Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho,
Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Nzega
katika ziara yake ya siku 10 mkoani Tabora.
“Hadi sasa hakuna matumaini kwamba Uchaguzi Mkuu
utafanyika kama ilivyopangwa, hivyo Rais lazima awepo nchini aangalie wapi
tumekwama na aingilie kati kunusuru mchakato huo,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kuwa makini,
vinginevyo uchaguzi utavurugwa.
“Tunatoa ushauri kwa Rais Kikwete kusitisha safari
zake za nje ya nchi ili aweze kuhakikisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu
yanakamilika kwa wakati, vinginevyo mambo yatavurugika,” alisema Profesa
Lipumba.
Mwenyekiti huyo wa CUF, pia alitoa wito kwa watu
wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura na asiwepo
mtu wa kuachwa kuandikishwa kwa kisingizio chochote.
Hata hivyo, aliilaumu Serikali kwa kile
alichokieleza kuwa imeipangia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), fedha kidogo kwa
ajili ya uchaguzi, jambo ambalo linaashiria kuwa hakuna maandalizi ya maana ya
Uchaguzi Mkuu.
Safari za Rais nje
Profesa Lipumba alisema safari za Rais Kikwete
nje ya nchi zinagharimu kati ya Sh5 bilioni na Sh10 bilioni. Alisema hayo
ni matumizi mabaya hasa kwa Serikali ambayo pia haiwajibiki kukusanya kodi
ipasavyo.
Profesa Lipumba pia aliishangaa Serikali kwa kutoa
misamaha ya kodi kwa kampuni mbalimbali, bila kuwa na vyanzo mbadala vya mapato
kwa ajli ya kuendeshea shughuli zake, akisema hatua hiyo ni hatari kwa ustawi
wa nchi.
Profesa Lipumba alisema kuwa kiinua mgongo cha Sh230
milioni kwa kila mbunge ni sehemu ya matumizi ya fedha za Serikali na ndiyo
kinachosababisha mivutano mikali wakati wa kura za maoni ndani ya CCM.
“Mkitaka maisha mazuri iondoeni Serikali ya CCM
isiyowajali wananchi wake na yenye matumizi mabaya ya fedha zenu wananchi,”
alisema.


0 comments:
Post a Comment