Dodoma.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa
sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri
wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo
mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na
hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu
maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza
nia yake ya kugombea urais.
Kuhama
CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda
upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa
kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo
Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka
ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha
(AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye
ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Kimya
miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008
kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake
baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.
“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza, askofu
mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu. Nilichagua kuwa
kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza, ningezungumza ningeweza
kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo ambayo hayapo.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi
yake.... sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na
kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni
jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema
Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Wagombea wapime afya
Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka,
alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa.
Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna
watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani
kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na
kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia
kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama
chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi,
tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.


0 comments:
Post a Comment