MWEZI Mei mwaka huu madereva wa vyombo vya usafirishaji katika maeneo
mbalimbali nchini walifanya mgomo wa kutotoa huduma za usafiri kwa
madai ya kutakiwa kurudi vyuoni kwa mafunzo zaidi ya usalama barabarani.
Hali ya mgomo huo ulisababisha adha kubwa kwa abiria wa vyombo hivyo,
hasa wale waliokuwa wakielekea mikoani, kwani katika Stendi Kuu ya
Mabasi ya Ubungo jijini Dar es Salaam, hakuna basi hata moja
lililoondoka huku daladala nazo zikiwa hazionekani kabisa vituoni.
Uongozi wa madereva walidai kuwa hawawezi kurudi mafunzoni kwani kazi
wazifanyazo si za kudumu na hivyo watakaporudi mafunzoni hali ya maisha
yao itatetereka, kutokuwa na uwezo wa kulipa ada na mengineyo.
Baada ya kutoa sababu hiyo Serikali na wamiliki waliingilia kati na
kukubali kuwalipia ada ya mafunzo hayo waliyotakiwa kufanya mara tu
leseni inapoisha yaani miaka mitatu na baadaye suala hilo likasitishwa.
Lakini baada ya kusitishwa kwa agizo hilo bado waliendelea kugoma na
kubadili madai yao kwa kusema wanahitaji Serikali kukaa na wamiliki na
kupatiwa mikataba ya kudumu ya kazi zao ambapo wamiliki walikubali.
Sasa wanatishia kugoma wakiwa na madai kuwa mikataba ya ajira
waliyopatiwa na wamikili Mei 19 mwaka huu yametolewa mambo muhimu ambayo
ni bima ya ajali, kodi ya nyumba, matibabu, usafiri, likizo na nauli ya
kila siku baada ya kazi.
Wamedai kuwa ikiwa Serikali haitakubaliana na wamiliki kurudisha
mambo hayo kwenye mikataba watafanya mgomo kuanzia Ijumaa, jambo ambalo
limepingwa na wamiliki wa mabasi nchini na kueleza watakaogoma wakati
mazungumzo yanaendelea watafukuzwa kazi.
Naunga mkono wamiliki waliotoa kauli bila kusita kwani madereva
wameonesha jinsi wamekosa shukrani licha ya kusikilizwa madai ya kila
walipotoa.
Ni dhahiri kuwa hata kama madai yao yangekuwa yana msingi, jambo la
kujiuliza ni kuwa hawana njia nyingine ya kutatua matatizo hayo bila ya
kufanya mgomo ambao unawaathiri wananchi ambao hawana uwezo wa kutimiza
matakwa yao?
Ikiwa wameweza kupatiwa mikataba ya ajira zao kwa nini wanashindwa
kuwa wavumilivu na kufuatilia wakati wamiliki wamekubali kufanya
mazungumzo na jambo la kujiuliza ni wafanyakazi wangapi nchini wanapata
mahitaji hayo wanayotaka.
Ili kudhibiti suala hilo ni vema mamlaka husika liwemo Jeshi la
Polisi kitengo cha Usalama Barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na Mamlaka nyinginezo kuingilia kati na
kuacha kuwabembeleza madereva hao kwa kuchukua hatua stahili. Kwa
hakika, migomo siyo suluhu la matatizo yoyote isipokuwa kukaa na mamlaka
husika.
Ni vema kuangalia suala hilo kwa hekima na undani ili kuwaondolea
usumbufu wananchi pale inapotokea mgomo kwa kuwapa mahitaji yao stahili
na ikiwa majadiliano yanaendelea ni vema kuwaeleza ili kuondoa jazba.
Kwani kusubiri wagome ndipo wasikilizwe matatizo yao ni hatari kwani
inakuwa tayari madhara mengi yamepatikana kwa wananchi wanaotegemea
usafiri wa umma, hivyo ni vema kusikilizwa nao kuelewa wanachoelezwa
bila kutoa vitisho vya kugoma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment