Ni dhahiri sasa kuwa hatua ya
vikao vya juu vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa wamefungiwa kwa kuanza
kampeni mapema na kutangaza tarehe za kuanza kuchukua fomu, vimechochea
harakati za kusaka urais na kuongeza urefu wa foleni ya wanaotaka kuelekea
Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya
siku nne baada ya uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada
wake, kuanza kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni
mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa,
Profesa Sospeter Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa
wanatangaza nia hiyo wiki ijayo.
Wakati Makongoro akisema sasa
anajisikia kuomba kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni
3, Profesa Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku
Profesa Mwandosya akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya
kuanza kuchukua fomu kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa mada hao
ambao kwa muda mrefu hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha
ya makada waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita ‘safari ya matumaini’
Jumamosi mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa atafanya hivyo hivi
karibuni huko Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili
aweze kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis
Kigwangalla, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa
Mataifa (UN), Amina Salum Ali.
Katika mlolongo huo wapo
makada waliokuwa wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana ni hiyo
ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi,
mbunge huyo wa Afrika Mashariki alisema: “Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza
Watanzania katika ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa kufanya
hivyo vinaniruhusu.”
Makongoro alisema hayo wakati
akitoa shukrani kwa viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka
kazi alizofanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na
machifu walioshiriki hafla hiyo, walimtaka Makongoro ‘kuvunja tetesi’
zinazosambazwa kupitia vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na
kumtaka atamke wazi juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa
Busokelo, Prince Mwaihojo alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia
ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo
mazito akiwa mkoani hapo.


0 comments:
Post a Comment