Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja tangu baadhi ya wanasiasa
wa chama cha CCM na wa upinzani waanze kutangaza azma yao ya kuwania
urais, mikakati mingi imetajwa ya kimaendeleo wanayoamini itaibadilisha
Tanzania kufikia malengo ya nchi ya kipato cha kati.
Kila kada aliyeweza kupata fursa ya kuhutubia
mkutano wa hadhara au kuzungumza na wanahabari, amejaribu kubainisha
masuala mbalimbali ya kiuchumi, siasa na kijamii ambayo anaamini akipata
ridhaa ya chama chake na wananchi atayasimamia.
Tayari kuna zaidi ya makada 35 kutoka CCM na watatu kutoka upinzani ambao wamebainisha kuwania kiti hicho cha juu nchini.
Walichosahau
Hata hivyo, mbali na mikakati na ahadi tamutamu za
awali walizozitoa, wengi wameshindwa kubainisha au hata kueleza kwa
kina baadhi ya mambo mtambuko kama vipaumbele vyao kiasi cha kuwafanya
wananchi au wanahabari kuwauliza iwapo siyo masuala ya msingi kwao au
la.
Pamoja na ukweli kwamba bado ilani za vyama vingi
kwa ajili ya uchaguzi huu hazijatolewa rasmi, watiania hao
wangeyazungumzia pia masuala hayo kama vipaumbele vyao kama walivyofanya
kwa mambo mengine.
Baadhi ya masuala hayo makubwa ambayo watiania hao
‘wamekwepa’ kuyataja au kueleza kwa kina ni pamoja na utunzaji wa
mazingira, michezo na utamaduni, mahusiano ya kimataifa na diplomasia ya
uchumi na mfumo mzima wa afya hususan Ukimwi.
Diplomasia ya kiuchumi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim
anasema asilimia kubwa ya watiania wamezungumza vitu vya kawaida japo
vinagusa maisha ya watu, huku msisitizo ukiwa kwenye mambo ya ndani ya
nchi kuliko nafasi ya Tanzania dhidi ya nchi nyingine kupitia diplomasia
ya uchumi.
“Tanzania siyo kisiwa ilibidi msisitizo uwekwe
namna nchi itakavyoshirikiana kisiasa na kiuchumi na Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Comesa, na jumuiya nyingine ulimwenguni kwa kuonyesha namna
ambavyo Watanzania watatumia fursa zilizopo kujiendeleza kupitia
diplomasia ya uchumi,” anasema Salim ambaye ni mtaalamu wa masuala ya
ushirikiano wa kimataifa.
Mbali na watiania hao kushindwa kutilia mkazo
suala la diplomasia ya uchumi, baadhi yao pia wameshindwa kuainisha kwa
kina namna watakavyobadili mfumo wa katiba na kutunza mazingira kama
anavyoeleza Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Patience Mlowe.
Mlowe anasema wagombea wengi wanazungumzia
kuulinda Muungano bila kueleza namna wakavyolivalia njuga suala la
Katiba Mpya ambalo kwa sasa limeligawa taifa na ndiyo msingi wa Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment