Msajili ambaye ni Mlezi wa Vyama vya Siasa nchini
kwenye mkutano wake juzi na waandishi wa habari alikuwa na hoja kuu mbili,
kwanza ni kuendelea kukumbusha angalizo lake kwa vyama hivyo la kuvitaka viache
kuanzisha ‘majeshi’ kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi.
Hata hivyo, hoja ya pili na ndiyo msingi wa maoni yetu
ni kuhusiana na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010, ambapo rasimu yake
ilijadiliwa kwa siku mbili na vyama vya siasa chini ya aliyekuwa Msajili wa
Vyama vya Siasa, John Tendwa.
Mkutano wa Tendwa na wanasiasa hao ulielezwa
kukubaliana kwamba fedha anazopaswa kutumia mgombea urais kuanzia mchakato wa
kuteuliwa na chama hadi kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu usizidi Sh5 bilioni, na
fedha anazotakiwa kutumia mgombea wa kiti cha ubunge zimegawanywa kulingana na
jimbo.
Kwa mantiki hiyo, Jaji Mutungi hazungumzi kitu kipya
kwa wanasiasa hao, anachofanya ni kuwakumbusha wajibu wao wa kutekeleza sheria
walioshiriki mchakato wake, kwamba matumizi ya fedha kupita kiasi yanaweza
kuondoa sifa kwa mgombea au chama husika.
Sote ni mashahidi kwamba wakati Jaji Mutungi akitoa
angalizo, tayari Chama cha Mapinduzi kiko kwenye mchakato wa kumtafuta mgombea wake
wa urais, na minong’ono ya matumizi makubwa ya fedha imeshaanza.
Msisitizo wa Jaji Mutungi ni kwamba ofisi yake
itachukua hatua dhidi ya ukiukaji wa sheria hiyo endapo atapata ushahidi wa
kutosha. Hatujui Jaji Mutungi anataka ushahidi gani, lakini watangulizi wake ni
mashuhuda wa malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani kwamba chama tawala
kimekuwa kikitumia mali za umma, kama magari na majengo katika kampeni za
kisiasa za wagombea wake na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Tunajiuliza hawa watanganzania ndani ya CCM ambao
baadhi ni watumishi wa Serikali na katika mchakato wa kutafuta wadhamini
mikoani kwa mujibu wa taratibu za chama chao, wanadaiwa kutumia vyombo vya
usafiri vya Serikali na kuna wengine wanatumia watumishi na ofisi za Serikali
katika kufanikisha safari zao za kisiasa, wanaguswa na sheria hii?
Huko mikoani wanakokwenda kutafuta wadhamini vipi
kuhusu mapokezi wanayoyapata kutoka kwa viongozi wa Serikali wa maeneo hayo,
tunajiuliza hivyo sababu kuna baadhi ya watangazania wana nyadhifa kubwa serikalini,
hivyo kuwafanya ma-RC na ma-DC kulazimika kujumuika nao katika safari zao za
kisiasa, na wao sheria inawagusaje?
Pamoja na kuungana na Jaji Mutungi kuwaonya wanasiasa,
lakini tunajiuliza iwapo gharama za uchaguzi zilizowekwa na mtangulizi wake kwa
kushirikiana na wadau wa vyama vya siasa kama bado zinaweza kukidhi gharama za
wakati huu za kisiasa, hasa ikizingatiwa shilingi imeshuka thamani na gharama
za maisha zimepanda. Tunasema hongera kwa kazi uliyoianza, lakini una kazi
kubwa.
0 comments:
Post a Comment