Vugu vugu la kuelekea uchaguzi mkuu ngoma nzito CCM watoana macho upande wa Urais
JOTO la Uchaguzi wa Rais ndani ya CCM linazidi kupanda huku makada na viongozi wa chama hicho wakipigana vijembe hadharani.
Hali hiyo inatokana na kile kinachojitokeza sasa, kuibuka kwa makundi ya jamii, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kuwashawishi makada kadhaa wa CCM wawanie nafasi hiyo ya uongozi wa nchi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Makada ambao wamekuwa wakishawishiwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wakati baadhi ya makada wengine wanaotajwa kutaka kuwania urais ndani ya CCM wakimlalamikia Lowassa, wachambuzi wa siasa wamekuwa wakihoji mpango wa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alipochapisha vitabu na kugawa kwa wajumbe wote wa mkutano mkuu, lakini makada wenzake wamekuwa kimya, hawajalalamikia kitendo chake hicho.
Mbali na hilo, pia anadaiwa kuwa alinunua simu za Gallaxy Sumsang zaidi ya 140, akazigawa kwa wajumbe wa Baraza la Vijana la CCM (UVCCM) Zanzibar suala ambalo bado hadi sasa hajalitolea ufafanuzi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye anatajwa kuwapo katika mbio za urais, alikuwa akitembea na mabango ya kuonyesha watu wakimwomba agombee jambo ambalo lilimfanya aandikiwe barua na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kusitisha ziara zake ambazo zilitajwa kuwa za kampeni za kuwania urais. Wafuasi wa Mwigulu pia wanadaiwa kuandika katika mawe makubwa katika barabara nchi nzima kwamba yeye ndiye Rais 2015.
Lowassa Jana, Lowassa amejibu mapigo na kusema hawezi kuwajibu wanaosema anawalipa wanaomshawishi kuwania nafasi hiyo, kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili na wanachofanya ni upuuzi na uongo.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais akisema kuna watu wanatumia vibaya umasikini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea ujumbe wa wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya kuwagharamia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi, na kwamba wengi wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.
“Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja) kusema leo kuna mtu (Makamba) kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo kidogo, nikimjibu nitakuwa nampa heshima, kwahiyo nampuuza, sina uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu.
“Ni mapenzi yao kwa taifa lao na Mungu wao, lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo,” alisema Lowassa.
Akizungumza juu ya ujio wa wachungaji hao, Lowassa alisema umeandika historia katika maisha yake kwani hakutegemea kupokea kundi kubwa kama hilo la watumishi wa Mungu.
“Wote waliokuja nimewaeleza kuwa hili ni suala kubwa linalohitaji sala na mimi ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu,” alisema.
Mapema, mratibu wa wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.
“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.
Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.
Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi, Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni, Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.
Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe na Kilolo.
Awali Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa wanalipwa, wameishiwa, wamefilisika na sasa wanatapatapa.
Alisema kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.
Mgeja alisema wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya si makosa.
“Nitaadharishe tu, tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni, suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi.
“Kama viongozi tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka mbele, niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna mwingine zaidi ila mheshimiwa Lowassa,” alisema Mgeja.
BULEMBO AIBUKA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, amewataka wajumbe 20 wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo waliokwenda kwa Lowassa kumwomba agombee urais, wajitokeze na kukanusha kauli hiyo.
Juzi wajumbe hao walikwenda kwa Lowassa eneo la Area C, Manispaa ya Dodoma na kumwambia jumuiya hiyo inamtaka agombee urais na kumchangia Sh 600,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bulembo, alisema wajumbe hao wa Baraza waliokwenda sio wasemaji wa chama na wala hawakutumwa na jumuiya.
“Tunawataka wajumbe wote 20 waliokwenda wakanushe kwenye vyombo vya habari ndani ya mwezi huu, mbali na kukanusha, Kamati ya Maadili ya Jumuiya itawajadili na kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni na miiko ya uongozi,” alisema.
