Rais Jakaya Kikwete amewaaga
rasmi mabalozi 36 wa Tanzania katika mataifa mbalimbali akiwaeleza kuwa
hatakuwa madarakani baada ya Oktoba.
Rais aliwaaga mabalozi hao
jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu utakaohitimishwa leo, ambao pamoja
na mambo mengine, utajadili ‘Diplomasia ya Tanzania Kuelekea Dira ya Taifa
2025.’
“Huu ni mkutano wangu wa
mwisho kuzungumza nanyi. Mmenisaidia vizuri katika kipindi chote cha utawala
wangu na niwaahidi tu kuwa nitaondoka Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema
Rais Kikwete.
Pamoja na kuaga, aliwaachia
mambo manne ya kuzingatia ili kuifanya Tanzania iendelee kuheshimika kimataifa.
Mambo hayo yanajumuisha; kuwasaidia wawekezaji wa Kitanzania kupata fursa
katika nchi wanazoziwakilisha; kuwasaidia Watanzania walioko katika nchi
wanakowakilisha kuunda umoja wao; kuzishawishi asasi za kiraia za
kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kutengeneza marafiki wa Taifa kwa
ujumla.
Rais alieleza kuwa wakati
Serikali ikitekeleza mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati
ifikapo 2025, tayari kuna wananchi wenye uwezo wa kiuchumi ambao wameshaanza
kuwekeza katika baadhi ya nchi Afrika na hata nchi za Magharibi, hivyo ni vyema
wakapewa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma zao.
“Niwakumbushe tu kuwa mahitaji
yamebadilika nanyi pia badilikeni. Kwa sasa ni vyema vipaumbele vyenu vikawa
uwezo wa kuleta mitaji nchini, kiasi cha misaada ya maendeleo mlichochangia,
masoko kwa bidhaa zetu mliyoyabainisha na wawekezaji wa nje mliowashawishi kuja
kuwekeza,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Achaneni na ripoti zenu za
kila mwisho wa mwezi mnazoleta za malalamiko mara eeeh wanataka mabadiliko
kwenye cyber crime (Sheria ya Makosa ya Mtandaoni) au Sheria ya Takwimu. Hayo
masharti wanayotoa ndiyo maana ilifikia hatua nikasema kuwa kama hatuwezi
kupata mikopo bila masharti ni bora tusipewe tu.”
Rais pia aliwataka mabalozi
hao kuzihoji serikali za nchi waliko juu ya mchango wao katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake zinaziathiri sana nchi zinazoendelea
kama Tanzania.
Alifafanua kuwa kama jotoridi
la dunia litaendelea kuongezeka upo uwezekano mkubwa ifikapo mwaka 2030 Mlima
Kilimanjaro usiwe na theluji iliyopo sasa, hali itakayopunguza mvuto wake na
hivyo kuathiri utalii.
Alisema: “Ukame umeongezeka…
mwaka jana hatukupata mvua kabisa za vuli. Mazao yamekauka na ipo dalili kuwa
kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula mwaka huu.”
Aliongeza kuwa aliingia
madarakani nchi ikiwa haina adui na anaondoka nchi ikiwa hivyo pia na
kuwakumbusha kuwa ni vyema kila mmoja akajitahidi katika hilo.
Akimkaribisha Rais kufungua
mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
alisema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita nchi imeshirikiana vyema na mataifa
mengi ulimwenguni jambo lililowezesha kufunguliwa kwa Ubalozi wa The Hague
pamoja na kufutiwa madeni na ongezeko la misaada ya maendeleo.


0 comments:
Post a Comment