STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe amesema endapo
angejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu ufungaji bora ungemhusu, lakini
amewaambia waliokuwa wanamjaji kwa kutofunga katika Kombe la Mapinduzi kuwa
walikosea kwani hana bahati na Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tambwe alijiunga na Yanga Desemba mwaka jana baada
ya kutemwa na Simba na ameifungia timu hiyo ya Jangwani mabao 13 kwenye mechi
za ligi na mengine matatu katika mechi za kimataifa. Jumla Tambwe ana mabao 14
(moja alifunga akiwa Simba) kwenye mechi za ligi na ni wa pili kwa ufungaji,
anaongoza Simon Msuva mwenye mabao 17.
Straika huyo wa zamani wa Vital ‘O ya Burundi,
alisema kwenye kikosi cha Yanga ana wachezaji wengi wa kumchezesha na
kumtengenezea nafasi za kufunga tofauti na ilivyokuwa akiwa Simba.
“Hilo lipo wazi, kama ningeanza msimu na Yanga
ningemaliza mfungaji bora, nimecheza mechi chache na nimefunga mabao mengi,
kama zile mechi saba za mwanzo ningekuwa Yanga ingekuwa balaa,” alisema.
“Hapa Yanga nina watu wengi wa kunitengenezea
nafasi, kuanzia viungo hadi mawinga, hii ni tofauti na Simba ambapo watu wa
kazi hiyo walikuwa wachache.”


0 comments:
Post a Comment