Kutupiana mpira kulijitokeza jana baada ya Spika
wa Bunge, Anne Makinda kusema Bunge linasubiri taarifa rasmi ya
kufukuzwa uanachama kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kutoka NEC,
ambayo hata hivyo, nayo ilisema inasubiri taarifa kutoka Chadema huku
chama hicho kikisema kinashughulikia kwanza kesi zinazowakabili
wanachama wake wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu
wake, Dk Willibrod Slaa.
Wakati Makinda akieleza hayo, taarifa kutoka kwa
watu wa karibu wa mbunge Zitto zilieleza kuwa leo ataibuka bungeni kwa
nia ya kuwaaga wabunge kama alivyoahidi wiki iliyopita.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Zitto alishindwa
kukubali wala kukataa, lakini akathibitisha kuwa atahudhuria kikao cha
Bunge leo.
Chadema ilimvua Zitto uanachama wiki iliyopita saa
chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka
chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa
nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote. Alipata amri
ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akifafanua suala hilo, Makinda alisema, “Unajua
suala hili lilikuwa mahakamani, hivyo ni lazima tupewe taratibu zote za
kimahakama. Kama kila kitu kikiwasilishwa moja wa moja uamuzi huo
utatangazwa wazi. Unajua suala hili lipo wazi na sisi kama Bunge
tunachokisubiri ni taarifa tu.”
Hata hivyo, alisema kwa muda uliobaki wa miezi
saba kabla ya uchaguzi mkuu, haiwezekani ukafanyika uchaguzi mdogo
katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, “Labda kama ingekuwa imebaki miezi 12
au zaidi kabla ya uchaguzi mkuu, hapo ungeweza kufanyika uchaguzi
mdogo.”
Katika mkutano wake na waandishi wa habari
alioufanya muda mfupi kabla ya kuwaaga wananchi wa jimbo lake Jumapili
iliyopita, Zitto alisema hatima yake ya ubunge itajulikana wiki hii kama
Bunge likipata taarifa za yeye kufukuzwa uanachama.
Alisema iwapo hatua hiyo itakamilika, ataeleza
hatua ambazo atazichukua na kufafanua kuwa mpaka sasa hajapata barua ya
wito wa kwenda kujitetea katika Kamati Kuu ya Chadema, hivyo mpaka sasa
bado ni mwanachama wa Chadema.
Alisema ataendelea kuwatumia Watanzania akiwa
mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini na kusisitiza kuwa atatoa
kauli iwapo atagombea ubunge katika jimbo lipi na kwa tiketi ya chama
kipi cha siasa.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba aliliambia
gazeti hili jana kwa simu kwamba bado hawajapata taarifa ya maandishi ya
kufukuzwa kwa Zitto, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.
Gazeti hili lilipowasiliana na Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema – Bara, John Mnyika kama chama hicho kimetoa taarifa za Zitto
NEC kuhusu kuvuliwa kwake uanachama, alijibu kuwa viongozi wakuu wa
chama hicho wanashughulikia kesi zinazowakabili wanachama wa chama hicho
wanaotuhumiwa kumpiga aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Slaa.
0 comments:
Post a Comment