Image
Image

Msitoe ardhi yenu kabla hamjalipwa fidia - Kinana.


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewatahadharisha wananchi kuacha kutoa maeneo yao kabla hawajalipwa fidia pindi wanapoletewa miradi ya kupanua miji na halmashauri zao.
Kinana alisema hayo juzi akiwa mjini hapa wakati akiendelea na ziara yake mkoani Kagera na kupata malalamiko juu ya kutotendewa haki miradi hiyo inapofanywa katika mashamba yao.
“Msikubali kuyaachia mashamba yenu kabla hamjalipwa fidia. Lazima mpewe mkono kwa mkono na siyo vinginevyo, Serikali haiwezi kutekeleza mradi kama haina fedha za kutosha kuwalipa,” alisema Kinana.
Katika Kijiji cha Nyakisasa alikozindua chanjo ya watoto pamoja na nyumba ya watumishi wa zahanati ya kata hiyo, Kinana aliwataka wananchi kuachana na imani za kishirikina bali wajitokeze kuwapeleka watoto na wajawazito kupata chanjo katika vituo vya afya.
Alitoa wito huo baada ya kupokea taarifa kuwa licha ya uwapo wa zahanati hiyo, mahudhurio siyo ya kuridhisha ingawa idadi ya wanaohitaji chanjo na tiba ni kubwa.
“Kinamama hamuwaleti watoto wenu kupata chanjo na kwa kadri nijuavyo wengi wenu mnaamini sana imani za kishirikina,” alisema Kinana na kuongeza:
“Achaneni na imani hizo, lengo la chanjo hizi ni kuimarisha afya zenu na watoto pia.”
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akihutubia mkutano huo, aliwataka wananchi kuachana na ushabiki wa kisiasa kwani madhara yake kwao ni makubwa.
Akirejea vurugu zilizotokea katika eneo hilo wakati wa mjadala wa Katiba Mpya, aliwakumbusha kuwa mchakato huo una manufaa zaidi kwa wanasiasa wakubwa na endapo mambo yataenda kombo, watakaoumia ni wananchi wa kawaida.
“Katiba ni mradi wa wanasiasa kugawana madaraka. Ipite au isipite wakubwa hao watakuwa Dar es Salaam wakigongeana glasi huku wewe ukishuhudia kupitia runinga. Tuwaache wao waendelee na suala hilo na sisi tufanye ya kwetu,” alisema Nape.
Aliwaasa kuachana na vurugu za kukatiana migomba, kuchoma nyumba za ibada pamoja na kujeruhiana na badala yake waendeleze mshikamano katika kujiletea maendeleo.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment