Kansela Angela Merkel alianza siku kwa
kumuonyesha ukarimu Rais Barack Obama katika tafrija ya jadi ya jimbo la
Bavaria la kubwia pombe na kitafunio cha mkate maalum kwenye bustani huku
wakibirudishwa na muziki unaopigwa na wenyeji waliovalia suruali za ngozi.
Lakini baada ya kutabasamu kwenye mwanga wa
jua viongozi wote wawili wametowa onyo kali kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi
juu ya kile Obama alichokisema kuwa ni "uchokozi" wake nchini
Ukraine.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imesema
viongozi hao wamekubali kwamba muda wa vikwazo unapaswa dhahir kufungamanishwa
na utekelezaji wa Urusi kikamilifu wa makubaliano ya amani ya Minsk na
kuheshimu uhuru wa Ukraine ikimaanisha makubaliano yaliofikiwa katika mji mkuu
wa Belarus.
Makaribisho ya kitamaduni na kuonyesha umoja
ulioko kati ya Ujerumani na Marekani havikuendana kabisa na msimamo wa viongozi
hao kwa Urusi ambao haukujumuishwa kwenye mazungumzo yao.
Msimamo mmoja dhidi ya Urusi
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Donald
Tusk ambaye pia anahudhuria mkutano huo unaofanyika kwenye jengo la ngome ya
Elmau eneo la mapumziko likiwa chini ya ulinzi mkali amesema anataka
kuyakinisha suala la umoja wa Kundi la G7 kuhusiana na sera za vikwazo dhidi ya
Urusi ambapo amesema itaendelea kubakia nje ya kundi hilo kwa kadri itakapokuwa
inaendeleza vitendo vyake vya ubabe kwa Ukraine na nchi nyengine.
Viongozi wa Japani na Canada walihakikisha
kwamba wanazuru Kiev mji mkuu wa Ukraine wakati wakiwa safarini kuja Ujerumani
hapo Jumamosi kuelezea uungaji mkono wao viongozi wa Ukraine wakati vikosi vya
serikali vikishambuliana tena na waasi mashariki mwa nchi hiyo,
Obama amesema kabla ya mazungumzo yake na
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kwamba suala kuu katika mkutano huo
"litakuwa ni kusimama kidete dhidi ya uchokozi wa Urusi nchini
Ukraine."Francois Hollande wa Ufaransa,Matteo Renzi wa Italia, Stephen
Harper wa Canada na Shinzo Abe wa Japani wanahuhuria mkutano huo.
Hofu ya kuvunjika makubaliano Ukraine
Kuzuka upya kwa mapigano mashariki mwa
Ukraine hivi karibuni kumesababisha watu 28 kupoteza maisha yao na kuzusha hofu
kwamba kupamba moto huko kwa mapigano kutavuruga makubaliano ya kusitisha
mapigano yaliopatikana kwa taabu chini ya usimamizi wa Ufaransa na Ujerumani
kwa miezi minne.
Obama bila ya kuitaja kwa jina Ugiriki
iliokumbwa na mzozo wa kiuchumi pia amegusia matatizo yanayoendelea kuwepo kati
ya Umoja wa Ulaya na Ugiriki ilioelemewa na mzigo wa madeni kwa kutaja kwamba
mada za juu katika mkutano huo wa kilele ni uchumi wa dunia ambao unazalisha
ajira na kuleta fursa na kuendelea kuufanya Umoja wa Ulaya uwe madhubuti na
wenye neema.
Merkel anayatetea mageuzi magumu na kubana
matumizi ili Ugiriki iweze kupatiwa mikopo amefanya juhudi za mwisho kuupatia
ufumbuzi mzozo huo wa Ugiriki siku chache kabla ya mkutano huu wa Kundi la
Mataifa Saba ambapo amekuwa na mashauriano na viongozi wa Shirika la Fedha la
KImataifa (IMF) Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya mjini
Berlin.
Suala la Ugiriki linatishia kuugubika mkutano
huo wa kilele ambao Merkel alitaraji kulenga kwenye matatizo mengine makuu
kuanzia na mabadliko ya tabia nchi na Waislamu wa itikadi kali,haki za wanawake,miradi
ya afya kwa wananchi na vita dhidi ya umaskini.
Siku moja baada ya kunadamana dhidi ya kundi
hilo la G7 katika maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani
waandamanaji kadhaa Jumapili walikuwa wamezinga njia kuelekea kwenye kasri ya
ngome ya Elmau unakofanyika mkutano huo jambo ambalo limepelekea waandishi
kupelekwa kwa helikopta kwenye eneo la mkutano huo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/AP
0 comments:
Post a Comment