Mchezaji huyo anayeichezea pia timu yake ya taifa,
amewaambia Yanga kwamba hajaja nchini kuuza sura, bali kufanya kazi na
ameangalia staili ya uchezaji ya Yanga kisha akasema: “Mbona freshi tu
hapa nitapiga kazi sana, mimi ni jembe.”
Naye wakala wake, Gibby Kalule, alisema Kamara ni
mchezaji mzuri lakini Yanga ndio yenye maamuzi ya mwisho kama kumsajili
au la, naye akasisitiza jamaa ni jembe.
Uongozi wa Yanga umemhakikishia maisha kiungo huyo
mrefu kuwa ukimwambia kuanzia Jumatatu kila kitu kitakuwa sawa huku
Mwanaspoti ikifahamu klabu hiyo inataka kujihakikishia juu ya idadi halisi ya
wachezaji wa kigeni watakaoruhusiwa kusajili msimu ujao.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kesho Jumapili
litakuwa na kikao kizito kitakachoamua mabadiliko ya idadi ya wachezaji wa
kigeni wanaopendekezwa kuzitumikia klabu shiriki za Ligi Kuu Bara kutoka watano
wa sasa hadi kuwa kumi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kamara alisema anasubiri
kwa hamu lolote ambalo Yanga watataka alifanye chini ya kocha Hans Pluijm.
Kamara alisema yuko tayari kufanyiwa majaribio
yoyote na Pluijm katika kupima ufanisi wake wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji
na hata mchezeshaji ambapo baada ya kuona soka la Yanga kwa sasa
amejihakikishia nafasi katika kikosi hicho.
“Nimekuja kufanya kazi hapa, ndiyo maana unaona
nafanya mazoezi yangu binafsi kujiweka sawa, sitaki kuharibu ubora wangu,
najiamini kwamba kazi naiweza nitawafanyia kazi Yanga ngoja tumalizane,”
alisema Kamara ambaye wakati wowote anaweza kupata taarifa za kuitwa baba kwa mara
ya kwanza.
Yanga kupitia Katibu wake, Dk. Jonas Tiboroha
aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa wamevutiwa na umbo la mchezaji huyo, pia hata
mikanda yake ya video lakini akataka wapewe muda.
“Tupeni muda kidogo tufanye majukumu yetu kwa kina,”
alisema Tiboroha.
Endapo Kamara atafanikiwa kusajiliwa na Yanga ni
wazi sasa safu ya kiungo mkabaji anayomudu kuichezea inaweza kuwa na ushindani
mkali.
Hiyo ni kutokana na ukweli kuwa tayari viungo Salum
Telela na kinda Said Juma Makapu wametangulia kujizolea sifa katika nafasi hiyo
katika mechi mbalimbali za Yanga.


0 comments:
Post a Comment