MVUA zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha watu waliopoteza maisha kwa kufariki dunia kufikia saba, huku nyumba zaidi ya 200 zikiwa zimezingirwa na maji katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Uchunguzi uliofanywa na TAMBARARE HALISI umebaini kuwa katika maeneo ya Buguruni Kwa Mnyamani baadhi ya nyumba bado zimengirwa na maji na kusababisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo kuhama kwa muda.
Mkazi wa Buguruni kwa Mnyamani, Mussa Abdallah, akiongea na TAMBARARE juu ya kuharibika kwa miundombinu ya makaravati amesema kumechangia na maji kutuama kwenye makazi yao.
“Hakuna daraja ndiyo maana maji yametuhama kwenye nyumba zetu, tunaiomba Serikali iweze kuchukua hatua za dharura kwa kujenga daraja ili tuweze kupunguza hali hii,” alisema Abdallah.
Alisema kutokana na mvua hizo, wamepata hasara kubwa ikiwamo kuharibika kwa mali zao vikiwamo vyombo vya ndani jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira ya umasikini.
“Vitu vyangu vyote vimeondoka na maji na kubaki masikini, jambo ambalo limenirudisha nyuma kimaendeleo, kutokana na hali hiyo, ninaiomba Serikali inisaidie,” alisema.
Alisema licha ya mvua kusomba vitu hivyo, lakini hawezi kuhama kwa sababu hawana mahali pa kwenda, na kwamba Serikali imeshindwa kuwasaidia kwa lolote.
“Hadi sasa hatujapata msaada wowote kutoka serikalini na kwamba hatuna pa kwenda, jambo ambalo linanifanya nishindwe kuhama kwenye nyumba yangu,” alisema.
Katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole na Mkunduge, Kigogo Bonde la Mto Msimbazi, Kinondoni Bonde la Mkwajuni, Jangwani na Magomeni Sunna, pia baadhi ya nyumba bado zimezingirwa na maji huku wananchi wakiwa wamehama kwa hofu ya kupoteza maisha.
“Nyumba zetu zimechukuliwa na maji kutokana na mvua zinazonyesha, hali iliyosababisha kuhamia nyumba za jirani kwa ajili ya kuomba hifadhi,” alisema Juma Hussein mkazi wa Tandale kwa Mkunduge.
Kutokana na mafuriko hayo, wameiomba Serikali kurekebisha miundombinu ya maji ikiwamo kujenga mifereji ya kisasa itakayoweza kusafirisha maji kwenda kwenye mkondo wa Mto Ng’ombe.
“Tumeamua kuhama kwa muda ili kupisha mvua ambazo tunahofu zinaweza kutuletea madhara, bila ya kufanya hivyo tunaweza kufa maji,” alisema Yusuph Hamis, mkazi wa Kigogo.
KAULI YA RC
Akizungumza na waandishi wa habari ,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alisema hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi za kuzibua mifereji katika eneo la Buguruni Kwa Mnyamani.
Alisema kwa sasa wanasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuweza kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao wameathiriwa na maji.
“Bado hatujajua kuna mahitaji gani kwa wakazi wale walioathirika na mvua hizi, tunawaomba viongozi wa Serikali za mitaa watuletee taarifa haraka ili tuweze kujua nini kinahitajika kama ni chakula na dawa basi tupeleke haraka.
“Kwetu ni vigumu kujua zaidi ya kutegemea taarifa kutoka kwa viongozi wetu wa mitaa ambao ndio wamekuwa wakiratibu shughuli za wananchi wao siku hadi siku,” alisema.
Alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo ambao wanaishi mabondeni na pembezoni mwa mito kuhama ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea katika kipindi hiki cha mvua.
Alisema Serikali haitatoa msaada wowote kwa wananchi watakaoathirika na mvua hizo, hasa wakazi wa mabondeni ambao walitakiwa kuondoka kwenye maeneo hayo lakini wamegoma kufanya hivyo.
“Hakuna msaada wowote ambao tutatoa kwa wananchi wa mabondeni na walio kando ya mifereji ya maji kwa sababu tulishatoa tahadhari ya muda mrefu lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji,” alisema.
KOVA NA MAFURIKO
Akitoa taarifa ya maafa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, alisema watu wengine wawili wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Alisema kutokana na watu hao, kunafanya idadi ya watu waliofariki dunia kwa mvua hiyo kufikia saba.
Kamishna Kova, alisema vifo hivyo vimetokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kuanguka kwa nyaya za umeme katika eneo la Kimara Stop Over.
“Taarifa ambazo tunazo sasa watu wengine watano walifariki dunia juzi baada ya nguzo ya umeme kusombwa na maji na kuangukia nyumba,” alisema.
Alisema kati yao, wawili walifariki baada ya kutoa msaada wa kusukuma gari, jambo ambalo lilisababisha kupigwa na shoti ya umeme.
“Dereva wa lori alienda kuomba watu msaada wa kusukuma gari lake ambapo watu wawili walikubali na kwenda kumsaidia.
“Baada ya hapo, walikanyaga maji yaliyokuwa yameangukiwa na nyaya za umeme na kupigwa shoti iliyosababisha kupoteza maisha,” alisema Kova.
0 comments:
Post a Comment