Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana wa
CCM kutokuwa makuwadi na madalali wa wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Rais Kikwete aliyasema hayo mjini hapa jana
alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo
vya Elimu ya Juu wa CCM.
“Vijana wasigeuke kuwa makuwadi wa kuwahonga vijana
wenzao ili wamchague mtu fulani. Kwa kufanya hivyo watakuwa wametoka kabisa nje
ya mstari.
“Tunataka vijana watakaosema tunatafuta viongozi wa
Taifa hili, ila watu wa aina hii hapana,” alisema Rais Kikwete.
Alisema lengo la kuanziasha shirikisho hilo ni
kuwaandaa vijana hao ili waujue uongozi na waweze kuwa viongozi wazuri katika
siku za baadaye.
“Viongozi wa vijana wanasafirishwa wanaletwa hapa
Dodoma kwa ajili ya kumsikiliza mzee fulani, ndiyo maana siku hizi hoja ya
vijana siyo tishio kwa mtu yeyote kwa sababu hawana mawazo ya kutoa kwa ajili
ya kukijenga chama na Taifa,” alisema Rais Kikwete.
Pia, aliwataka vijana hao kuhakikisha CCM
inaendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa hilo ndilo jukumu
lao.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi tunachotaka sisi ni
CCM iendelee kuongoza Tanzania na wapinzani waendelee kuisoma namba kama
ilivyokuwa kwa miaka mingine, nawaamini, nina matumaini na nyie pia CC ina
matumaini makubwa ya kukivusha chama hiki katika Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema
Rais Kikwete.


0 comments:
Post a Comment