Image
Image

Ukawa wagawana Majimbo 211 ambayo ni sawa na asilimia 88 kati ya majimbo yote 239


KAMATI maalumu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 211 ambayo ni sawa na asilimia 88 kati ya majimbo yote 239, imefahamika.
Wakati hayo yakiendelea, kamati hiyo imeshindwa kuafikiana katika majimbo 28 ambayo yanasubiri uamuzi wa wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, ambao watamaliza kiporo hicho mwezi huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa juu wa umoja huo, kutangaza mkakati wa kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Ukawa ni umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo maalumu ya Ukawa, kiliiambia MTANZANIA jana kuwa kwa muda wa wiki moja sasa, kamati hiyo imekamilisha kazi hiyo kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limeelezwa linaweza kutoa upinzani mkali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu.
“Tumekutana mara kadhaa na kukubaliana kuachiana majimbo. Tulijadili katika hatua za awali, na sasa kazi imekamilika kwa asilimia 88 na kubaki asilimia 12 ambayo itaamuliwa na wenyeviti.
“Majimbo 28 ambayo tumeshindwa kupata mwafaka tunaamini kamati ya kitaifa ya Ukawa inayoundwa na wenyeviti ndiyo itatoa dira ya nini kifanyike, ingawa sisi kama kamati maalumu tumekamilisha kazi yetu.
“Kamati ilitafiti namna gani bora ya kuachiana madiwani, wabunge na rais ili tusimamishe mgombea mmoja katika kila eneo, lakini tulivutana kwani kila upande uliangalia masilahi yake, ingawa katika suala linaloitwa la ushirikiano ni lazima ukubali kupoteza sehemu na ninaamini Ukawa sasa itakuwa imara zaidi,” kilisema chanzo chetu.
MAJIMBO YA DAR ES SALAAM
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo maalumu, mgawanyo wa majimbo kwa Mkoa wa Dar es Salaam umeangalia vigezo vya kukubalika kwa mtu pamoja na yalipo makao makuu ya chama.
Kutokana na hali hiyo, Chadema imekubaliwa itasimamisha wagombea katika majimbo ya Ubungo, Kawe, Kinondoni na Ukonga huku CUF ikiachiwa majimbo ya Segerea, Temeke na Kigamboni na NCCR-Mageuzi ikipewa Ilala.

KILIMANJARO
Chanzo hicho kiliyataja baadhi ya majimbo ambayo yamepitishwa uamuzi kuachiwa Chadema kuwa ni Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Rombo, Same Mashariki, Same Magharibi, Hai na Siha, huku NCCR-Mageuzi ikiachiwa Vunjo na Mwanga.

KIGOMA
Mgawanyo huo umeifanya NCCR-Mageuzi kuachiwa kusimamisha wagombea katika majimbo sita ya Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Buhigwe, Muhambwe, Buyungu na Kigoma Kusini na Chadema ikibaki na Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini.

MAJIMBO TATA
Katika majimbo 28 ambayo ni tata, kamati hiyo maalumu imeitaka kamati ya kitaifa ya Ukawa kuwezesha kukubaliana kwa baadhi ya vyama ambapo katika Jimbo la Mtwara Mjini NCCR-Mageuzi na CUF vinatakiwa kukaa na kukubaliana kuachiana.
Mbali na hilo pia katika Jimbo la Babati Vijijini, Chadema na NCCR-Mageuzi wanatakiwa kukaa na kukubaliana namna ya kuachiana.

MAJIMBO YA WAPINZANI
Kamati hiyo maalumu ya wataalamu wa Ukawa imeshauri kuwa kwa majimbo yanayoongozwa na wabunge kutoka upinzani kwa sasa yatabaki kwa vyama husika bila vyama vinavyounda Ukawa kuteua wagombea wengine.

WENYEVITI KUAMUA
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa ndani ya kamati hiyo maalumu, wajumbe walikubaliana kusitisha mazungumzo hayo na kuiachia kamati ya wenyeviti wa vyama kitaifa itakayokutana mapema mwezi huu.
“Kamati imefanya kazi yake na sasa tupo kwenye maandalizi ya kikao cha viongozi wa kitaifa ambao ndio watatoa dira ya namna ya kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu ujao hasa kwa majimbo ambayo tumekubaliana kupitia vikao vyetu.
“Kama wakifikia mwafaka na kila chama kuridhia, ni wazi siku za Serikali ya CCM kuendelea kuwa madarakani zinahesabika,” kilisema chanzo chetu.

VIONGOZI WA VYAMA WAJICHIMBIA
MTANZANIA ilipotaka kupata ufafanuzi kutoka kwa viongozi wakuu wa vyama hivyo jana, mara zote walikuwa wakisema wako kwenye vikao.
Ingawa hawakueleza ni vikao gani walivyokuwa wakihudhuria, inasemekana walikuwa kwenye vikao vya vyama vyao kujadili namna kupanga mikakati kwa majimbo 28 yaliyosalia ambayo yanahitaji kuamuliwa na viongozi wa juu wa Ukawa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment