Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
wa Tanzania Mhe. Bernard K. Membe jana aliongoza Jopo la Mawaziri wa Mambo ya
Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Burundi kwa lengo
la kupata hali ya maendeleo ya kisiasa nchini humo.
Wakiwa nchini humo, mawaziri hao walikutana na
kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi,
viongozi na wawakilishi wa vyama arobaini na tano vya siasa vya upinzani nchini
humo, ambapo walitoa salamu za Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Waziri Membe, kwenye mazungumzo yao na
Rais Nkurunziza yaliyodumu takriban saa moja na nusu, mawaziri hao walifikisha mwaliko
kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, kuhudhuria Mkutano wa dharura wa Wakuu
wa Nchi ambao umepangwa kufanyika Dar es Salaam Mei 13, 2015.
Kwenye jopo hilo la mawaziri liliongozwa na Mhe.
Bernard Membe wa Tanzania, walikuwepo pia Mhe. Balozi Amina Mohamed, Waziri wa
Mambo ya Nje wa Kenya na Mhe. Louise Mushikiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Rwanda, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda aliwakilishwa na Rtd Brig.
Matayo Kyaligonza Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Burundi.
“Lengo kuu la mkutano huo utakaofanyika jijini Dar
es salaam ni kujadili hali ya amani wakati wa kuelekea kipindi cha uchaguzi
nchini Burundi” Waziri Membe aliwaeleza waandishi wa habari waliokuwa
wakimsikiliza baada ya mazungumzo hayo.
Kwenye mazungumzo hayo ya Burundi Waziri Membe
alimuomba Rais Nkurunziza na viongozi wa vyama vya siasa nchini humo kutoa
maelezo, na maoni yao kwa jopo hilo kwa uwazi na kupendekeza namna ambavyo
viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakavyoweza kuisadia Burundi.
Pande zote mbili zilizoshiriki kwenye mazungumzo
hayo na jopo la mawaziri kwa nyakati tofauti walielezea kufurahishwa kwao na
hatua ya Rais Kikwete kuitisha kikao hicho cha Wakuu wa Nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili suala la Burundi kwa wakati muafaka.
Hadi wakati mazungumzo hayo, wakimbizi wapatao
ishirini na nane elfu wameikimbia nchi hiyo kwenda Rwanda na Tanzania ambapo
wengi wao wameingia nchini Rwanda.
“Hili ni janga la kibinadamu ambalo ni lazima
jumuiya yetu chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete kulipatia ufumbuzi kwa
haraka” alimalizia Waziri Membe.
Kwenye safari hiyo, Waziri Membe aliongozana na Wajumbe
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (NUU) pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Leticia Mageni Nyerere
(Mb.).
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI KWA UMMA,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
07 MEI 2015
0 comments:
Post a Comment