Siku mbili baada makada waliokuwa
wamefungiwa kwa makosa ya kukiuka kanuni za CCM kuachiwa huru, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameeleza nia yake kuwa wakati
ukifika atachukua fomu kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Membe alibainisha nia hiyo kwa mara ya kwanza juzi
usiku wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kuwa
atatangaza azma hiyo muda wowote kuanzia sasa akiwa jimboni kwake, Mtama mkoani
Lindi.
“Sasa ni rasmi kuwa nina nia ya kugombea urais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitatangaza nikiwa kijijini kwangu… mahali
nilipoanzia safari ya kwenda shule, safari ya kwenda usalama wa Taifa na safari
ya kwenda Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema.
Membe alikuwa miongoni mwa makada sita CCM waliokuwa
wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi
wakituhumiwa kuanza kampeni mapema kinyume na taratibu za chama hicho
kilicholazimika kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Makada hao walifungiwa tangu Februari, 2014 na
pamoja naye ni mawaziri wakuu wa zamani; Frederick Sumaye na Edward Lowassa;
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Akifafanua juu ya dalili za kutimia kwa ndoto yake
za kuiongoza nchi, Membe alisema Mwenyezi Mungu ana namna nyingi za kufikisha
ujumbe kwa mja ampendaye katika kumtumikia kwa mtindo autakao yeye. “Nimegundua
kuwa unaposema naomba nioteshwe… naomba nioteshwe kumbe Mungu anayo namna
nyingine. Anawaotesha wengine kwa ajili yako na ndivyo alivyofanya,” alisema.
Kuhusu hilo, Membe alisema kila mtu anasubiri kuona
CCM inatoka vipi na hata vyama vya upinzani vinasubiri hilo na ndiyo maana
navyo vimenyamaza.
Mpaka sasa ni chama cha Tanzania Labour (TLP),
kilichokwisha teua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo, Macmillan Lyimo.
“Watanzania wote macho yao yapo CCM, wanasubiri
kuona inafanya nini. Tunaona vyama vya vingine vimekaa kimya, wanasubiri CCM
iseme ili nao wafuate. Wanapiga kelele za Ukawa…Ukawa lakini hawawezi kufanya
chochote. Hata kama tutasogeza muda mbele bado wataendelea kusubiri,”
aliongeza.
Hali ya usalama Burundi
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hali
ya usalama inayoendelea kuyumba nchini Burundi kwamba kikao cha mawaziri
kinatarajia kuketi baada ya muda mfupi jijini Arusha ili kuona namna ya kutatua
mzozo uliopo.
Alisema Tanzania isingekwa radhi kuona mapinduzi ya
utawala wa Rais Pierre Nkuruzinza yanafanywa wakati akiwa nchini tena kwa
mwaliko na gharama za nchi hii. Alisema hiyo ingemaanisha Tanzania inahusika
nayo.


0 comments:
Post a Comment