Taarifa hiyo imebainisha kuwa
katika kipindi hicho, serikali imepoteza zaidi ya Sh. bilioni moja kwa
kuendelea kulipa mishahara hewa kwa watumishi wa umma waliofariki dunia,
waliostaafu na waliofukuzwa kazi katika halmashauri 36 nchini. Kiasi hicho
kimesababisha hasara kubwa kwani fedha hizo zilitengwa ili zitumiwe na
halmashauri na serikali za mitaa. Fedha nyingine kiasi cha zaidi ya Sh. milioni
140 zililipwa kwa wafu, wastaafu na watumishi wa umma walioacha kazi.
Taarifa hiyo ilifichua
vilevile kuwa zipo kampuni za madini zilizoisababishia serikali hasara ya Sh.
bilioni 22.33 kwa kuhujumu misamaha ya kodi waliyopewa. Maeneo mengine ambayo
wizi umeisababishia serikali hasara ni ule wa kuisamehe kodi ya zaidi ya Sh.
milioni 465 kwa kampuni moja ya Arusha, Sh. bilioni 2.3 zilizotumiwa na Mamlaka
ya Bonde la Ngorongoro kwa kununua bidhaa zisizokuwa na sababu ya msingi;
Kampuni ya Simu ya TTCL kufanya manunuzi yasiyokuwa ya lazima yenye thamani ya
Sh. milioni 381.97 na pia kasoro nyingine zimebainika katika Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) ambako kumefanyika manunuzi bila kushindanisha wazabuni, thamani
yake ikiwa ni Sh. bilioni 1.75. Yapo pia maeneo mengine mengi yaliyoainishwa na
CAG, na ambayo kwa ujumla yameisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha
za walipa kodi.
Sisi tunaona kwamba hali hii
haipaswi kuachwa. Haivumiliki. Kuna kila sababu kwa serikali kutumia vyombo
vyake vya dola kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika katika wizi wa fedha hizi
za umma wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Na hili linapaswa
kutiliwa mkazo. Vinginevyo, taarifa hii ya CAG itakosa maana.
Isipofanyiwa kazi haraka na
wahusika kuchukuliwa hatua, ni wazi kuwa hata taarifa yenyewe (ya CAG) itakuwa
ni muendelezo tu wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwani uandaaji wake
ulitumia fedha nyingi na muda katika kuikamilisha. Isitoshe, kwa kuwachukulia
hatua wahusika, ni wazi kwamba kutatoa somo kwa watu wengine wenye kujihusisha
na vitendo hivyo kutambua kuwa fedha za umma hazipaswi kuchezewa. Ni wazi
vilevile kuwa wananchi wenye kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi watafarijika
kusikia kuwa walaji wa fedha zao wanachukuliwa hatua zinazostahili. Wala si
vinginevyo.
Kadhalika, ikumbukwe kuwa
taifa hili ni changa sana kiuchumi. Kwa vigezo vyovyote vile, nchi yetu kwa
sasa haiwezi kukosekana katika kundi la nchi maskini sana duniani. Na ndiyo
maana licha ya kuwapo kwa jitihada zinazoendelea kila uchao katika kujikwamua
kiuchumi, bado kuna changamoto nyingi mbele yetu. Kuna utitiri wa vikwazo
katika kutekeleza miradi mbalimbali ili hatimaye kutimiza malengo tuliyojiwekea
kupitia 'Dira ya Taifa ya Mwaka 2025'.
Kwa mfano, hakuna asiyefahamu
kuwa maeneo mengi ya nchi yetu yanakabiliwa na ukosefu wa huduma za kijamii.
Hadi sasa baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, kuna maeneo mengi bado hayana
maji safi na salama. Yapo maeneo mengi pia yasiyofikika kwa urahisi katika muda
wote wa mwaka kutokana na ukosefu wa barabara. Upatikanaji wa huduma za afya ya
msingi pia ni tatizo kubwa, sawa na ilivyo kwa elimu ambako jitihada
zinaendelea kufanywa kukabiliana na uhaba wa walimu, ukosefu wa nyumba za
kuishi za walimu, ukosefu wa miundombinu muhimu na inayoendana na idadi ya
wanafunzi kama maabara na pia ukosefu wa vitabu na vifaa vya kufundishia.
Katika hali kama hii, ndipo
sisi tunapoona kwamba watu hawa waliokosa uzalendo, watu hawa wanaotumia mbinu
mbalimbali zikiwamo za kukiuka taratibu za fedha tulizojiwekea ili kujinufaisha
binafsi, kamwe hawastahili kuhurumiwa. Wachukuliwe hatua kali ili kuliepusha
taifa na aibu hii ya kuwapo kwa vitendo vya ufisadi kila uchao.


0 comments:
Post a Comment