London, England
Baada ya
wiki iliyopita Manchester United na Arsenal kutoka sare ya bao 1-1 kwenye
Uwanja wa Old Trafford, timu hizi zilionyesha kwamba haziwezi kuitoa Manchester
City katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England huku zikiwa
zimeishakubali Chelsea kuwa bingwa.
Jarida hili
la Spoti Mikiki linazichambua Manchester United na Arsenal kama zinaweza
kuizidi Chelsea msimu ujao na kutwaa ubingwa wa 2015/16.
Je, zina vikosi vitakavyowawezesha kutwaa
ubingwa au zinasajili wachezaji gani ili ziweze kutwaa ubingwa?
Arsenal
Miezi kadhaa
iliyopita nyota wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry aliwahi kukikosoa kikosi
cha Arsenal na kupendekeza kwamba kinatakiwa kufanya usajili haraka, Henry
alikuwa na pointi. Arsenal inatakiwa kuboresha idara ya golini. Kipa
Wojciech
Szczesny (ambaye alianza msimu huu akiwa chaguo la kwanza) na kipa David Ospina
(aliyemalizia msimu) wote walionyesha udhaifu kuliko makipa wengine wa timu
zilizo katika nafasi za juu katika msimu wa Ligi Kuu England. Katika kiungo,
kiungo mkabaji Francis Coquelin alijitahidi msimu huu, lakini Arsenal
wakimchukua na Morgan Schneiderlin wa Southampton watafanya vizuri. Katika safu
ya ushambuliaji mbadala wa Olivier Giroud unahitajika. Ni kazi kupata
washambuliaji bora, lakini Arsenal haina jinsi inatakiwa kusajili. Danny
Welbeck alijitahidi, lakini aliumia. Arsenal ipo vizuri katika safu ya ulinzi
wa kati na mwanzoni mwa mwaka huu ilimsajili beki Gabriel Paulista.
Manchester United
Usawa kwa wachezaji
katika kila nafasi ndiyo falsafa ya kocha Louis van Gaal wa Manchester United.
“Haijalishi
una kikosi kikubwa kiasi gani au idadi kubwa ya namba ya wachezaji,
kinachohitajika ni usawa wa wachezaji katika kila nafasi, ninapokuwa na
wachezaji wawili wenye uwezo wa juu katika kila nafasi basi huwa nina
furaha,”alisema Van Gaal.
Hata hivyo
tishio kubwa kwa Van Gaal ni taarifa kuwa kipa wake David de Gea anaoondoka na
kujiunga na Real Madrid. Ni taabu hivi sasa kupata kipa makipa wenye ubora wa
juu duniani. Hata hivyo Van Gaal akipata saini ya kipa wa Tottenham Hotspur,
Hugo Lloris atakuwa amelamba dume. Hata hivyo kocha huyu anatakiwa kusajili
zaidi, anatakiwa kusajili kiungo mwenye ubora wa juu kama Paul Pogba wa
Juventus, beki wa kulia kama Seamus Coleman wa Everton, beki wa kati kama Mats
Hummels wa Borussia Dortmund na washambuliaji kama Harry Kane wa Tottenham
Hotspur na Gareth Bale wa Real Madrid.
Je, makocha Arsene Wenger wa Arsenal
na Van Gaal wa Manchester United wafanye nini kubadilisha vikosi vyao ili
watwae ubingwa msimu ujao?


0 comments:
Post a Comment