Uamuzi huo ulitolewa baada ya Spika wa Baraza
hilo, Pandu Ameir Kificho kutoa utangulizi kwa wajumbe akiwataka
watengue kanuni ili viongozi wa kitaifa watakaohudhuria shughuli hiyo
waweze kuingia ukumbini badala ya kukaa sehemu ya kawaida ya wageni
waalikwa.
Baada ya kutoa utangulizi, Spika Kificho alianza
kuwahoji wajumbe wanaokubali viongozi wa kitaifa waruhusiwe kuingia
ndani ya Ukumbi wa Baraza kwa kuwataja wakiwamo Rais wa Zanzibar, Jaji
Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, mpambe wa Rais na kuungwa mkono
kwa kupigiwa makofi na sauti za ndiyo.
Hata hivyo, alipomtaja Makamu wa Kwanza wa Rais,
Maalim Seif Sharif Hamad wajumbe wote waliokuwapo katika Baraza hilo,
ambao wote ni wa CCM, walikataa wakisema kwa sauti “hapana,” kitendo
ambacho kilimfanya Spika kurudia kutamka jina hilo kwa zaidi ya mara
tatu na majibu yalikuwa hapana.
Hatua ya wawakilishi kumkataa Maalim Seif, imekuja
siku moja baada ya mawaziri na wajumbe wa CUF kutoka nje ya Baraza
wakisusa kujadili na kupitisha muswada wa sheria wa bajeti kuu ya
matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16 wakipinga pamoja na mambo
mengine, mchakato unaoendelea sasa wa uandikishaji wapigakura katika
Daftari la Kudumu.
“Mnakubali kutengua kanuni kuruhusu viongozi wa
kitaifa kuhudhuria katika shughuli yetu ndani ya ukumbi? Wageni wetu ni
Rais wa Zanzibar, mpambe wake, Jaji Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais,”
alihoji Spika Kificho lakini alipingwa baada ya kulitaja jina la Makamu
wa Kwanza wa Rais.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliwasilisha hati ya Serikali kuhusu
marekebisho ya kanuni za Baraza.
Waziri Aboud alisema, Rais wa Zanzibar atakagua
gwaride maalumu la Polisi kabla ya kuhutubia Baraza hilo saa 9.30
alasiri na kuwataka wajumbe wote kufika kabla ya kuwasili kwa Rais.
Kuhusu uamuzi wa kumkataa Maalim Seif, Aboud
alisema upo katika mamlaka ya wajumbe kwa mujibu wa kanuni za Baraza
hilo na kwamba hatua itakayofuata ni Spika kumwandikia barua Maalim Seif
ya kutohudhuria shughuli hiyo ili kulinda uamuzi wa baraza hilo.
“Baraza ni chombo cha kikatiba, Serikali hatuna
uwezo wa kuliingilia na kanuni ndivyo zinavyosema. Wageni ambao ni
viongozi wa kitaifa lazima utengue kanuni kwa kuwauliza wajumbe kama
wanakubali au kukataa,” alisema.
Waziri Aboud alisema SMZ haitaongeza muda wa
Baraza ili kutoa nafasi ya Mwakilishi wa Kwa Mtipura (CCM), Hamza Hassan
Juma kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka wananchi waulizwe kama wanataka
kuendelea na mfumo wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au la
akisema kwa mujibu wa ratiba ya kikao cha bajeti, muda umemalizika na
kumtaka kuangalia hoja yake katika siku za baadaye.
0 comments:
Post a Comment