Chama cha Wamiliki wa vyombo
vya Habari Tanzania (Moat) kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni
Dodoma kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari
baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na
Serikali na ulitakiwa kuwasilishwa katika kikao kilichopita kwa hati ya dharura
jambo ambalo halikuwezekana baada ya kupingwa na wadau na baadhi ya wabunge.
Hata hivyo, muswada huo
uliorejeshwa kwa wadau kujadiliwa, unatarajiwa kupelekwa kwa mara nyingine
katika kikao cha Bajeti kinachoendelea ingawa si kawaida kwa Bunge la Bajeti
kujadili miswada ya sheria.
Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Moat, Reginald Mengi
(pichani) alisema baada ya kuusoma, wamegundua kuwa kuna kasoro nyingi na
miongoni mwake ni adhabu kwa waandishi wa habari ambazo zitawafanya wawe waoga
katika kufanya kazi yao.
Alisema wadau wa habari na
wataalamu wa sekta hiyo wataendelea kuwaelewesha wabunge juu ya masuala
mbalimbali yaliyomo katika muswada huo ili hata wanapoupitia wawe na uelewa wa
kutosha wa kitu wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Alisema licha ya kasoro hizo,
pia kuna hila za kuupitisha kwa haraka kusudi wasitoe mawazo yao juu ya
vipengele kadhaa ambavyo vinafinya uhuru wa vyombo vya habari na hata uhuru wa
wananchi kupata habari.
“Wanasiasa hawa walitumia
sana vyombo vyetu vya habari wakati wakitafuta kura na sasa wameshapata uongozi
wanatuona hatufai badala yake wanataka kutukandamiza kwa kutuwekea sheria
nzito,” alisema Mengi.
“Huu muswada ukipita, utakuwa
ni sheria mbovu ambayo haina manufaa kwa nchi yetu, pia Watanzania watakosa
habari za uhakika kwani ikiwa kila ufikapo muda wa taarifa ya habari saa 2.00
usiku wote wanalazimika kutazama Televisheni ya Taifa, sasa hii ndiyo nini?”
alihoji.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Mwananchi Communications Ltd, Francis Nanai alisema ni vyema magazeti yakatumia
nafasi iliyopo kuandika makala maalumu kila siku kuhusu muswada huo ili wananchi
wajue matatizo yake.
Alisema pia wamiliki na
waandishi wote wa habari kwa pamoja wajiunge na wanaharakati wanaotaka kwenda
mahakamani kuupinga muswada huo ambao ni aibu kwa Taifa.
“Ni vyema muswada ukafanyiwa
kazi baada ya uchaguzi wa Oktoba na rais ajaye ndiye auhalalishe kwa kutia
saini,” alisema.
Mkurugenzi wa Sahara Media
Group, Samwel Nyala alisema suala la kulazimishwa kupeleka taarifa zao kwenye
runinga ya Taifa, kila saa mbili usiku ni kuwanyima wadau wa habari haki ya
upatikanaji wa habari.


0 comments:
Post a Comment