Image
Image

NEC, uandikishaji usiende pamoja na kampeni


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wiki hii imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani kwamba Agosti 21 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea hao.
Kwamba, baada ya NEC kupitisha wagombea walioteuliwa, vyama hivyo vitaruhusiwa kuanza kampeni za uchaguzi huo siku inayofuata, yaani, Agosti 22 ambazo zitafanyika kwa siku 64 hadi Oktoba 24, mwaka huu. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumapili ya mwisho wa Oktoba ya mwaka wa tano tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa mwisho na kwa mwaka huu, Jumapili ya mwisho ni Oktoba 25.
NEC imefanya vizuri kuwafahamisha mapema wadau wa uchaguzi mkuu ambao ni vyama vya siasa lakini hasa Watanzania kwa ujumla, ambao ndiyo wenye uamuzi wa mwisho wa nani awe kiongozi wao katika ngazi fulani. Jambo jingine zuri ni kwamba, NEC imetoa ratiba yake baada ya vyama vya siasa kutangaza ratiba zao za uteuzi wa wagombea.
Lakini kwa ratiba hii NEC, inajua changamoto zinazoikabili? Je, ina uhakika kwamba kazi ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura itakamilika kabla ya kuanza kampeni za wagombea?
Maswali haya mawili ni muhimu kwa NEC. Kazi ya uandikishaji wapigakura ilianza Februari 23 mwaka huu katika Mkoa wa Njombe na lengo lilikuwa kama kazi hiyo ingekamilika kwa wakati Watanzania, waweze kushiriki kupiga Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa Aprili 30.
Kazi hiyo ilishindikana na hivyo Kura ya Maoni ikaahirishwa. Leo ikiwa ni miezi mitatu na siku kadhaa tangu NEC ianze kazi ya uandikishaji kwa mfumo wa BVR, imekamilisha mkoa huo mmoja tu wa Njombe kati ya 30 iliyopo. Hata mkoa huo mmoja bado kuna watu ambao hawakufikiwa.
Pamoja na majigambo ya viongozi wa Serikali kwamba kazi ile ingefanikishwa katika kipindi kifupi, ukweli ni kwamba NEC ilikuwa na mashine za BVR 250 tu kati ya 8,000 zilizokuwa zinahitajika kwa kazi hiyo kubwa. Mbaya zaidi ni kwamba NEC ilianza kazi hiyo nyeti ikitegemea mashine za kuazima kutoka Kenya na Nigeria waliokuwa na uchaguzi Machi 28.
Inasikitisha kuona kwamba hadi sasa NEC imepata mashine zipatazo 4,500 kwa kazi hiyo muhimu. Tunaambiwa imepeleka mashine hizo mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara na Lindi, Rukwa, Kagera, Singida na Tabora.
Tunaambiwa kazi inakwenda mchakamchaka lakini katika baadhi ya kata waandikishaji wapigakura wanadaiwa kuondoa mashine kabla ya kuandikisha watu wote waliojitokeza; maeneo mengine inadaiwa waliojiandikisha, kadi zao zinasomeka tofauti na vituo walivyoandikishwa.
Tunaambiwa maeneo yenye watu zaidi ya 3,000 waliandikishwa chini ya nusu yao huku baadhi ya vijiji, mashine ziliendelea kutowatambua wenye sugu za vidole.
Wakati NEC inakabiliwa na changamoto hizo, imetangaza kwamba kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza Agosti 22, ikiwa na maana kwamba hapo NEC itakuwa imekamilisha kazi yake, maana ikiwa itakuwa bado uandikishaji huo unaweza kuharibika na kuzua sokomoko na taharuki katika jamii.
Tunaishauri NEC ikamilishe kazi hiyo mapema ili kampeni zikianza, wananchi wapate fursa ya kwenda kuwasikiliza wagombea wanavyojinadi na kuuza sera badala ya kujiandikisha. Kazi ikikamilika mapema, NEC pia itapata muda wa kuhakiki majina na vituo bila usumbufu mkubwa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment