Image
Image

Blatter ameonyesha uwajibikaji, wengine wamfuate.


Mapema wiki hii, Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani (Fifa), Joseph Blatter alitangaza kuwa atajiuzulu nafasi yake na kuitisha mkutano wa dharura wa uchaguzi ili kumpata rais mpya.
Blatter alilazimika kujiuzulu kutokana na ongezeko la tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikilisikama shirikisho hilo kwa muda mrefu, hasa kutokana na kutoa uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia kwa nchi za Qatar na Russia.
Tuhuma hizo za rushwa ya Dola 150 milioni zinawahusu viongozi kadhaa wa Fifa pamoja na kampuni za masoko ambazo huhusika katika kutafuta wadhamini wa fainali hizo.
Tayari kiongozi wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Soka vya Amerika Kaskazini na Kati (Concacaf), Chuck Blazer amekiri kuhusika katika kupokea rushwa ili kutoa uenyeji wa fainali za mwaka 1998 zilizofanyika Ufaransa na za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini. Uchunguzi wa miamala mbalimbali ya viongozi wa Fifa bado unaendelea.
Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Blatter alisema; “wakati nina uhalali niliopewa na wanachama wa Fifa, sidhani kama nina uhalali kwa dunia nzima- mashabiki, wachezaji na klabu, watu wanaoishi, kupumua na kuupenda mpira wa miguu”, akimaanisha kuwa pamoja na kuchaguliwa kihalali na mkutano mkuu wa Fifa, haoni kama ni busara kuendelea kama wadau wengine wa soka hawamkubali.
Hii ni kauli ya kistaarabu na yenye kuonyesha kuwajibika kwa wadau wote wa soka duniani. Viongozi wengi wametumia fedha kujijengea mazingira ndani ya vyama vyao kiasi kwamba ni vigumu kuwaondoa kidemokrasia.
Badala yake, wanaposhindwa kuongoza vizuri na hivyo kusababisha watu wawalalamikie, hujitetea kuwa eti walichaguliwa kihalali na mkutano mkuu na hivyo hawawezi kung’atuka.
Blatter, ambaye wiki moja iliyopita alichaguliwa tena kuongoza Fifa kwa miaka minne, amekuwa mfano mzuri wa uwajibikaji wa kuzingatia masilahi mapana ya mpira wa miguu, hata kama wanaomchagua hawapendi aondoke.
Mtu anaposhika nafasi ya umma, ni lazima awajibike pale mambo yanapokwenda kombo au panapokuwapo na tuhuma luluki za rushwa au utendaji mbovu, hata pale kiongozi anapoona kuwa yeye binafsi si chanzo cha tatizo hilo.
Ni vizuri viongozi wetu wakajifunza kutoka kwa Blatter kuwa masilahi mapana ya Taifa ni kitu cha kwanza. Kwa hiyo, wanapokuwa madarakani wanatakiwa waitumikie jamii inayowazunguka badala ya kutumia fedha nyingi kujijengea mazingira ya kutoondolewa madarakani kidemokrasia wakati uwezo wa kuendeleza chombo walichopewa ni mdogo.
Sakata la Fifa pia limetupa somo jingine zuri kwamba kila kunapokuwapo na tuhuma za uhalifu kwenye vyombo vya michezo na vingine, taasisi za Serikali zinazojihusisha na uchunguzi wa masuala kama hayo hazina budi kufanya kazi yake ipasavyo.
Mfano, katika sakata la Fifa, kumekuwapo na tuhuma za kukithiri kwa rushwa katika uendeshaji, hasa kwenye utoaji wa uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment