Vijana mkoani Lindi wametakiwa kuwa wazalendo na
kutobaguana bali wasambaze upendo na kujiona wote ni sawa kwa kufanya hivyo
wataondoa chuki na kudumisha amani, mshikamano na umoja katika jamii
inayowazunguka.
Mwito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete wakati akifungua klabu zalendo zilizopo katika Manispaa ya
Lindi.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete alisema kama jamii itajenga tabia ya ubaguzi italeta chuki na
upendo utatoweka na hivyo kusababisha vurugu zitakazopoteza amani
iliyopo.
Alisema uzalendo ni kiini cha maendeleo hivyo huwezi
kuwa mzalendo kama hupingi rushwa na matumizi ya madawa ya kulevya, hutunzi
mazingira, hushiriki kuchangia utoaji wa damu salama na kutokuchangamkia fursa
mbalimbali za maendeleo zilizopo katika jamii yako.
Mama Kikwete alisema, “Leo hii nimezindua klabu
zalendo, Mzalendo ni mtu mwenye huruma na mtu anayeona thamani ya kitu
alichonacho tunzeni vitu mlivyonavyo ikiwemo Amani ya nchi yetu na mjitoe
kufanya kazi kwa bidii ili muweze kupata maendeleo.
Aidha Mama Kikwete aliwahimiza wanafunzi
kujitendea haki kwa kusoma kwa bidii hadi elimu ya chuo kikuu kwa
kufanya hivyo wataweza kuajiriwa na kujiajiri katika katika fani mbalimbali na
kujiletea maendeleo katika mkoa wao wa Lindi.
Akisoma historia fupi ya klabu zalendo Mwalimu
Mwajuma Malugu ambaye ni Mwenyekiti alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa klabu
hiyo ni kuutetea na kuulinda muungano wa Tanganyika na Zanzibari ndiyo maana
wanatumia namba za #26464#ikimaanisha tarehe 26 mwezi wa 4 mwaka 1964 siku ya
muungano.
Aliyataja malengo mengine kuwa ni kuhamasisha
wanafunzi na vijana waliopo mtaani kuwa wazalendo na kuipenda nchi yao kwa
kufanya hivyo wataepukana na mambo yasiyofaa kwa maslai ya nchi yao.
“Mafanikio tuliyoyapata ni kujenga umoja na
ushirikiano, kuongeza idadi ya wanachama na hii inatokana na kufunguliwa kwa
matawi mengine ya uzalendo mashuleni na mitaani, kuongeza na kupanua uelewa kwa
wanafunzi na raia kuhusu klabu ya uzalendo, kuwahamasisha watu kuwa
wazalendo na kujitoa katika uchangiaji wa damu, kupinga rushwa, madawa ya
kulevya pamoja na kulinda Amani ya nchi.
Mwalimu Mwajuma alizitaja changamoto wanazokabiliana
nazo kuwa ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kuandaa makongamao na mabonanza
yatakayosaidia kuimarisha harakati zote za klabu ya uzalendo na
kushindwa kutuma wawakilishi katika mikutano na makongamano ya wanaklabu ngazi
ya taifa.
Pia kikundi kimekosa semina kwa wanaklabu hali
inayoplekea wanachama kukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhumuni ya
klabu hiyo.
Klabu zalendo ilianzishwa na walimu wa Shule ya
Sekondari Lindi katikati mwa mwaka jana hadi sasa inawanachama 1450 kutoka
shule za Sekondari Mkonge, Angaza, Ngongo, Ng’apa, Chikonji, Mingoyo,
Kineng’ene , chuo cha ufundi VETA na walimu wa shule za msingi pamoja na
wanafunzi wao.
Pia klabu hiyo imehusisha vijana kutoka mtaani
wanaofanya kazi za udereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wavuvi na
wanavikundi vya Sanaa.
Mama Kikwete aliahidi kukipatia kikundi hicho mipira
20 na jezi seti 10 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ambao
watashiriki katika mashindano mbalimbali `na kuangalia utaratibu wa kuwapatia
mradi ambao utawasaidia kuwainua kichumi.
0 comments:
Post a Comment