Lowassa: Siwezi kuzuia mafuriko kwa mikono
SIKU moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kusema Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ameanza kampeni na yuko hatarini kutolewa kwenye mbio za urais, kiongozi huyo amesema uamuzi wa chama hufanywa kwenye vikao na hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono.
Jana, Nape alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kitendo cha Lowassa kupokea makundi mbalimbali nyumbani kwake mjini Dodoma yanayomshawishi kuwania urais ni kuanza kampeni na yuko hatarini kuenguliwa.
“Labda niweke vizuri hili, mtu yeyote anayekiuka kanuni hatapitishwa, labda kama anakwenda kugombea kwa chama kingine.
“Kinachofanyika Dodoma kwa watu kuchukuliwa na magari huku wengine wakiwa hawajui, halafu wakifika wanakuta viti vimeshapangwa na vyakula, halafu eti wanamshawishi kugombea, ni kukiuka kanuni na anaweza kuondolewa,” alisema Nape.
MAPIGO YA LOWASSA
Akizungumza jana baada ya kupokea vijana takribani 60 waliotoka Mbarali mkoani Mbeya kwa bodaboda, Lowassa alisema mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama.
“Mnazungumza mnaelewana mnatoka. Mambo ya chama hayawezi kuwa kwenye vyombo vya habari; Tv, redio, mara huyu hivi, huyu hivi, mkiona chama kinakwenda kwenye utaratibu huo ni hatari sana,” alisema.
Alisema anategemea mambo hayo yanayozungumzwa yatajadiliwa kwenye vikao vya chama.
“Na utaratibu huu ulioanza na watu (wa kukutana na makundi ya watu), mimi ni vigumu kuuzuia. Mimi ni vigumu kuzuia mafuriko kwa mikono.
“Nazuiaje mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli?
“Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia, ila nashauri tufanye hivi, wengine ambao hawajaja wanisikilize, hebu tusubiri chama kitoe maelekezo, kama wamesema hii inatafsiriwa kwamba ni kampeni, tungoje basi waseme tufanye nini watu wanaotaka kuja kushawishi.
“Rais alikuwa Songea kule, na mimi nilikuwapo kiwanjani pale, akasema mkiona hao waliopo hawatoshi, bado muda upo, washawishini wengine waingie.
“Sasa mkifanya hivi ni kosa, ni kampeni, ipi siyo kampeni sasa. Ipi ni kampeni, ipi siyo kampeni?” alihoji Lowassa.
Alisema CCM anayoijua ni ya vikao, hivyo hakusudii kujibu hoja za watu hao, kwani rafiki yake Hussein Bashe ameshazijibu vizuri.
“Sikusudii kusema zaidi ya hayo yaliyosemwa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Hussein Bashe.
“Niseme mawili tu yanayonisikitisha, wanasema mnakuja nimewaiteni ninawapa fedha, hela za kuwapa ninazitoa wapi? Mkija hapa nikiwawekea maturubai ni kosa, mkiwa na viti ni makosa na wanasema nawapikieni chakula. Mambo ya ajabu sana, yanasemwa na watu wazima, watu wenye heshima zao,” alisema.
Alisema ni vibaya kudhalilisha watu na kuwaona kwamba maisha yao yote na akili zao zinafikiria tumbo pekee.
“Kwahiyo, mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa awape chakula, ni kudhalilisha watu,” alisema.
Alisema watu wanafika nyumbani kwake kwa utashi wao, gharama zao wenyewe na wala si yeye anayewashawishi waende kwake.
“Nimewahi kuja huko Mbarali kuwashawishi mje kwangu? Au nimewapeni hela leo mlipokuja hapa? Hata soda zenyewe hamjanywa.
“Yananisikitisha sana maneno hayo, lakini hayanikatishi tama, nitaendelea kama iivyo kawaida,” alisema.
ATOA NENO
Lowassa alisema wale waliopanga kwenda nyumbani kwake kumshawishi ni vyema wakasubiri ili chama kitoe mwongozo.
“Tungoje tupate maelekezo, mimi nina hakika tutapata nafasi, jambo moja nina hakika na ninataka kuwapa matumaini, ipo siku Watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi.