Pamoja na kutoa tamko hilo, Bulembo yeye binafsi amekuwa mstari wa mbele kumuunga mkono na kumfanyia kampeni Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika harakati za kuomba kuteuliwa na chama hicho.
Wanafunzi wamvaa January
Siku moja baada ya Nabu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kusema watu wanaoenda kwa Lowassa wanahongwa, viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara waliofika kwa waziri huyo juzi, wamesema wamedhalilishwa kwa kauli hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, viongozi hao walisema kauli hiyo inaashiria kuwadharau na kutaka watu wanaotoa matamko kama hayo wawaombe radhi.
Rais wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Angelo Madunda, alisema walifikia uamuzi wao baada ya kukaa chini kama wasomi na kukubaliana kwa mtazamo chanya kwamba Lowassa anawafaa.
“Watanzania wenyewe watafakari na kuangalia hili suala kwa ukubwa wake, pale kwa Lowassa hakukuwa na masufuria ya ubwabwa wala nini, Lowassa ni kama klabu ya mpira ana mashabiki wake, sisi ni sehemu ya hao mashabiki wake, wengine nao watafute mashabiki wao wawafuate,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga), Nobati Pangaselo, alisema kutokana na kauli zilizotolewa juu ya safari yao ya kwenda kwa Lowassa, ameamini kuwa hata kauli nyingine zinazosemwa juu ya waziri mkuu huyo wa zamani ni za uongo.
NYALANDU NA KINANA
Machi 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Madhehebu ya Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa, alimjia juu Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, kutokana na kauli anazozitoa kwa watendaji wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sheikh Alhad alisema baadhi ya kauli za Kinana anazozitoa kwenye mikutano ya hadhara zinawavunja moyo watendaji wa Serikali katika kutimiza wajibu wao.
Wiki iliyopita, Kinana alikaririwa akiwa mkoani Singida akisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, hana anachokifanya, badala yake anazurura tu na kwamba anathamini wanyama kuliko binadamu.
“Kamati imesikitishwa na kauli hii iliyolenga kumbeza au kubeza jitihada za Nyalandu. Tunaona kama inalenga kumvunja moyo. Ni vizuri mtu anapojituma apongezwe na huo ndio uadilifu.
“Mafaniko yamepatikana mengi chini ya uongozi wake (Nyalandu), iweje leo mtu hodari na mchapakazi kama huyu avunjwe moyo kwa kuambiwa eti anazurura tu badala ya kupongezwa?” alihoji Sheikh Alhad.
Alimtaka Kinana kuwa makini na kauli zake anapopokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kumtaka atumie busara anapotoa maelekezo kwa viongozi.
NAPE NA MIPANGO
Kutokana na mvutano ulioibuka ndani ya CCM, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema makada wa chama hicho wenye kupanga mipango ya kuiangusha CCM iwapo hawatateuliwa kugombea urais, wanajisumbua kwani wataanguka wao na kukiacha chama hicho kikiwa imara.
Kauli hiyo aliitoa juzi Arusha Mjini wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara ya Kinana mkoani Arusha.
“Wapo wanachama wanaopanga mipango haramu ya kukiangusha chama endapo hawatateuliwa kugombea urais. Wenye mipango hiyo wanajidanganya kwani hawatafanikiwa na wajue wazi kabla ya kuiangusha CCM wataanguka wao,” alisema Nape.
KINANA NA CHAMA
Kwa upande wake, Kinana alisema moja ya kazi anayofanya ni kujenga heshima ya CCM na kubwa zaidi kuwa msemaji wa wananchi.
“Zipo changamoto kutoka kwa wana CCM wasiopendezewa na hatua yangu hii. Hata hivyo sitarudi nyuma pamoja na baadhi ya watu kutaka kunikatisha tamaa,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vigumu kwa watu hao kumwondoa katika nafasi yake hiyo kwa vile anazo baraka za Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.
0 comments:
Post a Comment