Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Aprili 27, 2015) wakati
akifungua kongamano la siku tatu kuhusu Uongozi na Usimamizi wa Mifumo ya
Takwimu liliondaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Takwimu (International
Statistical Institute – ISI) kwenye hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wakuu wa taasisi za takwimu barani Afrika
wanaoshiriki mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Kongamano hilo limekusanya
washiriki zaidi ya 50 kutoka nchi 31 za Afrika zinazozungumza Kiingereza kwa
nia moja ya kuweka msukumo kwenye umuhimu wa matumizi ya takwimu katika kuleta
maendeleo ya nchi husika.
“Kama nchi, Tanzania tunakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa
takwimu lakini tumeanza kulitazama jambo hili na ndiyo maana nimesema Serikali
imedhamiria kuiwezesha taasisi hii ya takwimu ili itoe takwimu sahihi kwa
Serikali kwa upande mmoja na kwa wananchi kwa upande mwingine…wao ni wadau
wakuu wa takwimu hizi,” alisema Waziri Mkuu.
“Tuna lengo la kuifanya taasisi hii iwe na hadhi ya kimataifa
katika kutoa takwimu zake. Sote tunatambua kwamba ulimwengu wa sasa ni wa
kidigitali, na bila kuwekeza kwenye hilo hatuwezi kufika mbali,” alisema.
Aliwataka wakuu wa taasisi za takwimu barani Afrika waangalie
uwezekano wa kufanya kazi kwa karibu pamoja Halmashauri za miji na wilaya kwani
huko ndiko kwenye rasilmali kubwa ya takwimu na ndiko maendeleo ya wananchi
yaliko.
“Ukichukua mfano wa Tanzania, tuna Halmashauri za Wilaya na Miji
zaidi ya 160. Mkiamua kufanya kazi kwa karibu na Serikali za Mitaa mtapata
takwimu za ajabu kwani huko ndiko kwenye miradi yote ya maendeleo. Tukumbuke
kuwa asilimia 75 hadi 80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini,” alisema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua kongamano hilo, Waziri wa
Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema takwimu ni mali ya umma na
hazipaswi kutolewa kwa upendeleo.
Waziri Ghasia ambaye alizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha,
Bibi Saada Mkuya, alisema takwimu zenye ubora na ubunifu ni muhimu sana kwa
ajili ya kupanga kazi za maendeleo ya Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Dk. Albina
Chuwa alisema kuna haja ya Serikali za nchi za Afrika kuweka kipaumbele kwenye
suala la upatikanaji wa takwimu na lisiwe suala la kuchukuliwa kijuujuu tu,
bali lichukuliwe kama sekta kamili ya kipaumbele.
“Naziomba nchi za Afrika zianze kuchukulia takwimu kama sekta ya
kipaumbele kwenye mipango yao ya maendeleo ya Taifa… tunapokaribia kuhitimisha
muda wa kutekeleza malengo ya milenia (MDGs), tunapaswa kujielekeza kwenye
viashiria vipya zaidi ya 300 ambavyo vimeainishwa, hivi viko kwenye ngazi ya
kitaifa, kikanda na kimataifa”.
“Katika bara la Afrika, kama hatutaamua kuainisha viashiria vyetu
wenyewe kuanzia ngazi ya Kitaifa, wataibuka watu na kututengenezea viashiria
ambavyo havina uhalisia kwa sababu hawajui matatizo ambayo bara la Afrika linakumbana
nayo,” alisema Dk. Chuwa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMATATU, APRILI 27, 2015.
Irene K. Bwire
0 comments:
Post a Comment