Bajeti hiyo ni ya Sh22.49 trilioni na imelenga
kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa fedha za nchi wahisani na wafadhili.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya bajeti, Serikali imepania kupunguza utegemezi huo
hadi kufikia asilimia 8.
Pia, kwa maana hiyo, mkakati mkubwa utakuwa ni
katika kusimamia makusanyo ya kodi na mapato mengine, hali kadhalika kukopa
fedha kutoka taasisi mbalimbali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Uamuzi huo wa kupunguza utegemezi wa wahisani na
wafadhili unatokana na Serikali kuona kuwa fedha hizo hazina uhakika, hasa
wakati nchi hizo zinaposhinikiza Serikali kutekeleza jambo fulani kama
walipozuia fedha wakati wakishinikiza suala la sakata la uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow na lile la Epa.
Uamuzi huo umekuja wakati kukiwa na changamoto kubwa
ya makusanyo ya mapato kutokana na Serikali kushindwa kufikia malengo yake,
kushindwa kupata vyanzo vipya vya kodi na kushindwa kudhibiti wakwepa kodi.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, Serikali inatarajia
kukusanya Sh12,363 bilioni kutoka kwenye mapato ya kodi na Sh1,112.7 bilioni
kutoka kwenye mapato yasiyotokana na kodi.
Kwa tarakimu hizo tu ni dhahiri kuwa kuna kazi kubwa
ya kukusanya fedha kufikia takriban nusu ya kiwango cha bajeti ili Serikali
iweze kutekeleza sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo na shughuli nyingine.
Kwa mujibu wa mjadala wa bajeti za wizara
mbalimbali, Serikali haikuweza kupeleka fedha kwenye miradi mingi ya maendeleo
kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, jambo lililolalamikiwa sana na wabunge wakisema
maendeleo hayawezi kuja kwa shughuli za maendeleo kupata asilimia 30 tu ya
fedha zilizopangwa.
Wasiwasi wetu ni kwamba hali itajirudia tena mwaka
mpya wa fedha kwa Serikali kushindwa kukusanya fedha na hivyo kuzorotesha
utekelezwaji wa miradi ya maendeleo, jambo ambalo kwa njia fulani litazidisha
ugumu wa maisha kwa wananchi.
Ni vizuri kuondokana na utegemezi wa fedha kutoka
kwa nchi wahisani, lakini uamuzi huo ni lazima uendane na hali halisi ya humu
ndani na dhamiria ya kweli ya kuongeza juhudi za kukusanya mapato yanayotokana
na yasiyotokana na kodi.
Kwa mfano, ingeanza kwanza mikakati ya kukusanya
mapato kama ilivyoelezwa kwenye hotuba ya bajeti ambayo ni pamoja na kuwa na
mikataba ya kiutendaji na Mamlaka ya Mapato (TRA) kuhakikisha watendaji
wanafikia malengo na baada ya kuona mafanikio yake ndipo uamuzi wa pili wa
kupunguza kiwango fulani cha utegemezi na hali kuendelea hivyo hadi pale
tunapoona tumepunguza kwa kiasi kikubwa.
Juhudi za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima pia
zinatakiwa zifanyike kwa upana wake katika kuhakikisha kile kinachopatikana
kinatumiwa vizuri na kwa shughuli zilizokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment