Lowassa aliwasili Zanzibar juzi akitokea jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini wa kumdhamini ili agombee urais kupitia CCM.
Lowassa na ujumble wake waliingia Zanzibar kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume saa 1:30 jioni, ambapo alipokewa kwa shangwe na wana CCM, vikundi vya ngoma, waendesha pikipiki na magari na kuelekea mjini.
Jana alitembelea ofisi ya makao makuu ya CCM ya Kisiwandui na kupokewa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini, Borafya Silima, ambapo alitia saini kitabu cha wageni kisha akaelekea kwenye kaburi la hayati Abeid Karume lililopo karibu na ofisi hiyo.
Alitembelea pia ofisi ya CCM Mkoa wa Mjini alikopewa saini za wanachama 90 katika wilaya za Mjini na Amani.
Akizungumza katika ofisi ya Mkoa wa Magharibi, Lowassa aliwataka wanachama kuchagua mgombea anayefaa kuwa mwenyekiti wa chama, huku pia akisisitiza kuyaenzi mapinduzi ya Zanzibar.
Alipofika katika wilaya za Mfenesini na Dimani, alisema:
“La kwanza nawashukuru kwa kunidhamini na ninaahidi kutowaangusha. Unapochagua rais, unachagua pia mwenyekiti wa CCM, unapochagua Rais wa Zanzibar unachagua makamu mwenyekiti wa chama. Tutafute mtu anayekijua chama, maana kuna watu wamechupia tu.
“Nathamini Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano. Kuna watu wanabeza Muungano, mimi ninaahidi kuulinda.”
Lowassa alisema lengo la kugombea urais ni kutetea sera ya CCM ya kupambana na umasikini.
“Nimeamua kugombea urais ili nipambane na umasikini, nachukia umasikini. Nimekuwa mwanachama wa CCM kwa karibu nusu ya umri wangu. Nataka kutekeleza sera ya CCM ya kupambana na umasikini,” alisema.
Lowassa alitembelea mikoa ya Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini na Mkoa wa Kusini ambako kote alipata saini 360 za wana CCM.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, mgombea anatakiwa kukusanya saini ya saini 450 kutoka mikoa 15 ambapo kati yao mitatu inatoka Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment