Timu hiyo iliyoshiriki ikiwa mwalikwa pamoja na
Black Stars ya Ghana, ilikwenda kwa matumaini ya kuongeza chachu na ushindani
kwenye mashindano hayo ya Kanda yanayoshirikisha nchi kutoka Kusini mwa Afrika
zinazounda shirikisho la Cosafa.
Tunawapongeza Cosafa kwa kuipa heshima kubwa
nchi yetu na nafasi ya kupeleka timu ili kushiriki mashindano hayo, hata kama
imeondolewa mapema, tena kwa aibu ya aina yake ya kufungwa mechi zote tatu.
Tunaamini, kutolewa kwa Stars baada ya kufungwa
mabao manne bila kupata hata bao moja ni changamoto kubwa, hasa kwa benchi la
ufundi la timu hiyo chini ya kocha Martin Ignatius au Mart Nooij na matokeo
hayo yamethibisha kwamba soka ni mchezo mgumu unaochezwa uwanjani, wala si kwa
maneno.
Tunasema imepata fundisho ambalo Nooij na vijana
wake watalitumia kwenye mashindano mengine ambayo timu hiyo inashiriki mwaka
huu.
Tunatambua kuwa Stars haikuwa mtalii kule Afrika
Kusini, bali safari hiyo ilitosha kuwapa somo wachezaji wake na Watanzania kwa
jumla kuhusu soka na jinsi inavyochezwa kwa sasa ulimwenguni.
Tunashawishika kuamini kuwa Nooij, kocha ambaye ana
uzoefu mkubwa baada ya kuifundisha kwa mafanikio Mambas ya Msumbiji, atakuwa
amejifunza kitu kutoka kwenye mashindano hayo, hata kama timu yake imeaibishwa
kwa vipigo vitatu.
Tunasema, wachezaji wetu walioshiriki mashindano
hayo watakuwa wamefunguka macho na kutambua wapi walikosea, wapi wanahitaji
marekebisho, wanapojiandaa kuikabili Misri, timu ngumu na yenye ubora zaidi
kuliko zilivyo Swaziland, Madagacar na Lesotho, ambazo zimeifunga Stars.
Kwa maana hiyo, tunaamini hakuna sababu ya kuanza
kusaka mchawi na badala yake, Nooij na msaidizi wake, Salum Mayanga na
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi lazima
wakae chini kuangalia wapi Stars ilikosea, idara ipi inahitaji marekebisho na
kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Pia, tunaamini kuwa benchi hilo la ufundi litaangalia
kwa mfano, sehemu zote zilizopwaya, kwenye ulinzi, ushambuliaji au timu nzima,
si kwa lengo la kuifumua.
Tunashauri wairekebishe wakati wa kujiandaa na mechi
dhidi ya Misri kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka
2017 huko Gabon.
Tunasema, Nooij na wenzake wakubali kuwa kuteleza si
kuanguka na badala yake watumie mashindano ya Cosafa kuandaa timu ya ushindani
inayoweza kucheza na Misri mwezi ujao, ambayo itakuwa imejifunza kutokana na
makosa kule Afrika Kusini.


0 comments:
Post a Comment