“Ipo siku watapiga kura zao kusema naam ama hapana, kwahiyo tungojee hiyo siku. Nina hakika wapo Watanzania wengi wanaonipenda kama walivyosema kwa kazi zangu, watapata nafasi ya kusema naam ama hapana.
“Kwahiyo, huyo anayepiga kelele nyingi sijui nitoke chama sijui nifanye kitu gani angoje wana CCM na Watanzania waamue. Mimi ni mwanademokrasia, naamini kwenye demokrasia, lakini naamini kwenye utendaji bora,” alisema Lowassa.
Alisema walichofanya vijana hao kusafiri kwa bodaboda kilomita 600 kutoka Mbarali hadi Dodoma, ni kazi kubwa ya utashi mkubwa.
Lowassa alisema ana Watanzania wengi wanaomwamini kwa mambo aliyoyafanya akiwa serikalini, hivyo watu wamuhukumu kwa mambo hayo.
“Naomba waendelee kunihukumu kwa niliyofanya na yoyote nitakayoyafanya kwa nafasi yoyote nitakayokuwa nayo kwenye nchi hii.
“Nawashukuru sana kwa kuja, karibu sana, nasikitika kwa maneno haya mliyoyasikia, lakini kwa viongozi wa chama hakuna maneno ya mitaani, hufanywa kwenye vikao vya chama, ndiko uamuzi hufanyika, maneno mengine haya msiyasikilize, endeleeni na morali wa kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi,” alisema Lowassa.
BODABODA WANAFANYA KAZI KUBWA
Alisema waendesha bodaboda wanafanya kazi kubwa ambayo watu hawaijui.
“Wanafanya kazi kubwa ya ulinzi na usalama, kama siyo bodaboda watu wengi zaidi wangeuawa, kwahiyo kwa kweli wanasaidia na wengi (bodaboda) ni vijana, wanatakiwa kusaidiwa zaidi ili wapate ajira zaidi.
“Mimi nitaendelea kushirikiana nao siku zote katika nafasi yoyote nitakayokuwa nayo,” alisema.
BODABODA WANENA
Mwenyekiti wa waendesha bodaboda wilayani humo, Yahya Katagara, alisema kundi lao linamuunga mkono Lowassa kutokana na utendaji na msimamo wake wa kutetea wanyonge.
Alisema baada ya ujenzi wa shule za kata chini ya usimamizi wa Lowassa, vijana wengi walikabiliwa na tatizo la ajira na ndio ambao wameamua kujiingiza kwenye ajira ya bodaboda ambayo nayo iliasisiwa na Lowassa.
Katagara alisema waendesha bodaboda 60 wametoka Mbarali bila kushawishiwa wala kushurutishwa, na wamefanya hivyo kutokana na mapenzi yao kwa Lowassa.
KAMANDA WA VIJANA MBARALI
Awali Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Mbarali, Ibrahim Mwakabwanga, alisema wamefika kwa kiongozi huyo kwa gharama zao na watu wanaozuia watu kwenda kwake wanawanyima haki yao.
“Wanaokerwa kwa sisi kuja hapa kukushawishi wanatunyima haki.
“Ukiona mchezaji anakabwa na wachezaji zaidi ya watatu hadi inakuwa penati, ujue ni mchezaji makini. Sisi tuko nyuma yako, tunakuunga mkono na wewe usisikilize maneno ya mtaani wala usirudi nyuma,” alisema Mwakabwanga.
Alisema hivi sasa kila mtu (ndani ya CCM) ana mgombea wake anayemuunga mkono, na kwamba muda ukifika watavunja makundi na kumuunga mkono mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho.
Kwa takribani majuma mawili sasa nyumbani kwa Lowassa, mjini Dodoma, makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakipishana na kupigana vikumbo yakimshawishi awanie urais baadaye mwaka huu.
Walianza wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Wilaya ya Arumeru, kisha marafiki wa Lowassa, Kanda ya Kaskazini na uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma).
Baadaye, walikwenda nyumbani kwake masheikh 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Walikwenda pia wanafunzi wa vyuo vikuu sita mkoani Dodoma, wenyeviti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, wamachinga na waendesha bodaboda zaidi ya 350 kabla wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini kufuata nyayo hizo juzi.
0 comments:
Post a Comment