Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa suluhisho la
kisiasa la matatizo ya sasa ya Burundi yatapatikana kwa wananchi wa Burundi
kuheshimimu Katiba na Sheria ya Uchaguzi na kuwa ni jukumu la jumuia ya
kimataifa kuisaidia nchi hiyo kuvuka katika changamoto za sasa.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumatatu, Mei 4, 2015
kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York wakati alipokutana na
Katibu Mkuu wa Umoja huo, Mheshimiwa Ban Ki Moon ambaye alimwuliza Rais Kikwete
kuelezea hali ilivyo Burundi mwishoni mwa kikao kati ya Ban Ki Moon na Wajumbe
wa Jopo la Watu Maarufu Duniani ambalo limeteuliwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon
kutafuta njia za jinsi dunia inavyoweza kukabiliana vizuri zaidi na magonjwa ya
milipuko katika siku zijazo.
Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete: “Mheshimiwa
Rais tuelezee kidogo hali ya Burundi kufuatia uamuzi wa Rais wa Burundi
kugombea Urais kwa mara ya tatu…uamuzi huu unaweza kuendeleza hali ya machafuko
na mauaji. Tunataka kujua maoni ya nchi jirani na Burundi na pengine wewe,
Mheshimiwa Rais, ni mmoja wa watu wachache, wachache sana duniani ambao
wanaweza kusaidia kubadilisha hali ilivyo katika Burundi.”
Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Ban Ki Moon: “Kama
unavyojua Mheshimiwa Katibu Mkuu kwa sasa mimi ni mwenyekiti wa EAC na
nimeagiza mawaziri wa nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kwenda Burundi
kuzungumza na wadau wote muhimu na baada ya hapo watuletee ripoti na kutushauri
jinsi tunavyoweza kusaidia katika Burundi.”
Rais Kikwete amesema kuwa mawaziri hao watakuwa
wamemaliza kazi yao mwishoni mwa wiki hii na baada ya hapo EAC itaweza kujua
nini la kufanya. “Aidha, kama unavyojua, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi
alikuwa Tanzania leo, akizungumza na Waziri wetu wa Mambo ya Mambo ya Nje
kuhusu hali ya Burundi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa majawabu ya
changamoto za sasa katika Burundi ni kwa wananchi wa Burundi kuongozwa na
Katiba ya nchi na Sheria ya Uchaguzi ya nchi hiyo. “Kama kuna watu wanadhani
kuwa uteuzi wa Rais wa Burundi kugombea tena urais nchini humo ni kuvunja
sheria, basi wafuate mkondo wa sheria kuweza kupata ukweli na majawabu siyo
kutumia nguvu”.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
5 Mei, 2015
0 comments:
Post a Comment