliiambia MTANZANIA kwa simu
juzi kwamba zaidi ya kaya 100 zimeathiriwa na mvua hiyo, nyumba 160
zilibomolewa na zaidi ya watu 600 hawana makazi.
Kuhusu vifo vilivyotokea, Mpesya alisema kuna baadhi ya familia
zilipoteza watu wote na nyingine zilipoteza baadhi ya wanafamilia.
“Kuna familia moja ilikuwa na watu saba wote wamefariki dunia, familia
nyingine ilikuwa na watu watano, wote wamepoteza maisha na familia
nyingine zilipoteza watu kadhaa tu,” alisema Mpesya.
Katika maelezo yake, Mpesya alisema mvua ya mwisho kubwa kunyesha mkoani
Shinyanga ilikuwa Septemba 4 mwaka jana ambako mabwawa ya maji katika
Mgodi wa Dhahabu wa Bulyankulu yalifurika maji na kutiririsha maji ya
kemikali katika maeneo ya makazi ya wananchi.
Wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, mtoa taarifa mwingine
aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Karandi, mkazi wa Kijiji cha
Mwendakulima ambaye alikwenda kijijini hapo baada ya mvua hiyo kunyesha,
aliiambia MTANZANIA kwa simu juzi kwamba mifugo mbalimbali ikiwamo
ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, nguruwe na mingine, imekufa maisha
kutokana na kukumbwa na mafuriko.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment