Wadau wa habari, ambao
wamekuwa wakipigania kupata sheria itakayowapa uhuru wa kukusanya, kuandika na
kusambaza habari kwa kuzingatia maslahi ya taifa, watafurahi kuona rais wao
anasaini, kuwa sheria, miswada yenye maudhui rafiki, lakini si kama ilivyo kwa
miswada hii miwili.
Harakati za wadau wa habari
zilianza katikati ya miaka ya 1990, kupigania chombo huru cha kusimamia
wanahabari ambacho ni Baraza la Habari Tanzania (MCT) na itungwe sheria mpya
itakayotoa uhuru wa habari.
Baadaye walijikusanya na
kuandaa miswada miwili; mmoja ni wa Haki ya Kupata Habari na wa pili ni wa
Huduma za Vyombo vya Habari na wakawasilisha serikalini. Serikali ilipokea
miswada hiyo na iliahidi kuiwasilisha bungeni, kwa mara ya kwanza mwaka 2007.
Hata hivyo, haikuwasilisha
miswada hiyo, badala yake ilianza kuhangaika kutunga vipengele vya marekebisho
ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 1993
kuongeza vifungo, faini ya mamilioni ya shilingi na kesi zilizofunguliwa dhidi
ya mwanahabari aliyeshitakiwa kwa kuandika habari za kashfa ziharakishwe
kusikilizwa. Wabunge walikataa marekebisho hayo wakataka Serikali iwasilishe
sheria nzima kama ilivyokubaliwa na wadau wa habari.
Katika namna inayoshangaza,
baada ya danadana za muda mrefu, Serikali iliwasilisha miswada hiyo katika Bunge
la Februari ijadiliwe, chini ya hati ya dharura. Wadau wa habari walijiuliza,
kwa nini Serikali iwasilishe miswada hiyo kwa dharura? Kwa nini iwasilishe
miswada hiyo bila kuwapa wadau fursa ya kujadili maudhui yake? Je, Serikali
inaogopa nini kukutana na wadau wa habari kujadili miswada hiyo?
Kumbe Serikali iliingiza
vipengele ambavyo si rafiki kwa wadau wa habari kwani badala ya kukuza uhuru na
maadili ya habari vinakandamiza uhuru na kupora haki yao kama ilivyoainishwa
katika Ibara ya 18 ya Katiba.
Katika miswada hiyo,
imependekezwa: Kiwango cha elimu kwa mwanahabari kiwe shahada ya kwanza; mtu
haruhusiwi kumiliki vyombo vingi vya habari; mwandishi atakayepatikana na kosa
faini Sh20 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote mbili kwa
pamoja kwa mshitakiwa atakayethibitishwa na mahakama kutenda kosa.
Vilevile, imependekezwa
vyombo vya habari vya binafsi kutakiwa kujiunga na Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) saa 2.00 usiku kila siku kwa ajili ya taarifa ya habari.
Vipengele hivi ni vizito na havifai.
Ni jambo zuri kwa mwanahabari
kuwa na elimu nzuri ili aweze kuwa na umilisi wa kazi yake ya kuhabarisha na
kuelimisha jamii, lakini tunajiuliza kwa nini sharti la elimu ya juu liwe kwa wanahabari
tu na siyo kwa walimu, mahakimu, na viongozi? Kwa nini Serikali inatunga sheria
kuvibana vyombo vya habari vya hapa nchini na siyo vya kimataifa?
Kwa nini mkazo wa adhabu
usiwe kwa mafisadi, wabadhirifu wa mali ya umma badala yake Serikali imewalenga
wanahabari? Kwa nini Serikali imevizia dakika za mwisho na kuanzisha mgogoro na
wadau wa habari tena kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu?
Tunawaomba wabunge, wapitie
miswada hiyo kwa umakini, waisome na kukataa vipengele vyote ambavyo havitoi
afya njema kwa tasnia ya habari. Wanahabari wanahitaji uhuru na jamii inataka
uhuru kwa kusoma na kusikia habari wanazotaka kutoka vyombo binafsi bila
kulazimishwa kwa sheria.
0 comments:
Post a Comment